Man United yavamia dili la Viktor Gyokeres
Muktasari:
- Hadi sasa Arsenal na Sporting zimeshindwa kufikia mwafaka juu ya namna ya kulipana pesa ya nyongeza na Sporting inataka kurahisishwe masharti ya ulipaji.
LICHA ya mchezaji mwenyewe kuonyesha nia ya kutaka kujiunga na Arsenal pekee, inaelezwa Manchester United imeingia katika vita dhidi ya Arsenal na kutaka kuwasilisha ofa ili kuipata huduma ya straika wa Sporting Lisbon na timu ya taifa ya Sweden, Viktor Gyokeres, mwenye umri wa miaka 27, katika diriha hili.
Hadi sasa Arsenal na Sporting zimeshindwa kufikia mwafaka juu ya namna ya kulipana pesa ya nyongeza na Sporting inataka kurahisishwe masharti ya ulipaji.
Ripoti zinaeleza hadi sasa zimepita siku saba tangu mara ya mwisho mabosi wa Arsenal walipowasiliana na Sporting kuhusu Gyokeres.
Mkataba wa staa huyu unatarajiwa kumalizika mwaka 2028 na amegoma kabisa kurejea kwenye kikosi cha Lisbon na kusisitiza anahitaji kujiunga na Arsenal dirisha hili.
Gyokeres amegoma kurejea kwenye kikosi cha Lisbon kwa sababu anadaiwa timu hiyo imekiuka makubaliano waliyoweka dirisha la majira ya baridi mwaka huu ambayo ilikuwa ni kumruhusu kuondoka kwa kiasi cha chini tofauti na kile ambacho kipo katika mkataba.
Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta alihitaji dili la staa huyu likamilike katika wiki iliyopita ili kuweza kumjumuisha katika kikosi kinachosafiri kwenda Asia kwa ajili ya maandalizi ya msimu ujao.
Armand Lauriente
SUNDERLAND imejiondoa kwenye dili la kumsajili mshambuliaji wa Sassuolo, Mfaransa Armand Lauriente, mwenye miaka 26, dirisha hili. Staa huyu ambaye Sunderland ipo tayari kumuuza kwa Pauni 17.5 milioni katika dirisha hili, mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2027. Msimu uliopita Serie B, alicheza mechi 40 za michuano yote, amefunga mabao matano na kutoa asisti sita. msimu uliopita alicheza mechi 33 na kufunga mabao 18.
Renato Veiga
ATLETICO Madrid imeripotiwa kuwasiliana na Chelsea ili kuulizia uwezekano wa kuipata saini ya beki wa kati wa timu hiyo, Renato Veiga katika dirisha hili. Atletico inamwona fundi huyu kama chaguo sahihi na la bei rahisi kwao ukilinganisha na wachezaji wengine lakini itawahitaji kushinda vita ili kumpata. Kwa mujibu wa ripoti, Veiga anauzwa kwa Pauni 26 milioni hadi Pauni 30 milioni, hivyo timu ambayo itaweka ofa nono ndio inaweza kupata huduma yake. Veiga ana umri wa miaka 21.
Gabriel Martinelli
Al-Nassr inafikiria kuhamishia nguvu zao kwa winga wa Arsenal na timu ya taifa y Brazil, Gabriel Martinelli, 24, baada ya mchakato wa kuipata saini ya mshambuliaji wa Liverpool na timu ya taifa ya Colombia, Luis Diaz, 28, kuwa na ugumu sana. Licha ya kutoonyesha kiwango bora sana msimu uliopita wa Ligi Kuu England, haionekani kama itakuwa rahisi kwa Arsenal kumwachia Martinelli.
Oleksandr Zinchenko
AC Milan wanataka kumsajili beki wa Arsenal na Ukraine, Oleksandr Zinchenko, mwenye umri wa miaka 28, ambaye hapati nafasi ya kutosha katika kikosi cha kwanza cha Arsenal, hali inayosababisha atamani kuondoka dirisha lijalo kujiunga na timu itakayompa nafasi kubwa zaidi ya kucheza. Mbali ya Milan, timu kadhaa za ndani ya England zimetuma maomba ya kumsajili kwa mkopo.
Jorrel Hato
ARSENAL bado inafanya mazungumzo na Ajax ili kuipata huduma ya beki wa kati wa klabu hiyo na Uholanzi, Jorrel Hato, mwenye umri wa miaka 19. Inaelezwa baadhi ya wawakilishi wa Arsenal walisafiri tena mwanzoni mwa mwezi huu kwenda Uholanzi kwa ajili ya kufanya mazungumzo zaidi juu ya beki huyu. Benchi la ufundi la Arsenal linapambana kuboresha kikosi chao kuhakikisha wanafanya vizuri kwa msimu ujao.
Cody Gakpo
BAYERN Munich bado inahitaji kumsajili mshambuliaji wa Liverpool, Cody Gakpo, 26, katika dirisha hili ikiwa ni katika mpango wa kusuka safu yao ya ushambuliaji. Awali Bayern ilikuwa ikitajwa kutaka kumsajili winga wa kimataifa wa Hispania anayeichezea Athletic Bilbao, Nico Williams, 22, kabla hajasaini mkataba mpya wa kuendelea kusalia katika timu yake.
Maxime Esteve
BURNLEY imeendelea kushikilia msimamo wao wa kuhitaji Pauni 50 milioni ili kumuuza beki wao, Maxime Esteve,23, anayewindwa sana na Bayern Munich. Inaelezwa kocha wa Bayern, Vincent Kompany ni shabiki mkubwa wa staa huyu ambaye aliwahi kumfundisha akiwa Burnley. Mkataba wake unamalizika mwaka 2029.