Ancelotti ataja mechi nne zilizompa presha Real Madrid
Muktasari:
- Ancelotti alikuwa kocha wa Real Madrid kabla ya kuondoka miezi michache iliyopita na kwenda kuiongoza timu ya taifa ya Brazil. Kocha huyo raia wa Italia alishinda mataji kadhaa, ikiwemo Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa na klabu hiyo ya mjini Madrid.
Kocha mkuu wa timu ya taifa ya Brazil, Carlo Ancelotti, ametaja mechi nne zilizompa ‘presha’ katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya (UEFA Champions League) ambayo Real Madrid hawataisahau kamwe.
Ancelotti alikuwa kocha wa Real Madrid kabla ya kuondoka miezi michache iliyopita na kwenda kuiongoza timu ya taifa ya Brazil. Kocha huyo raia wa Italia alishinda mataji kadhaa, ikiwemo Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa na klabu hiyo ya mjini Madrid.
Akizungumza na mwandishi wa habari wa Hispania, Tomás Roncero, Ancelotti amesema mechi dhidi ya Chelsea, Bayern Munich, Manchester City, na Paris Saint-Germain (PSG) zitabaki kwenye kumbukumbu zake na anaamini hata baadhi ya mashabiki Los Blancos hawatazisahau milele.
“Ukirudia nyuma, tulikuwa na nyakati za ajabu, miaka ya kushangaza. Sio kwa sababu ya taji pekee, bali kwa kila kitu kilichohitajika kushinda,” amesema Ancelotti kupitia AS.
“Kurudi nyuma katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya ni kumbukumbu zisizosahaulika. Tukirudi kwenye mechi dhidi ya PSG, Chelsea, Man City, Bayern Munich huko Bernabéu hazitasahaulika kamwe, hakuna mtu atakayesahau mechi hizo na zitabaki kwenye vichwa vyetu milele.”
Katika msimu wa 2021-2022 wa Champions League, Real Madrid ilipoteza 1-0 dhidi ya PSG katika raundi ya 16, lakini ilishinda 3-1 katika mechi ya mkondo wa pili iliyochezwa Santiago Bernabéu.
Pia katika msimu huohuo, Real Madrid ilishinda 3-1 dhidi ya Chelsea katika mechi ya kwanza ya robo fainali Stamford Bridge, lakini ililazimika kutoka nyuma baada ya kutanguliwa kwa 3-0 katika mechi ya mkondo wa pili, ikafunga mabao mawili, ikapoteza kwa 3-2, lakini ikasonga mbele kwenye hatua inayofuata kwa jumla ya mabao 5-3.
Aidha, katika nusu fainali ya msimu huo, Real Madrid ilipoteza 4-3 dhidi ya Manchester City katika mechi ya kwanza, lakini ikashinda 3-1 katika mechi ya mkondo wa pili na kufuzu fainali kwa jumla ya mabao 6-5.
Katika kampeni ya msimu wa 2023-2024, Real Madrid ilipata sare ya 2-2 na Bayern Munich katika mechi ya kwanza ya nusu fainali, lakini ilishinda 2-1 kwenye mechi ya mkondo wa pili iliyopigwa Santiago Bernabéu. Ikawa imepata ushindi wa jumla 4-3.