Konate aingia anga za Real Madrid, dili ni mwakani
Muktasari:
- Konate ambaye mkataba wake unamalizika mwisho wa msimu ujao, amekuwa katika rada za Madrid dirisha hili lakini changamoto kubwa imekuwa ni Liverpool ambayo haitaki kumuuza kwa sasa na ina imani atasaini mkataba mpya.
REAL Madrid iko tayari kusubiri hadi msimu ujao ili kumsajili beki wa Liverpool na timu ya taifa ya Ufaransa, Ibrahima Konate, mwenye umri wa miaka 26, kwa uhamisho wa bure.
Konate ambaye mkataba wake unamalizika mwisho wa msimu ujao, amekuwa katika rada za Madrid dirisha hili lakini changamoto kubwa imekuwa ni Liverpool ambayo haitaki kumuuza kwa sasa na ina imani atasaini mkataba mpya.
Mabosi wa Madrid wanahitaji kuboresha timu yao baada ya kufanya vibaya msimu uliopita na moja kati ya maeneo ambayo yanaonekana kuwa na udhaifu ni safu ya ulinzi.
Konate anadaiwa kutamani sana kutua Madrid lakini hana mpango wa kulazimisha hilo kutokea na anasubiri kuona ikiwa timu hiyo itafikia makubaliano na Liverpool.
Madrid inataka kukamilisha dili la staa huyu kama ilivyofanya kwa Trent Alexander Arnold ambaye ilipata kwa usajili huru katika dirisha hili.
Katika msimu uliopita staa jhuyu alicheza mechi 42 za ,michuano yote na kufunga mabao mawili.
Ripoti zinaeleza Liverpool inafikiria kuanzisha mazungumzo na wawakilishi wa beki huyu kwa ajili ya kumsainisha mkataba mpya.
William Saliba
REAL Madrid inamfuatilia kwa karibu beki wa Arsenal na timu ya taifa ya Ufaransa, William Saliba,24, ili kumsajili dirisha hili. Saliba ambaye mkataba wake na Arsenal unamalizika mwaka 2027, amekuwa akitajwa kuwa katika rada za Madrid kwa muda mrefu lakini ameonyesha kuwa na mpango wa kubakia Arsenal. Beki huyu ambaye ni miongoni mwa wachezaji tegemeo wa Arsenal, msimu uliopita alicheza mechi 51 za michuano yote.
James McAtee
MANCHESTER City inahitaji kiasi kisichopungua Pauni 35 milioni ili kumuuza kiungo wao raia wa England, James McAtee,22, katika dirisha hili. Staa huyu ambaye mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwakani, anawindwa na timu kibao ikiwemo West Ham na Eintracht Frankfurt. McAtee anadaiwa kuomba mwenyewe kuondoka kwa ajili ya kujiunga na timu ambayo itampa nafasi kubwa ya kucheza kwa msimu ujao.
Mateo Joseph
LEEDS United inasubiri ofa nono ili kumuuza mshambuliaji wao, Mateo Joseph,21, na kupata pesa za kumsajili mshambuliaji wa Fulham, Rodrigo Muniz, mwenye miaka 24. Joseph ambaye anahusishwa sana na Celta Vigo inayoshiriki La Liga, mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwaka 2028. Akiwa na Leeds msimu uliopita alicheza mechi 41 za michuano yote, akafunga mabao matatu na kutoa asisti nne.
Francesco Pio Esposito
INTER Milan imekataa ofa kutoka kwa Manchester United inayohitaji saini ya mshambuliaji wao wa kimataifa wa Italia, Francesco Pio Esposito, mwenye umri wa miaka 20, katika dirisha hili. Vigogo wa Inter wamekataa ofa hiyo kwa sababu hawahitaji kumruhusu fundi huyu aondoke lakini wanaweza kufikia uamuzi huo ikiwa itapokea ofa nono. Mkataba wa sasa wa Esposito, unatarajiwa kumalizika mwaka 2030.
Bryan Mbeumo
MSHAMBULIAJI wa Brentford na timu ya taifa ya Cameroon, Bryan Mbeumo, mwenye umri miaka 25, amefaulu vipimo vya afya kwa ajili ya kujiunga na Manchester United na hivyo dili hilo lipo katika hatua za mwisho kukamilika. Mbeumo ambaye mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2026, msimu uliopita alicheza mechi 42 za michuano yote na kufunga mabao 20.
Illia Zabarnyi
TOTTENHAM iko tayari kulipa kiasi kinachohitajika na Bournemouth ili kuipata saini ya beki wa timu hiyo, Illia Zabarnyi,22. Zabarnyi ni miongoni mwa wachezaji walioonyesha kiwango bora msimu uliopita na kuzivutia timu nyingi barani Ulaya. Mkataba wa sasa wa staa huyu unatarajiwa kumalizika mwaka 2029, msimu uliopita alicheza mechi 39 za michuano yote.
Jacob Ramsey
NOTTINGHAM Forest ndiyo inayoongoza katika vita ya kuiwania saini ya kiungo wa Aston Villa, Jacob Ramsey, mwenye umri wa miaka 24, katika dirisha hili. Ramsey ni miongoni mwa wachezaji waliofanya vizuri katika msimu uliopita ambapo amecheza mechi 46 za michuano yote. Mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2027.