Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Makocha wapya EPL: Nani atatoboa?

MAKOCHA Pict

Muktasari:

  • Miongoni mwa waliokumbana na presha hiyo ni Ange Postecoglou aliyedumu siku 39, pekee Nottingham Forest. Kocha Graham Potter naye alikumbwa na kipindi kigumu West Ham.

LONDON, ENGLAND: Msimu mpya wa Ligi Kuu England umeanza ukiwa na sura mpya kwenye benchi za ufundi, huku klabu tisa zikiwa na makocha wapya na kila mmoja akiwa na malengo yake.

Hata hivyo, Ligi Kuu England si mahali pa watu wa moyo mwepesi. Msimu uliopita ulionyesha jinsi benchi la ufundi linavyoweza kuwa na presha kubwa, huku baadhi ya makocha wakishindwa kumaliza msimu na klabu zao.

Miongoni mwa waliokumbana na presha hiyo ni Ange Postecoglou aliyedumu siku 39, pekee Nottingham Forest. Kocha Graham Potter naye alikumbwa na kipindi kigumu West Ham.

Sasa swali ni moja: makocha hawa wapya wana nafasi gani ya kufanikiwa?

MAKO 07

MARESCA – MAN CITY

Kujiamini: 7/10

Enzo Maresca anakabiliwa na moja ya kazi ngumu zaidi ya kujaribu kuchukua nafasi ya Pep Guardiola, kocha aliyeacha alama kubwa Manchester City.

Guardiola aliiongoza City kutwaa mataji sita ya Ligi Kuu England, Ligi ya Mabingwa Ulaya pamoja na FA Cup na Kombe la Ligi.

Maresca anafahamu mazingira ya klabu hiyo baada ya kufanya kazi chini ya Guardiola, jambo linaloweza kumsaidia kuingia vizuri kwenye majukumu yake.

Pia, anaweza kunufaika na ukweli kwamba City haikutwaa ubingwa wa England msimu uliopita, huku yeye akiwa amepata muda wa kujiandaa baada ya kuanza kuhusishwa na nafasi hiyo katikati ya msimu uliopita.

Changamoto kubwa kwake itakuwa kujenga utambulisho wake bila kuishi kwenye kivuli cha Guardiola.

MAKO 01

IRAOLA – LIVERPOOL

Kujiamini: 6/10

Andoni Iraola amepewa jukumu la kuiongoza Liverpool baada ya kuondoka kwa Arne Slot, huku akitarajiwa kuleta soka lake la kushambuliaji na mbinu zisizotabirika Anfield.

Iraola aliacha alama Bournemouth kwa kuifikisha kwenye nafasi yao bora zaidi ya ligi, kuvunja rekodi ya pointi na kuiwezesha kushiriki michuano ya Ulaya katika msimu wake wa mwisho.

Mashabiki wa Liverpool wana matumaini na soka la kushambulia analoahidi, lakini uvumilivu wao unaweza kuwa mdogo baada ya Slot kuondoka.

Iraola anatakiwa kuanza kwa kasi, hasa kutokana na wasiwasi uliopo kwenye safu ya ulinzi ambao ulionekana pia katika maandalizi ya msimu.

MAKO 02

ROSE – BOURNEMOUTH

Kujiamini: 4/10

Marco Rose amepewa jukumu la kuchukua nafasi ya Iraola, lakini historia yake ya ukocha imekuwa na mafanikio na misukosuko kwa wakati mmoja.

Alipata umaarufu zaidi Borussia Dortmund, ambako alidumu msimu mmoja pekee baada ya timu kushindwa kufika hatua ya mtoano ya Ligi ya Mabingwa.

RB Leipzig alishinda German Cup, lakini baadaye alifutwa kazi kutokana na matokeo yasiyoridhisha Bundesliga na Ligi ya Mabingwa.

Hata hivyo, uwezo wake wa kukuza vipaji vya vijana unaweza kuendana vizuri na mfumo wa usajili wa Bournemouth.

MAKO 03

ALONSO – CHELSEA

Kujiamini: 6/10

Xabi Alonso anarejea England akiwa na kumbukumbu nzuri za Bayer Leverkusen, ambako aliandika historia mwaka 2024 kwa kuiongoza klabu hiyo kutwaa Bundesliga kwa mara ya kwanza na kukamilisha msimu bila kupoteza.

Leverkusen pia iliweka rekodi ya Ulaya ya kucheza mechi 51 bila kufungwa, jambo lililomfanya Alonso kuwa mmoja wa makocha vijana waliotafutwa zaidi barani Ulaya.

Hata hivyo, changamoto yake kubwa ni kipindi kifupi alichokuwa Real Madrid msimu uliopita, ambako aliondoka baada ya mwanzo mbaya wa msimu na kutokuelewana na baadhi ya mastaa.

Chelsea naye ana kikosi kikubwa na mazingira yenye presha, hivyo Alonso atalazimika kuweka mpangilio Stamford Bridge.

Kwa kiasi cha vipaji vilivyopo, Chelsea inaweza kuwaduwaza katika mbio za mataji ya ndani.

MAKO 04

ARBELOA – FULHAM

Kujiamini: 3/10

Alvaro Arbeloa amepewa nafasi ya kuchukua mikoba ya Marco Silva baada ya kocha huyo kumaliza kipindi chake cha miaka mitano Fulham.

Changamoto kubwa kwa Arbeloa ni uzoefu mdogo wa kuiongoza timu ya wakubwa. Uzoefu wake mkubwa ulikuwa kipindi cha miezi sita Real Madrid, ambako alishindwa kupata matokeo yaliyotarajiwa.

Hata hivyo, uhusiano wake na Madrid umemsaidia kuwapeleka Fulham wachezaji Gonzalo Garcia na Cesar Palacios.Presha itakuwa kubwa kutokana na viwango vilivyowekwa na Silva. Arbeloa anatakiwa kuanza vizuri la sivyo anaweza kujikuta akihusishwa mapema na orodha ya makocha wanaoweza kufukuzwa.

MAKO 05

JAISSLE – NEWCASTLE

Kujiamini: 5/10

Matthias Jaissle alifanya vizuri Red Bull Salzburg, ambako alishinda mataji mawili ya ndani na kuipeleka timu hiyo hatua ya mtoano ya Ligi ya Mabingwa.

Baadaye alijiunga na Al-Ahli ya Saudi Arabia na kushinda mataji mawili mfululizo ya Ligi ya Mabingwa Asia.

Lakini Newcastle aliyokutana nayo si ile iliyokuwepo mwishoni mwa msimu uliopita, baada ya kuondoka kwa Sandro Tonali, Bruno Guimaraes na Anthony Gordon.

Jaissle (38), hajawahi kuthibitisha uwezo wake katika moja ya ligi kubwa za Ulaya. Bila usajili mkubwa wa wachezaji, kazi yake inaweza kuwa ngumu.

MAKO 06

SAGE – CRYSTAL PALACE

Kujiamini: 6/10

Pierre Sage amepewa kazi Palace baada ya kufanya vizuri Lens, ambako aliiongoza kutwaa French Cup na kumaliza nafasi ya pili Ligue 1, matokeo yaliyoipeleka timu hiyo Ligi ya Mabingwa.

Rekodi hiyo imewapa mashabiki wa Palace matumaini, ingawa bado hana uzoefu wa muda mrefu katika kiwango hicho.

Sage anategemewa kuleta utulivu, ujasiri na mbinu zisizo na hofu kwenye Uwanja wa Selhurst Park.

MAKO 08

GLASNER – NOTTINGHAM FOREST

Kujiamini: 8/10

Oliver Glasner amekubali kuhamia Nottingham Forest baada ya kumaliza kipindi chake kizuri Crystal Palace, akivutiwa na mipango na matarajio ya mmiliki Evangelos Marinakis.

Kocha huyo wa Austria anajulikana kwa mbinu zake bora na soka la mashambulizi ya kushtukiza.

Kazi ya Forest inaweza kuwa na presha, lakini Glasner alikuwa na nafasi ya kuchagua klabu nyingine kubwa Ulaya na uamuzi wake wa kwenda City Ground unaonyesha ukubwa wa mradi huo.

Swali ni kama ataweza kuifanya Forest ipige hatua nyingine zaidi ya alichokifanya Nuno Espirito Santo, au uhusiano wake na Marinakis utaanza kuyumba kama ilivyowahi kutokea kwa makocha wengine.

MAKO 09
MAKO 09

O’NEIL – IPSWICH

Kujiamini: 3/10

Gary O’Neil amechukua nafasi ya Kieran McKenna, ambaye aliondoka Ipswich baada ya kuiongoza timu hiyo kurejea Ligi Kuu England.

O’Neil mara ya mwisho alifundisha EPL akiwa Wolves, ambako alifutwa kazi Desemba 2024 wakati timu ikiwa pointi nne tu juu ya mstari wa kushuka daraja.

Hata hivyo, haipaswi kusahaulika kazi nzuri aliyofanya Bournemouth msimu wa 2022/23, alipoiweka timu hiyo salama baada ya kutengeneza mfululizo wa mechi sita bila kupoteza.

Iwapo ataweza kuiweka Ipswich salama EPL, O’Neil anaweza kujikuta akitajwa miongoni mwa makocha bora wa msimu.


HITIMISHO

Msimu huu unaonekana kuwa mtihani mkubwa kwa makocha wote tisa. Wengine wanaingia wakiwa na uzoefu na mataji, huku wengine wakipewa nafasi ya kwanza kuthibitisha uwezo wao katika mazingira yenye presha kubwa.

Lakini EPL ina sheria moja isiyoandikwa: matokeo ndiyo yanayomlinda kocha kubaki katika kibarua chake.

Kwa baadhi yao, presha ya kufukuzwa inaweza kuanza hata kabla ya nusu ya msimu.