Man City, Liverpool vita kali kumuwania Rodrygo
Muktasari:
- Arsenal, Manchester City na Liverpool zote zimeanza kufuatilia kwa karibu hali ya staa huyo huku zikisubiri uamuzi wa mwisho kutoka kwa mabosi wa Real Madrid ikiwa watakuwa tayari kumuuza au la.
WINGA wa Real Madrid na timu ya taifa ya Brazil, Rodrygo Goes, 24, ameonyesha nia ya kuondoka katika dirisha hili kutokana na kutoridhishwa na nafasi yake ndani ya kikosi hicho.
Arsenal, Manchester City na Liverpool zote zimeanza kufuatilia kwa karibu hali ya staa huyo huku zikisubiri uamuzi wa mwisho kutoka kwa mabosi wa Real Madrid ikiwa watakuwa tayari kumuuza au la.
Rodrygo ambaye amekuwa akichezeshwa mara kwa mara nje ya nafasi yake halisi pamoja na kuanzishwa benchi anaamini anaweza kupata nafasi kubwa zaidi na kuwa tegemeo ikiwa atatua kwenye moja kati ya timu za Ligi Kuu England.
Mkataba wake na Real Madrid unatarajiwa kumalizika ifikapo 2028 na msimu huu amecheza mechi 22 za michuano yote, akifunga mabao manne na kutoa asisti mbili.
Joe Willock
CRYSTAL Palace, Leeds United na Nottingham Forest zote zimeonyesha nia ya kutaka kumsajili kiungo wa Newcastle United, Joe Willock, 26.
Willock ambaye amekuwa akipata nafasi finyu ndani ya kikosi cha Newcastle United, anatajwa kutaka kutafuta changamoto mpya ili kurejesha makali aliyoyaonyesha misimu ya nyuma. Newcastle ipo tayari kusikiliza ofa mpya, lakini haina mpango wa kumuuza kwa bei ya hasara.
Ricardo Pepi
FULHAM inakabiliwa na wakati mgumu katika mpango wa kumsajili mshambuliaji wa PSV Eindhoven na timu ya taifa ya Marekani, Ricardo Pepi, 22.
Hata hivyo, PSV inaonekana haina nia ya kumuuza staa huyo kutokana na umuhimu wake ndani ya kikosi na mchango wake wa mabao msimu huu.
Fulham bado inaendelea kufuatilia hali yake lakini italazimika kuweka ofa nono au kusubiri.
Morgan Rogers
CHELSEA inaandaa mipango ya kufanya usajili wa dili kiungo wa Aston Villa na timu ya taifa ya England, Morgan Rogers, 23.
Mbali na Rogers, Chelsea pia imeonyesha nia ya kutaka kumsajili chipukizi wa Arsenal na timu ya taifa ya vijana ya England chini ya umri wa miaka 21, Ethan Nwaneri, 18.
Chelsea inataka kuwapata mastaa hao ikiwa ni mwendelezo wa mkakati wa kuwekeza kwa vijana.
Othmane Maamma
LIVERPOOL, Manchester United na Newcastle United zinaendelea kumfuatilia kwa karibu mshambuliaji wa Watford na timu ya taifa ya Morocco, Othmane Maamma, 20.
Staa huyo amevutia macho ya maskauti wengi wa vigogo hao ambao wamekuwa wakimfuatilia kwa muda mrefu.
Watford inatajwa kuwa tayari kumuuza, lakini kwa klabu ambayo itawasilisha ofa nono katika dirisha hili au lijalo la majira ya kiangazi.
Guido Rodriguez
JUVENTUS imeanza mawasiliano na West Ham United ili kuulizia uwezekano wa kuipata saini ya kiungo wa klabu hiyo na timu ya taifa ya Argentina, Guido Rodriguez, 31, katika dirisha hili la majira ya baridi lililofunguliwa huko Ulaya.
Taarifa zinadai Rodriguez ambaye ana uzoefu anaonekana kuwa chaguo la muda mfupi kwa Juventus wakati ikitathmini mipango ya muda mrefu.
West Ham bado haijaweka wazi msimamo wake lakini inaelezwa kuwa tayari kusikiliza ofa itakayowaridhisha.
Carlos Baleba
MANCHESTER United inaendelea kufuatilia uwezekano wa kumsajili kiungo wa Brighton na timu ya taifa ya Cameroon, Carlos Baleba, 21, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi badala ya hili la Januari.
Hata hivyo, changamoto kubwa inaonekana kuwa kwenye kiasi cha pesa ambacho Brighton inakitaka kuwa kikubwa.
Mabosi wa Man United wanaamini bei ya Baleba anayeuzwa kwa Pauni 90 milioni inaweza kushuka ifikapo mwisho wa msimu huu.
Taty Castellanos
WEST HAM United iko kwenye mazungumzo na Lazio ili kumsajili mshambuliaji wa timu hiyo na timu ya taifa ya Argentina, Taty Castellanos, 27, kwa dau linalokadiriwa kufikia Pauni 25 milioni.
Kocha wa West Ham anataka kuongeza nguvu katika safu ya ushambuliaji baada ya kuona changamoto ya upachikaji mabao msimu huu.
Castellanos ambaye amewahi kucheza pia La Liga akiwa Girona anadaiwa kuuzwa kwa takribani Pauni 30 milioni.