Liverpool yamwomba Mo Salah Misri
Muktasari:
- Mafarao walitolewa na Senegal kwa kichapo cha bao 1-0 katika nusu fainali, huku bao la Senegal likifungwa na Sadio Mane dakika ya 76, aliyepiga shuti kali akiwa nje ya boksi.
LIVERPOOL, ENGLAND: LIVERPOOL italazimika imetuma maombi kwenda Misri kwa ajili ya kuipata haraka huduma ya mshambuliaji wao wa kimataifa wa Misri, Mohamed Salah, baada ya taifa lake kuwa tayari imetolewa kwenye Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) na Senegal.
Mafarao walitolewa na Senegal kwa kichapo cha bao 1-0 katika nusu fainali, huku bao la Senegal likifungwa na Sadio Mane dakika ya 76, aliyepiga shuti kali akiwa nje ya boksi.
Salah alikuwa amefunga mabao manne kabla ya mechi hiyo lakini kutolewa kwake kunazima ndoto zake za kuwa mfungaji bora wa mashindano hayo kwa msimu huu pia ndoto ya kushinda taji lake la kwanza la AFCON akiwa na Misri.
Baada ya kutolewa, ripoti zinadai kuna uwezekano Salah akaruhusiwa kuondoka mapema na asisubirie mechi ya mshindi wa tatu dhidi ya Nigeria itakayopigwa wikiendi ijayo.
Taarifa za ndani zinadai Liverpool imewasilisha maombi ya kutaka staa huyo arudi na kuwahi mechi dhidi ya Burnley Jumamosi au ikishindikana aiwahi mechi ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Marseille Jumatano Januari 21.
Hata hivyo, ikiwa Misri itagoma kumwachia staa huyu kuna uwezekano Salah akarejea uwanjani katika mechi ya Jumamosi, Januari 24, ugenini dhidi ya Bournemouth.
Kurejea kwa Salah England kunaweza kufungua upya mjadala kuhusu mustakabali wake katika viunga vya Liverpool.
Kwa sasa mambo yanaonekana kutulia, lakini kabla ya kwenda AFCON Desemba, nyota huyo mwenye umri wa miaka 33 alimshambulia hadharani kocha wa Liverpool, Arne Slot, akidai anajaribu kumtumia yeye kama mbuzi wa kafara kutokana na matokeo mabovu ya timu kwa wakati huo.
Hiyo ilisababisha asisafiri kwenda katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa dhidi ya Inter nchini Italia, kabla ya kurejea uwanjani katika mechi yake ya mwisho dhidi ya Brighton, kisha kusafiri kwenda Morocco kwa ajili ya mashindano ya AFCON.
Kwa kuwa dirisha la usajili la Januari sasa liko wazi, ripoti zinadai Liverpool inaweza kusikiliza ofa nono kwa timu zinazohitaji huduma yake hususani Saudi Arabia.