Luis Diaz, Bayern Munich haijaisha hadi iishe
Muktasari:
- Bayern imeingia katika vita ya kuiwania saini ya staa huyu baada ya kuona kuba ugumu wa kumpata Rodrygo ambaye ilihamia kwake baada ya kumkosa Nico Williams.
WINGA wa kimataifa wa Colombia Luis Diaz, 28, bado ana dhamira ya kuondoka Liverpool dirisha hili la usajili la majira ya kiangazi na Bayern Munich ni miongoni mwa timu anazoweza kutua.
Bayern imeingia katika vita ya kuiwania saini ya staa huyu baada ya kuona kuba ugumu wa kumpata Rodrygo ambaye ilihamia kwake baada ya kumkosa Nico Williams.
Liverpool inaripotiwa kuhitaji zaidi ya Pauni 60 milioni kama ada ya uhamisho ya staa huyu.
Awali Diaz alikuwa akitajwa Barcelona lakini timu hiyo ilikuwa ikipata changamoto kubwa kwenye ada yake ya uhamisho ambayo kwao ilikuwa kubwa hususani katika kipindi hiki ambacho vitabu vyao vya mahesabu havipo sawa.
Diaz anataka kupata changamoto mpya sehemu nyingine na anaamini timu nyingine atakayojiunga nayo itampa ofa kubwa zaidi ya ile ambayo anaipata kwa sasa.
Bayern inahitaji sana huduma yake lakini pia inafanya mazungunzo na wawakilishi wa Liverpool kuona kama wanaweza kukubali kupunguza bei.
Mkataba wa sasa wa Diaz unamalizika mwaka 2027 na msimu uliopita alicheza mechi 50 za michuano yote, amefunga mabao 17 na kutoa asisti nane.
Ikiwa Bayern itashindwa kufikia mwafaka na Liverpool juu ya ada yake ya uhamisho, Diaz huenda akatimkia Saudi Arabia ambako baadhi ya timu zipo tayari kulipa kiasi hicho cha pesa ili kuipata saini yake.
James McConnell
KIUNGO wa kati wa Liverpool na timu ya taifa ya England ya vijana chini ya miaka 20, James McConnell, mwenye umri wa miaka 20, yuko karibu kusaini mkataba mpya wa muda mrefu na klabu hiyo katika dirisha hili. Kwa mujibu wa tovuti ya Daily Mail, Liverpool imepanga kumsainisha mkataba mpya fundi huyu kisha kumtoa kwa mkopo kwenda timu moja wapo ya Ligi Daraja la Kwanza England ili aendelee kuimarika zaidi wakiamini atakuja kuwa tegemeo kwenye timu kwa siku za usoni.
Granit Xhaka
SUNDERLAND na Fenerbahce bado zina nia ya kumsajili kiungo wa Bayer Leverkusen na timu ya taifa ya Switzerland, Granit Xhaka, licha ya ofs zao za hivi karibuni kukataliwa. Licha ya ofa nono ambazo zimewasilishwa na timu mbalimbali mabosi wa Leverkusen wanaonekana kuwa wagumu kumruhusu staa huyu kuondoka katika dirisha hili. Mbali ya timu za Ulaya huduma yake pia inahitajika na timu za Saudi Arabia lakini mwenyewe bado anahitaji kuendelea kucheza soka la kiushindani.
Federico Chiesa
Napoli, AC Milan, Roma, Juventus na Inter Milan zote zipo katika vita kali ya kuiwania saini ya winga wa Liverpool, Federico Chies, 27 hili. Chiesa msimu uliopita hakupata nafasi kubwa ya kucheza Liverpool baada ya kujiunga nao akitokea Juventus. Hata yeye mwenyewe pia ameonyesha nia ya kuondoka na Liverpool inadaiwa kutaka chini ya Pauni 30 milioni kam ada yake ya uhamisho, pia ipo tayari kumwachia kwa mkopo.
Takefusa Kubo
EVERTON imezungumza na Real Sociedad kuhusu uwezekano wa kuipata saini ya winga wa timu hiyo na Japan, Takefusa Kubo, mwenye miaka 24, katika dirisha hili. Kubo ambaye alionyesha kiwango bora katika msimu uliopita amekuwa akihitajika na timu nyingi barani Ulaya ambazo zimevutiwa sana na kiwango chake. Inaelezwa Everton inataka kutoa zaidi ya Pauni 30 milioni kwa ajili ya kukamilisha dili la fundi huyu.
Benjamin Lecomte
FULHAM inatarajiwa kukamilisha usajili wa kipa wa kimataifa wa Ufaransa mwenye umri wa miaka 34 kutoka Montpellier, Benjamin Lecomte, katika siku chache zijazo. Fulham imekuwa katika mazungumzo ya kumsajili kipa huyu tangu Januari mwaka huu lakini ilishindikana kumpata kwa wakati huo. Lacomte mwenyewe alionyesha nia ya kutaka kuondoka kwa sababu ni ndoto yake kucheza Ligi Kuu England.
Gianluigi Donnarumma
GALATASARAY inataka kumsajili kipa wa Paris Saint-Germain, Gianluigi Donnarumma, 26, ambaye amebakiza mwaka mmoja kwenye mkataba wake wa sasa. Licha ya mazungumzo yaliyofanywa hadi sasa kipa huyu bado hajakubali kusaini mkataba mpya haliinayoiaminisha Galatasaray kwamba inaweza kumpata.
Morgan Gibbs-White
NOTTINGHAM Forest imefikia hatua nzuri katika jitihada zao za kumshawishi kiungo wao raia wa England, Morgan Gibbs-White, 25, asaini mkataba wa muda mrefu wa kuendelea kusalia kwenye kikosi chao. Mabosi wa Forest wameanza harakati hizo baada ya kuona timu nyingi ikiwemo Tottenham zinainyemelea saini yake, hivyo inataka kumpa mkataba mpya ili hata ikumuuza imuuze kwa pesa nyingi zaidi.