Paul Scholes amkataa Michael Carrick Man United
Muktasari:
- Katika ukurasa wake wa Instagram, Scholes aliikosoa Man United baada ya kiwango kibovu ilichocheza na kushindwa kutumia vyema kadi nyekundu ya Jacob Ramsey iliyotolewa kipindi cha kwanza.
MANCHESTER, ENGLAND: NYOTA wa zamani wa Manchester United, Paul Scholes amemrushia dongo Kocha wa Manchester United, Michael Carrick baada ya timu hiyo kupoteza kwa mabao 2-1 dhidi ya Newcastle United, licha ya wapinzani wao kubaki na wachezaji 10.
Katika ukurasa wake wa Instagram, Scholes aliikosoa Man United baada ya kiwango kibovu ilichocheza na kushindwa kutumia vyema kadi nyekundu ya Jacob Ramsey iliyotolewa kipindi cha kwanza.
"Michael bila shaka ana kitu cha kipekee ndani yake kinachomwezesha kushinda … kwa sababu Man United imekuwa mbovu sana katika mechi nne zilizopita."
Scholes na Carrick walicheza mechi 160 pamoja katika kikosi cha Man United kati ya mwaka 2006 na 2013, wakitwaa mataji manane makubwa yakiwemo matano ya Ligi Kuu England na moja la Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Carrick aliajiriwa na Man United kwa muda baada ya klabu hiyo kumfuta kazi Ruben Amorim mwanzoni mwa Januari na tangu achukue mikoba matokeo yanaonekana kuimarika.
Carrick mwenyewe alikiri kutoridhishwa na kiwango kilichoonyeshwa na mastaa wake kwenye Uwanja wa St James’ Park.
"Hatujaridhishwi na uchezaji wetu wa leo. Mchezo ulikuwa mikononi mwetu kwa kiasi kikubwa, lakini nitoe pongezi kwa Newcastle. Tulikuwa katika nafasi nzuri za kufunga lakini hatukufanya hivyo."
“Sidhani kama ilikuwa suala la wao kubaki na watu 10, ukweli ni sisi hatukuwa wazuri vya kutosha. Hakuna visingizio, kila mmoja wetu anawajibika."
Awali, Roy Keane alishamkataa Carrick akisema anakosa maarifa ya soka ya kuiongoza Man United na sasa Scholes anaonekana kuwa na mtazamo unaofanana.
Akizungumza kwenye podikasti yake The Good, The Bad and The Football wiki hii, Scholes alimtaja Carlo Ancelotti kama mtu sahihi ambaye klabu inapaswa kumfuata na kumpa kazi baada ya Kombe la Dunia lijalo kumalizika.