Liverpool vs Man United kuna mtu atapigwa nyingiii!

Muktasari:
- Hicho kinahusu kipute cha kesho Jumapili, huko Anfield wakati Liverpool itakuwa mwenyeji kukipiga na Manchester United. Patachimbika.
LONDON, ENGLAND: KWENYE karatasi zinaonekana ni pointi tatu nyepesi kabisa kwa Liverpool. Shida ipo uwanjani, litathibitika hilo?
Hicho kinahusu kipute cha kesho Jumapili, huko Anfield wakati Liverpool itakuwa mwenyeji kukipiga na Manchester United. Patachimbika.
Man United imepoteza mechi tano kati ya saba za Ligi Kuu England walizocheza mwezi uliopita. Wanakwenda Anfield wakitokea kuchapwa kwenye mechi tatu mfululizo kwenye ligi hiyo mbele ya Bournemouth, Wolves na Newcastle United. Je, watapigwa tena?
Presha ni kubwa kwenye kikosi hicho cha kocha Ruben Amorim, ambacho kimeruhusu mabao saba bila ya majibu katika mechi tatu zilizopita, huku wanatambua wanakwenda kukutana na Liverpool yenye safu hatari ya ushambuliaji. Liverpool imefunga mabao 14 katika mechi tatu zilizopita, huku winga wao Mohamed Salah akiwa kwenye kiwango bora kabisa cha maisha yake ya soka. Je, kuna mtu anapigwa nyingi? Tusubiri hapo kesho.
Kipute cha Liverpool na Man United ni cha kibabe zaidi kwa wikiendi hii. Takwimu zinaonyesha kwamba, timu hizo zimekutana mara 65 kwenye Ligi Kuu England, ambapo mechi 16 zilimalizika kwa sare, huku Liverpool ikishinda 20, mara 12 ilipocheza nyumbani Anfield na nane ugenini, wakati Man United imeshinda 29, mara 17 ilipocheza nyumbani Old Trafford na 12 ugenini, kwa maana kwenye uwanja wa nyumbani wa Liverpool. Hiyo ina maana, Man United imeshinda idadi sawa ya mechi ilizoshinda Liverpool uwanjani Anfield ilipokwenda kucheza mechi za ligi.
Kipute kingine cha Ligi Kuu England kwa kesho kitazikutanisha Fulham itakayokuwa kwao Craven Cottage kukipiga na Ipswich Town inayopambana kujiondoka kutoka kwenye timu zinazopambana kukwepa kushuka daraja.
Keshokutwa Jumatatu, kutakuwa na mchezo mmoja tu, ambapo Wolves iliyo kwenye kiwango bora kabisa kwa sasa, itakapokuwa nyumbani Molineux Stadium kucheza na Nottingham Forest, ambao wapo kwenye kiwango bora msimu huu na kushangaza wengi kwenye Ligi Kuu England. Kinachofurahisha kuhusu mechi hiyo ni kwamba Wolves na Forest zimekutana mara tano kwenye Ligi Kuu England, ambapo katika mechi hizo sare ni nne na Wolves imeshinda moja, ilipocheza nyumbani. Je, itapata ushindi wa pili au itakuwa sare nyingine kama Forest hawajapa ushindi wao wa kwanza? Ni mechi ya kibabe kabisa inayokutanisha timu mbili ambazo zipo kwenye viwango bora kwa sasa.
Kivumbi na jasho kitaanzia leo Jumamosi kwa mechi kibao, huku wengi wakisubiri kuona kitakachotokea huko Tottenham Hotspur, ambao watakuwa nyumbani kucheza na Newcastle United. Mechi hiyo ni ngumu na ina mvuto mkubwa, ambapo Newcastle imeonekana kujipata huku Spurs ikiwa kwenye mwendo wa kusuasua na kumpa presha kocha wao, Ange Postecoglou juu ya usalama wa kibarua chake huko London.
Mara 59 ambazo timu hizo zimekutana kwenye Ligi Kuu England, Spurs imeshinda 25 na Newcastle 26. Katika mechi hizo, Spurs imeshinda nyumbani mara 16 na ugenini tisa, wakati Newcastle imeshinda ugenini 11 na nyumbani 15, huku mechi nane baina yao zilimalizika kwa sare. Mchezo wa mwisho, Newcastle iliichapa Spurs 2-1.
Kasheshe jingine litakuwa huko Villa Park, ambapo Aston Villa ya Unai Emery itakuwa na kibarua mbele ya Leicester City, ambayo imekuwa kwenye mwendo wa hovyo kwa siku za karibuni, huku Bournemouth ikiwa na kazi nzito mbele ya Everton inayopambana kuhakikisha mambo yanakuwa sawa na kurudi kwenye mstari.
Huko Selhurst Park kutakuwa na kipute cha London derby, wakati Crystal Palace itakapoikaribisha Chelsea, ambayo itakwenda kwenye mechi hiyo ya ugenini ikiwa na kumbukumbu ya kuchapwa mechi mbili zilizopita. Kwenye takwimu, Chelsea imeonekana kuwa mbaya wa mechi zao dhidi ya Palace, ambapo mara 31 ilizokutana kwenye ligi, imeshinda 24, mara 12 nyumbani na 12 nyingine ugenini, huku Palace yenyewe imeshinda nne tu, mbili nyumbani na mbili nyingine ugenini, wakati mara tatu timu hizo zilitoka sare. Je, Chelsea itaendeleza ubabe wake mbele ya Palace au itapoteza kwenye mchezo wa tatu mfululizo na kumweka pagumu kocha Enzo Maresca? Ngoja tuone.
Southampton itaulizana maswali na Brentford, lakini wengi watasubiri kuona kama Arsenal itatumia vyema fursa na faida ya kutangulia kucheza kabla ya Liverpool ili kupunguza pengo la pointi itakapokwenda ugenini kukipiga na Brighton. Miamba hiyo miwili ni kama inaviana kwenye namba zao za mechi walizokutana kwenye Ligi Kuu England, ambapo mara 15 walizokutana, Arsenal imeshinda sita, tatu nyumbani na tatu ugenini, huku Brighton imeshinda tano, mbili nyumbani na tatu ugenini. Mechi nne zilimalizika kwa sare, huku mara ya mwisho zilifungana bao 1-1. Ushindi wa Arsenal utawafanya kupunguza pengo la pointi na kubaki tatu baina yao na vinara Liverpool, ambao wao watasubiri kesho kukwaana na mahasimu wao, Man United.
Manchester City baada ya kupata ushindi kwenye mechi iliyopita itashuka uwanjani Etihad kuwakaribisha West Ham United. Kocha Pep Guardiola na kikosi chake cha Man City atahitaji ushindi katika mchezo huo wa nyumbani ili kuifanya timu yake kurudisha hali ya kujiamini. Takwimu zinawabeba, ambapo kwenye mechi 47 za ligi, Man City imeshinda 30, mara 19 nyumbani na 11 ugenini, huku West Ham imeshinda tisa tu, saba nyumbani na mbili ugenini, wakati kuna mechi nane zilimalizika kwa sare. Mechi ya mwisho zilipokutana, Man City ilishinda 3-1. Je, safari hii itakuwaje? Man City itashinda tena au itarudishwa kulekule kwenye majanga ya vichapo na sare? Patamu hapo.