Man United mfumo umekubali
Muktasari:
- Matheus Cunha alifunga bao lake la kwanza Man United kwenye ligi tangu alipojiunga akitokea Wolves wakati wa dirisha lililopita la majira ya kiangazi.
MANCHESTER, ENGLAND: MANCHESTER United gari limewaka. Ndicho unachoweza kusema baada ya kikosi hicho cha kocha Ruben Amorim kushinda mechi ya tatu mfululizo kwenye Ligi Kuu England ilipoichapa Brighton 4-2 uwanjani Old Trafford.
Matheus Cunha alifunga bao lake la kwanza Man United kwenye ligi tangu alipojiunga akitokea Wolves wakati wa dirisha lililopita la majira ya kiangazi.
Cunha alifunga kwa shuti la chinichini dakika ya 24 kufuatia pasi ya Mbrazili mwenzake, Casemiro. Baadaye, Casemiro, ambaye alipika bao la kwanza alifunga la pili dakika 10 baadaye.
Shuti la Casemiro lilimbabatiza Yasin Ayari mgongoni na kumpoteza kipa wa Brighton, Bart Verbruggen na hivyo mpira kutinga kwenye nyavu.
Staa mwingine mpya wa Man United, Bryan Mbeumo alifunga bao la tatu na kuiweka timu hiyo kwenye uhakika wa kushinda mchezo wa tatu mfululizo kwenye ligi.
Kocha Amorim baada ya kuwatoa wachezaji muhimu, Brighton ilizinduka na kufunga mara mbili, Danny Welbeck kwa mpira wa adhabu, uliomshinda kipa Senne Lammens kabla ya Charalampos Kostoulas kufunga kwa kichwa mpira wa kona uliopigwa na James Milner katika dakika za majeruhi za kipindi cha pili.
Presha ilikuwa kubwa kwa Man United baada ya ubao wa matokeo kusomeka 3-2. Lakini, Mbeumo alihakikishia miamba hiyo ya Old Trafford ushindi usioshaka baada ya kufunga bao la nne na la pili kwake kwenye mchezo huo katika dakika ya mwisho kabisa ya mechi.
Ushindi huo uliifanya Man United kupanda hadi nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi, ikivuna pointi 16 katika mechi tisa.