Man United yaichokoza Arsenal
Muktasari:
- Chipukizi Lewis-Skelly, ambaye pia ni mchezaji wa timu ya taifa ya England, ametolewa kwa Manchester United na Chelsea huku Arsenal ikielezwa kuwa tayari kusikiliza ofa zinazofikia pauni60 milioni.
LONDON, England: MANCHESTER United imeanza mpango wa kumsajili kwa kushtukiza beki wa Arsenal, Myles Lewis-Skelly, huku mustakabali wa kinda huyo mwenye umri wa miaka 19 akiwa hana uhakika wa namba ndani Emirates.
Chipukizi Lewis-Skelly, ambaye pia ni mchezaji wa timu ya taifa ya England, ametolewa kwa Manchester United na Chelsea huku Arsenal ikielezwa kuwa tayari kusikiliza ofa zinazofikia pauni60 milioni.
Hata hivyo, United inaona thamani hiyo kuwa kubwa na haijawa tayari kufikia kiwango hicho cha fedha.
Klabu hiyo ya Old Trafford inamchukulia Lewis-Skelly kama chaguo la beki wa kushoto baada ya kukutana na ugumu katika juhudi zake za kumnunua Lewis Hall kutoka Newcastle United.
Man United tayari imekuwa ikiona baadhi ya wachezaji inayowalenga ndani ya Ligi Kuu England wakiwa na bei kubwa, hali iliyosababisha klabu hiyo kuwa makini katika matumizi yake ya fedha kwenye dirisha hili la usajili.
Hadi sasa, Man United imetumia takribani pauni milioni 85 katika kuwasajili Andrey Santos na Youri Tielemans. Tielemans alijiunga na United baada ya klabu hiyo kuvurugikiwa mpango wa kumsajili kiungo wa Atalanta, Ederson, huku akiwa na kipengele cha kuvunja mkataba cha pauni milioni 35 akiwa Aston Villa.
Lewis-Skelly amekuwa akihusishwa na uwezekano wa kuondoka Arsenal baada ya klabu hiyo kuimarisha safu yake ya kiungo kwa kumsajili Bruno Guimaraes kwa pauni milioni 75 mwishoni mwa wiki.
Ingawa nafasi yake kuu ni beki wa kushoto, Lewis-Skelly pia ana uwezo wa kucheza kama kiungo mkabaji, eneo ambalo Manchester United inataka kuliongezea nguvu.
Vyanzo vinaeleza kuwa uhamisho huo unaweza kuwa mgumu kutokana na mawakala kadhaa kujaribu kusaidia kufanikisha dili hilo.
Lewis-Skelly anawakilishwa na mama yake, Marcia, ambaye amekuwa akisimamia kwa umakini maendeleo ya mwanaye tangu alipokuwa mwanafunzi.
Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta, alimpa Lewis-Skelly nafasi chache mwanzoni mwa msimu uliopita, ambapo alicheza mechi mbili tu za Ligi Kuu England katika miezi minane ya kwanza kutokana na wasiwasi kuhusu kiwango chake cha ukomavu.
Hata hivyo, hali ilibadilika mwishoni mwa msimu, ambapo alianza katika mechi tano kati ya sita za mwisho za Arsenal, ikiwemo mchezo wa nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Atletico Madrid ambao Arsenal ilishinda, pamoja na fainali iliyopoteza dhidi ya Paris Saint-Germain.
Chelsea pia imepewa nafasi ya kumsajili Lewis-Skelly baada ya beki wao wa kushoto, Marc Cucurella, kujiunga na Real Madrid.
Manchester United inahitaji beki wa kushoto kutokana na Luke Shaw, mwenye umri wa miaka 31, kuelekea kumaliza mkataba wake mwakani.
United imekuwa ikimfuatilia Lewis-Skelly kwa miezi kadhaa, lakini awali ilimchukulia Lewis Hall kama chaguo bora zaidi.