Camavinga akataa ofa ya Liverpool, ataka kubaki
Muktasari:
- Camavinga mwenye umri wa miaka 23, ana uwezo wa kucheza kama kiungo wa kati pamoja na beki wa kushoto jambo ambalo linaitamanisha zaidi Liverpool.
KIUNGO wa kati wa Ufaransa, Eduardo Camavinga, ameonyesha nia ya kubaki katika viunga vya Real Madrid, licha ya timu kibao za Ligi Kuu England ikiwamo Liverpool kuonyesha nia ya kutaka kumsajili.
Liverpool imekuwa ikihitaji kumsajili staa huyu tangu dirisha la majira ya kiangazi mwaka jana na ilipofeli ilikuwa inaangalia uwezekano wa kumpata Januari, lakini sasa inaonekana kuangukia pua baada ya mchezaji mwenyewe kuonyesha nia ya kuendelea kusalia Madrid. Mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2029.
Camavinga mwenye umri wa miaka 23, ana uwezo wa kucheza kama kiungo wa kati pamoja na beki wa kushoto jambo ambalo linaitamanisha zaidi Liverpool.
Vyanzo vya karibu na mchezaji huyo, vinadai kwamba hafikirii kuondoka kwa sasa.
Labda katika dirisa la majira ya kiangazi mwakani.
Tangu kuanza kwa msimu huu, Camavinga amecheza mechi 16 za michuano yote na kati ya hizo ni sita tu ndio alianza katika kikosi cha kwanza na zilizobaki aliingia akitokea benchini.
Hivi karibuni, majeraha ya goti yanatajwa kuwa moja kati ya sababu zinazomfanya asiwe na mwendelezo mzuri.
Manuel Ugarte
MABINGWA wa Uturuki, Galatasaray, wameonyesha nia ya kumchukua kwa mkopo kiungo wa kati wa Manchester United, Manuel Ugarte mwenye umri wa miaka 24.
Staa huyu wa kimataifa wa Uruguay ambaye mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwaka 2029, anahusishwa kuondoka kwa sababu hapati nafasi ya kutosha katika kikosi cha kwanza cha Man United ambapo msimu huu amecheza mechi 14 za michuano yote.
Julian Araujo
CELTIC wako katika mazungumzo na Bournemouth kwa ajili ya kumsajili kwa mkopo beki wao wa kulia, Julian Araujo, mwenye umri miaka 24, kutoka Mexico.
Mabosi wa Celtic walitaka kumsajili staa huyo ili acheze mechi dhidi ya Rangers Januari 3 kabla ya kumruhusu kuondoka katika dirisha hili. Araujo amekuwa hapati nafasi ya kutosha katika kikosi cha kwanza cha Bournemouth.
Adama Traore
WEST Ham ipo tayari kutuma ofa kwa ajili ya kumsajili mshambuliaji wa Fulham, Adama Traore, mwenye umri wa miaka 29, katika dirisha la usajili la Januari.
Mabosi wa West Ham wanataka kuhakikisha wanafanikisha usajili wa nyota huyu kabla ya dirisha kufungwa na inadaiwa inataka kutuma ofa isiyozidi Pauni 10 milioni. Mkataba wake wa sasa na Fulham unamalizika Juni mwaka huu.
Jean-Philippe Mateta
MANCHESTER United inataka kupambana kuhakikisha inamsajili mshambuliaji wa Crystal Palace, Jean-Philippe Mateta, mwenye umri wa miaka 28.
Mchezaji huyu bado hajasaini mkataba mpya na mkataba wake wa sasa utamalizika katika dirisha la majira ya kiangazi mwaka 2027.
Mateta ni miongoni mwa wachezaji tegemeo katika kikosi cha kwanza cha Palace na timu hiyo ipo tayari kumuuza ikiwa mchezaji mwenyewe atahitaji kuondoka.
Msimu huu amefunga mabao tisa katika mechi 29 za michuano yote.
Ethan Nwaneri
BOURNEMOUTH ni miongoni mwa klabu za Ligi Kuu England zinazofikiria kumsajili kiungo wa Arsenal, Ethan Nwaneri mwenye umri wa miaka 18.
Nwaneri amekuwa akionyesha kiwango bora mara zote anazopewa nafasi ya kucheza, lakini muda mwingi amekuwa nje ya Uwanja kutokana na ushindani wa namba.
Benchi la ufundi la Arsenal linaamini staa huyu anahitaji kwenda timu nyingine kwa mkopo ili kukomaa zaidi.
Yan Diomande
MANCHESTER United inakumbana na ushindani mkali kutoka kwa Bayern Munich na Paris St-Germain katika harakati za kutaka kumsajili kiungo wa pembeni wa Ivory Coast, Yan Diomande anayeichezea RB Leipzig.
Diomande, mwenye umri wa miaka 19 ni mmoja kati ya mastaa ambao wapo sokoni katika dirisha hili, lakini timu yake inahitaji takribani Pauni 61 milioni ili kumuuza. Mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2030.
Nathan Ake
MANCHESTER CITY imekubali kumuuza beki wake wa kimataifa wa Uholanzi, Nathan Ake, lakini staa huyo nwenye umri wa miaka 30 amekataa kujiunga na West Ham badala yake anataka kusikiliza ofa kutoka timu nyingine.
Man City bado wako tayari kuzungumza na klabu nyingine zitakazopenda kumnunua mchezaji huyo, na baada ya Ake mwenyewe kukataa ofa ya West Ham inaelezwa Everton na AC Milan zimerudi tena mezani ili kumsajili.