Kitambaa cha unahodha chazua mzozo Liverpool
Muktasari:
- Tukio hilo linaaminika kuhususu uteuzi wa mchezaji aliyepaswa kuvaa kitambaa cha unahodha baada ya Szoboszlai kutolewa nje ya uwanja.
NEW YORK, MAREKANI: Wachezaji wa Liverpool, Curtis Jones na Dominik Szoboszlai, walioonekana wakizibana vikali uwanjani baada ya kumalizika kwa mchezo wa kirafiki ambao Liverpool iliifunga Wrexham bao 1-0 kwenye Uwanja wa Yankee jijini New York, Marekani, wamezua sintofahamu juu ya nidhamu kikosini.
Tukio hilo linaaminika kuhususu uteuzi wa mchezaji aliyepaswa kuvaa kitambaa cha unahodha baada ya Szoboszlai kutolewa nje ya uwanja.
Katika mchezo huo, Szoboszlai alitoa pasi ya bao lililofungwa na Rio Ngumoha kabla ya kutolewa, na alipokuwa anatoka uwanjani alivua kitambaa cha unahodha na kumkabidhi Kostas Tsimikas, ambaye alikuwa ameingia kipindi cha pili.
Baada ya filimbi ya mwisho, Szoboszlai na Tsimikas walionekana wakijadiliana jambo huku wakirushiana maneno makali na video za tukio hilo zilisambaa kwenye mitandao ya kijamii.
Ingawa sababu halisi ya mabishano hayo haijawekwa wazi, mashabiki wengi wamehusisha tukio hilo na uamuzi wa Szoboszlai kumpa Tsimikas kitambaa cha unahodha badala ya Jones, ambaye ni zao la akademi ya Liverpool.
Jones alionekana mwenye hasira wakati akizungumza na Szoboszlai kabla ya baadhi ya wachezaji kuingilia kati ili kutuliza hali.
Baadaye, Tsimikas aliungana kwenye mazungumzo hayo na kutupa kitambaa cha unahodha chini. Jones alikiokota na baadaye alimkumbatia Szoboszlai, ishara iliyoonyesha kuwa hali ilitulia kabla ya kila mmoja kuondoka.
Alipoulizwa kuhusu tukio hilo katika mkutano na waandishi wa habari baada ya mechi, Szoboszlai hakutaka kulizungumzia moja kwa moja.
“Baadhi ya wachezaji wameondoka, na ingawa huenda sisi si wakubwa zaidi kwenye kikosi, tumekuwa hapa kwa muda mrefu,” alisema.
“Sote tuna lengo moja na tunataka yaliyo bora kwa klabu na kwa kila mmoja wetu. Tunaye nahodha wetu, Virgil van Dijk, na tutamfuata pamoja na maelekezo ya kocha kila wakati.”
Aliongeza: “Ninaamini ninaweza kuzungumza kwa niaba ya kila mmoja kwamba tunataka kufanikiwa msimu huu.”
Ziara ya maandalizi ya Liverpool nchini Marekani itahitimishwa Jumapili kwa mchezo dhidi ya Leeds United jijini Chicago, kabla ya kucheza mechi nyingine za kirafiki dhidi ya Monaco na Como.