Kocha England hacheki na wowote
Muktasari:
- England ilipata moja ya matokeo bora kabisa katika miaka ya hivi karibuni baada ya kuichapa Serbia 5-0, na ilifanya hivyo bila wachezaji nyota kama Jude Bellingham, Bukayo Saka, Cole Palmer na Trent Alexander-Arnold.
LONOND, ENGLAND: KOCHA wa timu ya taifa ya England, Thomas Tuchel ameahidi kuendelea kuwachukua wachezaji wanaoonyesha kiwango bora tu na hatojali hata kama ataacha kuwachezesha au kuwaita wachezaji wenye majina makubwa.
England ilipata moja ya matokeo bora kabisa katika miaka ya hivi karibuni baada ya kuichapa Serbia 5-0, na ilifanya hivyo bila wachezaji nyota kama Jude Bellingham, Bukayo Saka, Cole Palmer na Trent Alexander-Arnold.
Morgan Rogers, Noni Madueke na Elliot Anderson walicheza kwa kiwango cha juu na kujihakikishia nafasi, huku Tuchel akiahidi ushindani mkali wa namba katika kikosi chake kuelekea Kombe la Dunia mwakani.
Tuchel alisisitiza kuwa anataka kutengeneza kikosi cha idadi ndogo ya wachezaji ili kuwe na msukumo chanya kambini na wachezaji waone kila wanapoitwa katika timu ya taifa ni heshima kubwa.
Vilevile alionyesha wazi kuwa yuko tayari kufanya uamuzi mgumu na atafanya hivyo tena kuelekea kwenye Kombe la Dunia lijalo.
Kocha huyo wa England alisema: “Mimi huwa jasiri kila wakati. Mnajua hilo. Lakini siwezi sasa kuzungumzia majina ya kufikirika ambayo yanaweza kuachwa katika Kombe la Dunia. Tusubiri tuone nani yuko fiti na atakayepatikana. Nafikiri tayari tumefanya uamuzi wa kishujaa. Tuliita kikosi cha wachezaji 21 tu ili kuhakikisha ushindani unabaki. Ikiwa uko kambini, lazima uwe katika tabia bora, umbo bora, na fomu bora.”
“Ni heshima kuwa kambini na kupigania nafasi yako. Ikiwa unaweza kuwasaidia wengine kuwa bora na kukua, basi huo ndio msingi wetu.”
Tuchel pia alisema ushindi wa Serbia umeonyesha wazi umuhimu wa mshikamano na kupambana kwa ajili ya timu.
“Ushirikiano, juhudi tulizoonyesha na kusaidiana wakati wa mchezo ilitubeba. Hatukuacha kukimbia pale tulipokuwa tuna mpira au laa na hatukukata tamaa.”