Man United kuvunja benki kusaka washambuliaji
Muktasari:
- Kocha huyo mpya wa Manchester United yupo tayari kufungulia pochi kwa kiwango chochote kile ambacho atapewa na bilionea Sir Jim Ratcliffe kwenye dirisha hili la uhamisho wa wachezaji la Januari.
LONDON, ENGLAND: RUBEN Amorim atalazimika kuvunja benki kupata washambuliaji wenye uwezo wa kufunga mabao wakakipige Old Trafford.
Kocha huyo mpya wa Manchester United yupo tayari kufungulia pochi kwa kiwango chochote kile ambacho atapewa na bilionea Sir Jim Ratcliffe kwenye dirisha hili la uhamisho wa wachezaji la Januari.
Amorim anataka wachezaji ambao wamekuwa na mwendelezo wa kupasia mipira nyavuni na hao ndio waliopo kwenye orodha ya bidhaa anazotaka kocha huyo.
Majina ya mastaa wanne yamewekwa ubaoni kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya baridi lililofunguliwa Januari 1 - na kinachotazamwa ni mchezaji gani kwenye orodha hiyo atakwenda kufiti moja kwa moja kwenye mtindo wa kiuchezaji wa miamba hiyo ya Old Trafford.
Kinachoelezwa ni kwamba Marcus Rashford amewekwa kwenye mpango wa kubadilishwa na straika wa Napoli, Victor Osimhen.
Osimhen, 26 ni mshambuliaji wa kimataifa wa Nigeria mwenye uwezo mkubwa wa kufunga mabao na sasa anakipiga kwa mkopo Galatasaray, alikojiunga akitokea Napoli kwenye dirisha lililopita la uhamisho wa majira ya kiangazi. Na fowadi huyo alitimkia Uturuki baada ya kukwama kujiunga na Chelsea na Saudi Pro League kwenye siku ya mwisho ya kufungwa kwa dirisha la majira ya kiangazi mwaka jana na hakuwa tayari kubaki Naples.
Amefunga mabao 13 katika mechi 16 msimu huu huku akiwa na wastani wa bao 0.79 kwa kila dakika 90 tangu kuanza kwa msimu uliopita. Na Man United inaweza kumpata Osimhen kwa Pauni 62 milioni kwenye dirisha hili la Januari kutokana na kipengele kilichowekwa kwenye mkataba wake, licha ya kwamba mshahara wake unaweza kuwa mkubwa.
Kocha Amorim atapenda pia kufanya kazi na mshambuliaji wake wa zamani waliyekuwa pamoja Sporting Lisbon, Viktor Gyokeres, lakini kinachoelezwa ni kwamba kulikuwa na makubaliano ya kuzuiwa kwenda kusajili mchezaji kwenye timu hiyo kwenye dirisha hili hadi itakapofika mwisho wa msimu. Gyokeres, ambaye aliwahi kuichecheza Coventry City kabla ya kwenda Lisbon mwaka 2023, amefunga mabao 30 katika mechi 28 alizocheza msimu huu, huku Arsenal pia ikiripotiwa kuhitaji huduma ya mshambuliaji huyo. Rekodi za Gykores, 26, kwenye kufunga mabao hilo linampa nafasi kubwa, ambapo amekuwa na wastani wa kufunga bao moja katika kila baada ya dakika 89 kwa rekodi za kuanzia mwanzoni mwa msimu uliopita.
Lakini, kwa Man United kunasa saini yake itahitaji zaidi ya Pauni 70 milioni ili kumng’oa Sporting. Miamba hiyo ya Old Trafford inamtzama pia straika wa Paris Saint-Germain, Randal Kolo Muani kuwa ni jibu sahihi kwenda kumaliza tatizo la mabao katika kikosi hicho.
Kolo Muani, 26, amefunga mabao 11 katika mechi 54 tangu alipojiunga na miamba hiyo ya Ufaransa akitokea Eintracht Frankfurt, Septemba 2023. Dili la uhamisho wa mkopo linafikiriwa kutokana na mchezaji huyo kuwa na mkataba hadi 2028 na anahitaji muda wa kucheza. Msimu huu amefunga mabao mawili tu katika mechi 14 na PSG ilimvuta Parc des Princes kwa ada ya Pauni 77 milioni miezi 16 iliyopita.
Namba za Kolo Muani hazivutii sana kwa kuzilinganisha na za Osimhen na Gyokeres, lakini amekuwa mzuri kwenye eneo la kuasisti. Jina la mwisho kwenye orodha hiyo ya Amorim ni straika wa Juventus, Dusan Vlahovic huku miamba hiyo ya Serie A ikiripotiwa kuhitaji hilo lifanyike kwa kuzingatia dili la kubadilishana wachezaji ili wao wamchukue Joshua Zirkzee arudi kukipiga Italia. Mdachi, Zirkzee amekuwa na wakati mgumu katika miezi yake sita ya kwanza Old Trafford, ambako alijiunga kwa ada ya Pauni 36.5 milioni kutoka Bologna.
Na straika, Vlahovic amebakiza miezi 18 kwenye mkataba wake na Juventus haitaki kumpoteza mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 24 bila ya faida yoyote.
Vlahovic, ambaye alijiunga na Old Lady akitokea Fiorentina kwa ada ya Pauni 67 milioni mwaka 2022, amefunga mabao 12 katika michuano yote msimu huu.
Man United imekuwa na mwanzo mbaya kwenye Ligi Kuu England msimu huu licha ya kutumia Pauni 206 milioni kwenye usajili wa dirisha lililopita la uhamisho wa majira ya kiangazi ilipokuwa chini ya kocha Erik ten Hag. Kutokana na hilo, kocha Amorim anataka kutumia akili nyingi kwenye kufanya usajili kwa maana ya kuhakikisha ananasa wachezaji ambao watakuja kumaliza tatizo la msingi kweye kikosi hicho kwa maana ya kufunga mabao ya kutosha.