Kwa Arsenal hii mtateswa juu, mtateswa chini
Muktasari:
- Wiki hii, Arsenal imekamilisha usajili wa kiungo Christian Norgaard, balaa jingine hilo kwenye vita ya ana kwa ana. Norgaard wanamwita 'Duel Monster', sasa amejiunga kwenye kikosi hicho cha Mikel Arteta.
LONDON, ENGLAND: ARSENAL inafanya usajili, ambao utawapasua vichwa wapinzani wao, kwenye ishu ya kupitisha mipira, wapite wapi - chini tatizo na juu ndiyo usiseme.
Wiki hii, Arsenal imekamilisha usajili wa kiungo Christian Norgaard, balaa jingine hilo kwenye vita ya ana kwa ana. Norgaard wanamwita 'Duel Monster', sasa amejiunga kwenye kikosi hicho cha Mikel Arteta.
Kinachovutia kuhusu Arteta ni anahitaji wachezaji wenye vimo virefu na wenye uzuri pia wa kuuchezea mpira, ili timu yake iwe na udhibiti kwenye mipira ya chini na ile ya juu.
Kwenye usajili huo wa Norgaard, Arsenal imeleta mchezaji mwingine asiyeshindika kirahisi kwenye suala la kugombania mpira na mchezaji wa upinzani.
Umri wa kiungo huyo ni miaka 31, hivyo ana uzoefu wa kutosha, huku akisaini miaka miwili yenye kipengele cha kuongeza mwaka wa tatu, endapo kama huduma yake itakuwa bora Emirates. Kocha Arteta alihitaji kuboresha safu yake ya kiungo baada ya kuondoka Thomas Partey na Jorginho.
Ukimweka kando Norgaard, kiungo mwingine aliyenaswa na Arsenal ni Mhispaniola, Martin Zubimendi, aliyetua Emirates akitokea Real Sociedad kwa ada ya Pauni 51 milioni.
Kiungo Norgaard si kwamba ataleta ubora wake kwenye kikosi cha Arsenal, bali pia staa huyo wa Denmark mwenye kimo cha futi 6 na inchi 1, ataongeza idadi ya wachezaji warefu kwenye timu hiyo, akiwa na nguvu na uwezo wa kucheza mipira ya juu, hivyo The Gunners itaendelea kuwa tishio kwenye ile mipira yao ya kutenga, ambayo wamekuwa wakiitumia kuwatesa wapinzani.
Wakati Arteta alipomsajili kiungo wa futi 6 na inchi 2, Mikel Merino kutoka Sociedad dirisha la majira ya kiangazi la mwaka jana kwa ada ya Pauni 31.6 milioni, Mhispaniola huyo aliitwa “Duel Monster” – akishinda vita zote za ana kwa ana na wachezaji wengine, akifanya hivyo mara nyingi kuliko mchezaji yeyote kwenye ligi tano kubwa za Ulaya. Na sasa kwenye kikosi hicho cha Arsenal, ameongezeka mwingine, Norgaard. Mtapita wapi?
Katika mechi yake ya kwanza akiwa benchi, Desemba 2019, zaidi ya nusu ya kikosi kilichoanza katika Arsenal ya Arteta ilikuwa na wachezaji waliokuwa na vimo chini ya futi 6.
Hadi sasa, baada ya usajili wa Norgaard, hilo litafanya kikosi cha kwanza cha Arsenal sasa kuwa na wachezaji tisa wenye vimo vinavyozidi futi 6. Mipira ya juu yote ni yao.
Wakati anasajiliwa Merino, kulikuwa na kejeli Arsenal inatengeneza kikosi cha timu ya mpira wa kikapu kutokana vimo vya wachezaji wake, lakini baada ya hapo chama hilo la Emirates, lilikwenda kufunga mabao 21 iliyotokana na mipira ya kutenga, yasiyohusisha mikwaju ya penalti kwa msimu uliopita.
Kuhusu Norgaard, takwimu zinaonyesha wazi kile ambacho Arsenal itakwenda kuvuna kwa mchezaji huyo atakapoingia kwenye kikosi chao. Akiwa Brentford msimu uliopita, Norgaard alikuwa na wastani wa 2.7 wa kushinda vita ya kugombea mipira ya juu kwa dakika 90. Ukilinganisha na Partey – mwenye kimo cha futi 6 na inchi 1 – alikuwa na wastani wa 1.8, na Jorginho alikuwa na wastani wa 1.
Norgaard alikuwa na wastani wa 1.6 wa kufanikiwa kwenye tackles kutoka kwenye tackles 2.5 kwa kila mechi. Licha ya kuonyeshwa kadi nane za njano katika mechi 34 alizocheza Ligi Kuu England msimu uliopita, ukilinganisha na Partey, aliyeonyeshwa nne katika mechi 35 na Jorginho tano katika mechi 15 – Norgaard alicheza faulo chache ndani ya dakika 90. Kinachovutia, kadi hizo mbili alionyeshwa kwenye mechi dhidi ya Arsenal, nyumbani na ugenini, ikiwamo ile aliyomchezea rafu Gabriel Martinelli, ambayo wengi waliamini ilistahili kuwa kadi nyekundu.
Kwenye kushambulia Norgaard ndiyo balaa zaidi na sasa safu hiyo ya kiungo ya Arsenal itakuwa na wakali wenye uwezo wa kufunga kwa staili zote wakiwamo Zubimendi, Declan Rice na Martin Odegaard. Mechi yake ya kwanza Brentford kwenye ligi, Agosti 2021, Norgaard alifunga kwa kichwa dhidi ya timu ya Arteta kwa mipira wa kurusha katika ushindi wa 2-0 – hivyo kuhamia Arsenal, ambako anakwenda kufanya kazi na kocha hodari wa mipira iliyokufa, Nicolas Jover hilo litamfanya Norgaard kuwa balaa zaidi.
Kwa maana hiyo, ni rahisi kusema kwa msimu ujao, usiwaruhusu Arsenal kuja kupiga mipira iliyokufa karibu na goli lako, watakupa maumivu. Norgaard alifunga mabao matano na kuasisti mara nne msimu uliopita, huku mabao matatu akifunga kwa kichwa.
UTAPITA WAPI JUU
-William Saliba: Futi 6, inchi 4.
-Kai Havertz: Futi 6, inchi 4.
-Gabriel: Futi 6, inchi 3.
-Declan Rice: Futi 6, inchi 2.
-Mikel Merino: Futi 6, inchi 2
-Jakub Kiwior: Futi 6, inchi 2.
-Ben White: Futi 6, inchi 1.
-David Raya: Futi 6, inchi 0.