Liverpool yapanga kumsajili Greenwood dirisha hili dogo
Muktasari:
- Greenwood amekuwa katika kiwango bora akiwa na Marseille msimu huu, hali iliyowavutia vigogo hao wa Anfield na kuanza kumfuatilia kwa karibu ikiamini anaweza kuwa mbadala wa Mohamed Salah.
LIVERPOOL inafikiria kuwasilisha ofa kwa ajili ya kumsajili aliyekuwa mshambuliaji wa Manchester United, Mason Greenwood, mwenye umri wa miaka 24.
Greenwood amekuwa katika kiwango bora akiwa na Marseille msimu huu, hali iliyowavutia vigogo hao wa Anfield na kuanza kumfuatilia kwa karibu ikiamini anaweza kuwa mbadala wa Mohamed Salah.
Mshambuliaji huyo wa kimataifa wa England ameongeka thamani yake sokoni kutokana na kiwango chake akifunga mabao 15 katika mechi 23 za michuano yote tangu kuanza kwa msimu huu.
Hata hivyo, bado haijulikani kama Marseille itakuwa tayari kumuuza kirahisi nyota huyo ambaye ameonekana kuwa mhimili muhimu katika kikosi chao.
Mkataba wa sasa wa staa huyu unatarajiwa kumalizika mwaka 2029 na ili kumuuza huenda Marseille ikahitaji kiasi kikubwa cha pesa kinachoweza kufikia Pauni 90 milioni.
Awali, Greenwood pia alihusishwa na baadhi ya klabu za Italia lakini Marseille ilishikilia msimamo wa kutohitaji kumuuza.
Mario Balotelli
ALIYEKUWA mshambuliaji wa Manchester City na Liverpool, Mario Balotelli, yuko mbioni kujiunga na klabu ya 14 katika maisha yake ya soka baada ya kufikia makubaliano na Al Ittifaq ya Falme za Kiarabu.
Balotelli, mwenye umri wa miaka 35, anatarajiwa kujiunga na klabu hiyo ya daraja la pili ndani ya siku chache zijazo. Nyota huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Italia amecheza katika klabu nyingi barani Ulaya.
Mike Maignan
KIPA wa AC Milan na timu ya taifa ya Ufaransa, Mike Maignan, mwenye umri wa miaka 30, ambaye amekuwa akihusishwa na uhamisho wa kwenda Chelsea, yuko karibu kusaini mkataba mpya wa kuendelea kuitumikia Milan.
Milan inamchukulia kipa huyo kama nguzo muhimu ya kikosi chao na inataka kumpa mkataba wa muda mrefu ili kuondoa kabisa tetesi za kuondoka kwake.
Chelsea inatajwa kumfuatilia kwa karibu lakini nafasi ya kumsajili inaonekana kuwa ndogo kwa sasa.
Dayot Upamecano
BEKI wa Bayern Munich na timu ya taifa ya Ufaransa, Dayot Upamecano, 27, amefikia makubaliano ya awali ya kusaini mkataba mpya wa kuendelea kusalia katika kikosi hicho.
Mshahara, muundo na urefu wa mkataba mpya vimekubaliwa baada ya Bayern kutoa ofa yao bora kabisa ili kumbakiza beki huyo.
Kipengele pekee kilichobaki kukamilishwa ni kifungu cha kuachiliwa (release clause).
John Stones
BEKI wa Manchester City na timu ya taifa ya England, John Stones, mwenye umri wa miaka 31, yuko katika mwaka wa mwisho wa mkataba wake na klabu hiyo na hadi sasa hakuna mazungumzo yoyote ya mkataba mpya.
Stones amekuwa akisumbuliwa na majeraha ya mara kwa mara hali iliyopunguza muda wake wa kucheza katika kikosi cha kwanza cha msimu huu.
Mabosi wa Man City wanataka kujadili hatma ya beki huyu baada ya msimu kumalizika.
Murillo
AC MILAN inaendelea kufanya maboresho katika safu yake ya ulinzi na imeweka macho kwa mabeki wawili, Joe Gomez wa Liverpool na Murillo wa Nottingham Forest.
Gomez, 28, ana uzoefu mkubwa wa Ligi Kuu ya England pamoja na michuano ya Ulaya, jambo linalomfanya kuwa chaguo linalovutia zaidi kwa vigogo hao wa Italia.
Kwa upande mwingine, Murillo mwenye umri wa miaka 23, naye anahitajika sana, lakini changamoto ni ada yake ya uhamisho.
Marc Guehi
LIVERPOOL inatajwa kuandaa ofa ya Pauni 20 milioni kwa ajili ya kumsajili beki wa Crystal Palace na timu ya taifa ya England, Marc Guehi, mwenye umri wa miaka 25.
Guehi amekuwa mmoja wa mabeki wanaohitajika zaidi katika Ligi Kuu ya England kutokana na kiwango chake bora alichoonyesha tangu msimu uliopita.
Palace inahitaji zaidi ya Pauni 40 milioni kumuuza beki huyo ambaye mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwisho wa msimu.
Ethan Nwaneri
BOURNEMOUTH imeonyesha nia ya kumsajili kwa mkopo kinda wa Arsenal na timu ya taifa ya England kwa vijana wenye umri chini ya miaka 21, Ethan Nwaneri, mwenye umri wa miaka 18.
Nwaneri amekuwa hapati nafasi ya kutosha katika kikosi cha kwanza cha The Gunners hali iliyofanya Bournemouth kuona fursa ya kumsajili kwa mkopo wa nusu msimu.
Hata hivyo, taarifa zinaeleza kuwa Nwaneri mwenyewe anataka kubaki katika viunga vya Emirates na kupigania nafasi yake chini ya kocha Mikel Arteta.