Machimbo sita ya straika Alexander Isak
Muktasari:
- Isak, 25, anataka kuachana na Newcastle kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi baada ya kugomea dili la mkataba mpya lenye thamani ya kulipwa mshahara wa Pauni 300,000 kwa wiki.
NEWCASTLE, ENGLAND: ALEXANDER Isak huenda akaanzisha vita kali baada ya kuiambia Newcastle United anataka kuhama.
Isak, 25, anataka kuachana na Newcastle kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi baada ya kugomea dili la mkataba mpya lenye thamani ya kulipwa mshahara wa Pauni 300,000 kwa wiki.
Staa huyo wa kimataifa wa Sweden ametoweka kwenye mechi za pre-season za Newcastle, huku klabu hiyo ya St James’ Park ikidai mchezaji ni majeruhi.
Newcastle imesema mara kadhaa mchezaji wao huyo hauzwi, lakini hilo halijazizuia klabu nyingi kumfukuzia straika huyo, ambaye sasa anataka kuondoka. Liverpool imeonyesha dhamira ya kumsajili, licha ya kwamba imeshamnasa straika mwingine, Hugo Ekitike.
Lakini, Arsenal pia ni kati ya klabu zinazohitaji huduma ya Isak. Na sasa kuna klabu sita ambazo zinaweza kuwa machimbo yajayo ya Isak, atakapoachana na Newcastle ambayo inamthaminisha kuwa na thamani ya Pauni 150 milioni.
LIVERPOOL
Anfield panaonekana panaweza kuwa maskani mpya ya Isak endapo kama atauzwa na Newcastle. Liverpool licha ya kutumia karibu Pauni 300 milioni kwenye usajili wa nyota wapya katika dirisha hili la majira ya kiangazi, akiwamo straika wa Pauni 79 milioni, Ekitike, bado inamtaka Isak. Miamba hiyo inaripotiwa kuweka mezani ofa ya Pauni 120 milioni kwa ajili ya Isak.
ARSENAL
Kocha Mikel Arteta anafahamika wazi ni shabiki wa Isak na straika huyo wa Sweden alikuwa kwenye rada za Arsenal kwenye usajili wa dirisha hili. Lakini, lakini baada ya kuona ugumu, Arsenal ilihamia kwa straika wa Sporting CP, Viktor Gyokeres, ambaye sasa inakaribua kumnasa baada ya kuafikiana ada ya Pauni 54.8 milioni na bonasi ya Pauni 8.6 milioni.
CHELSEA
Kama kuna timu ambayo inaonekana haijali kuhusu matumizi basi ni Chelsea. Kinachoripotiwa ni kwamba Chelsea kwa sasa kikosi chao kina ruhusa ya kusajili mchezaji wa Pauni 100 milioni. Inahusishwa na Xavi Simon na Jorrel Hato, lakini kocha Enzo Maresca anaweza kushawishika kuvamia kwenye dili la kumnasa Isak licha ya kuwa na washambuliaji Liam Delap na Joao Pedro aliowanasa kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi.
MAN UNITED
Ruben Amorim ana matumaini ya kuongeza straika kwenye kikosi chake kabla ya msimu mpya kuanza. Isak anaweza kuwa usajili wa ndoto kwenye kikosi cha Manchester United ili kwenda kuongeza makali kwenye safu ya ushambuliaji baada ya kuwakosa Gyokeres na Ekitike. Lakini, kuna vitu viwili vinavyoweza kuzuia dili la Isak huko Old Trafford, kwanza ufinyu wa bajeti na pili ni kukosekana kwa soka la Ulaya msimu ujao.
REAL MADRID
Kama ni ishu ya kwenda kutamba kwenye soka la Ulaya inayomsumbua Isak, basi klabu ambayo atapenda kuungana nayo ni Real Madrid. Isak anaweza kujiunga na timu ya mastaa watupu Galacticos, ambayo ni ndoto ya wachezaji wengi. Miamba hiyo ya La Liga bado haina straika wa asili kwenye safu yake ya wakali watatu mbele na imekuwa ikiwatumia Kylian Mbappe na Vinicius Junior. Hivyo, Isak anaweza kuwa chaguo bora kwa kocha Xabi Alonso akitua hapo.
AL HILAL
Ripoti zinafichua kwamba klabu za Saudi Arabia zinafuatilia ishu ya Isak na Al-Hilal ni kati ya timu hizo. Na ada ya Pauni 150 milioni inaweza isiwe tatizo kabisa kwa timu hiyo, kwa sababu yenyewe imeshaweka mezani ofa inayozidi Pauni 250 milioni. Kuhamia Mashariki ya Kati hasa Al-Hilal kunaweza kuibua gumzo kubwa kutokana na wamiliki wa klabu hiyo Saudi Arabian Public Investment Fund (PIF) - kuwa ndiyo wanaoimiliki Newcastle pia.