Kocha DRC afungiwa miaka 25 unyanyasaji wa kingono
Muktasari:
- Jonathan Bukabakwa, anayejulikana kwa jina la Messi, pia ameamriwa kulipa faini ya ziada ya Dola 15,000 (takriban Sh39.7 milioni) baada ya gazeti la The Guardian la Uingereza kufichua kuwa alikuwa akiendelea kufanya kazi na wachezaji wadogo licha ya kufungiwa.
ZURICH, USWISI: Kocha Jonathan Bukabakwa, raia wa DR Congo aliyefungiwa kujihusisha na soka kwa miaka 20 na Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) kutokana na unyanyasaji wa kingono dhidi ya mtoto, ameongezewa adhabu ya miaka mitano hadi mwaka 2048.
Jonathan Bukabakwa, anayejulikana kwa jina la Messi, pia ameamriwa kulipa faini ya ziada ya Dola 15,000 (takriban Sh39.7 milioni) baada ya gazeti la The Guardian la Uingereza kufichua kuwa alikuwa akiendelea kufanya kazi na wachezaji wadogo licha ya kufungiwa.
Shirikisho la Soka la DR Congo (FECOFA) na Racing Club Baki, ambako Bukabakwa alikuwa akifundisha, zimepigwa faini ya Dola 50,000 (takriban Sh132.3 milioni) kila moja na Kamati ya Maadili ya FIFA kwa kushindwa kutekeleza uamuzi wa kumfungia kocha huyo miaka 20 mwaka 2023.
FECOFA pia imeagizwa kuanzisha mpango mpana wa elimu, uzingatiaji wa kanuni na ufuatiliaji kwa viongozi wake, klabu zilizo chini yake na wanachama waliosajiliwa ili kuhakikisha tukio kama hilo halijirudii.
“Shirikisho la Soka la DR Congo, Racing Club Baki (zamani ikijulikana kama Esperanto FC), na kocha Jonathan Bukabakwa wamekutwa na hatia ya kushindwa kutekeleza uamuzi uliotolewa na Kamati ya Maadili ya FIFA Oktoba 18, 2023,” ilisema taarifa ya FIFA.
Bukabakwa, ambaye awali alifundisha timu za vijana katika maeneo ya Limpopo na Malabo, alipatikana na hatia ya kuwafanyia watoto unyanyasaji wa kingono na mamlaka za DR Congo, na aliachiliwa kutoka gerezani mwaka jana.
Uchunguzi uliofanywa na The Guardian, mwezi Agosti, ulifichua kuwa kulikuwa na video zilizomuonyesha akiwafundisha wachezaji vijana katika Klabu ya Esperanto iliyopo eneo la Limete jijini Kinshasa, mji mkuu wa nchi hiyo.
Vyanzo vya habari vya eneo hilo vilithibitisha kuwa alikuwa akionekana mara kwa mara akiwaongoza wachezaji kwenye uwanja wa shule.
Bukabakwa hakukanusha kuendelea kuwafundisha wachezaji vijana, lakini alidai kuwa hakuwahi kupewa taarifa kuhusu adhabu yake ya FIFA.
Amesema kwamba hakuwahi kuhojiwa wala kupokea mawasiliano yoyote kutoka kwa chombo hicho kinachosimamia soka duniani, akikanusha tuhuma zilizokuwa zikimkabili. Kesi hiyo imeibua maswali zaidi kuhusu ulinzi wa watoto katika soka la DR Congo, pamoja na uwezo wa mamlaka kuhakikisha watu waliofungiwa hawaendelei kujihusisha na mchezo huo.
Bukabakwa alisimamishwa kwa muda na FECOFA Novemba 2022, kufuatia taarifa za vyombo vya habari kuhusu madai ya unyanyasaji wa kingono ulioenea nchini DR Congo. Makocha wengine kadhaa pia walisimamishwa kwa muda wakati huo, ingawa uchunguzi kuhusu baadhi ya kesi hizo haukupata ushahidi wa kutosha kuchukua hatua zaidi dhidi yao kupitia FECOFA au FIFA.
Veron Mosengo-Omba, aliyechaguliwa kuwa rais wa FECOFA mwezi Mei, ameahidi kuzifanyia kazi upya kesi zilizopita mara tu atakapokuwa ameunda tena kamati ya nidhamu. FECOFA ilikuwa chini ya kamati ya urekebishaji iliyoteuliwa na FIFA kuanzia 2023 hadi Mosengo-Omba alipochaguliwa.
“Tunahakikisha kuwa hakuna mtu anayefanya mambo ya aina hii atakayeruhusiwa kujihusisha na soka katika nchi hii,” amesema.