Klabu UIaya zamiminika kumgombania Ivan Toney
Muktasari:
- Toney mwenye umri wa miaka 29, anaonekana kuwa tayari kurudi England lakini mshahara anaohitaji unaonekana kuwa kikwazo.
KLABU kadhaa za Ligi Kuu England ambazo ni pamoja na Tottenham Hotspur na Aston Villa zinaonyesha nia ya kumsajili straika wa kimataifa wa England Ivan Toney anayeichezea Al-Ahli ya Saudi Arabia.
Toney mwenye umri wa miaka 29, anaonekana kuwa tayari kurudi England lakini mshahara anaohitaji unaonekana kuwa kikwazo.
Toney kwa zasa analipwa zaidi ya pauni 350,000 kwa wiki, na anaonekana kuwa na uwezekano mkubwa wa kutua Spurs ambayo inafundishwa na kocha wake wa zamani Thomas Frank.
Mkataba wa sasa wa Toney unatarajiwa kumalizika mwaka 2028 na tangu kuanza kwa msimu huu amecheza mechi 15 za michuano yote na kufunga mabao 11.
Tayari, kocha Frank ameshaanza kufanya mawasiliano binafsi na Toney ili kumshawishi akubali kutua katika kikosi chao na tayari fundi huyu amekubali, hivyo kinachosubiriwa ni makubaliano ya kimkataba.
Kennet Eichhorn
MANCHESTER United imeingia katika vita dhidi ya klabu nyingine kubwa barani Ulaya ikiwamo Real Madrid, Barcelona, Paris Saint-Germain na Bayern Munich katika mbio za kumsajili kiungo kinda wa Hertha Berlin, Kennet Eichhorn, mwenye umri wa miaka 16. Eichhorn amekuwa akivutia klabu nyingi kutokana na uwezo mkubwa alioonyesha akiwa na timu za vijana na kikosi cha wakubwa. Inasemekana ana kipengele kinachomwezesha kuondoka endapo timu inayomhitaji italipa Pauni 12 milioni.
Myles Lewis-Skelly
EVERTON, Fulham, West Ham United na Nottingham Forest zinafuatilia kwa karibu maendeleo ya beki wa kushoto wa Arsenal, Myles Lewis-Skelly mwenye umri wa miaka 19.
Staa huyu ameonyesha nia ya kutaka kuondoka ili kupata nafasi zaidi ya kucheza tofauti na ilivyo sasa.
Ripoti zinadai fundi Myles anataka kuondoka hata kwa mkopo wa nusu msimu ili kufufua matumaini ya kuitwa katika kikosi cha timu ya taifa ya England cha Kombe la Dunia 2026.
Casemiro
KOCHA wa Manchester United, Ruben Amorim, ameonyesha nia ya kumbakisha kiungo wao wa kimataifa wa Brazil, Casemiro ambaye mkataba wake unaisha mwisho wa msimu huu. Amorim amevutiwa na huduma ya mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 33, lakini vigogo wa timu hiyo wanataka akubali kupunguza mshahara ili apewe mkataba mpya. Casemiro kwa sasa anakunja takribani Pauni 350,000 kwa wiki na ameambiwa akubali kulipwa Pauni 200,000.
Nico Schlotterbeck
BORUSSIA Dortmund ina matumaini ya kumbakisha beki wake wa kimataifa wa Ujerumani, Nico Schlotterbeck, 25. Staa huyu amekuwa akiwindwa na vigogo mbalimbali barani Ulaya ikiwa pamoja na Bayern Munich na Liverpool.
Inaelezwa Mjerumani huyu mwenye umri wa miaka 25 hana furaha katika kikosi cha Dortmund, hivyo anataka kuondoka ili kupata chagamoto mpya sehemu nyingine.
Moises Caicedo
CHELSEA inajipanga kumpa mkataba mpya kiungo wake kutoka Ecuador, Moises Caicedo, 24, kutokana na mchango wake mkubwa katika timu. Ripoti kutoka Sky Sports zinaeleza kuwa licha ya mkataba wa fundi huyu kuwa unamalizika mwaka 2031, Chelsea inataka izidi kumuongeza kwa sababu imeona timu mbalimbali kama Real Madrid na Paris Saint-Germain zimeingia sokoni kutafuta viungo.
Joshua Zirkzee
EVERTON inatafuta mshambuliaji mpya kwa dirisha lijalo la usajili la Januari na imemweka katika rada straika wa Manchester United na timu ya taifa ya Uholanzi, Joshua Zirkzee, 24. Zirkzee, ambaye amesajiliwa na United akitokea Bologna anahusishwa kuondoka kwa sababu hapati nafasi ya kucheza jambo linalofifisha matumaini yake ya kuitwa katika kikosi cha Kombe la Dunia.
Conor Gallagher
MANCHESTER United inapanga kusajili kiungo mpya Januari mwakani na tayari ina orodha ya wachezaji sita ambao miongoni mwao ni pamoja na Conor Gallagher kutoka Atletico Madrid, Adam Wharton wa Crystal Palace na Elliot Anderson kutoka Nottingham Forest. Mashetani hawa wekundu wanataka kuongeza ubunifu katikati mwa uwanja.