Kisa Tevez: Ronaldo, Messi kucheza pamoja?
Muktasari:
- Ronaldo na Messi wamekuwa wakishindana kwa zaidi ya miongo miwili, huku kila mmoja akijijengea heshima kubwa katika historia ya mchezo huo.
BUENOS AIRES, ARGENTINA: MASTAA wawili wakubwa wa soka wa kizazi hiki, Cristiano Ronaldo na Lionel Messi wanaweza kuandika historia mpya kwa kucheza pamoja katika timu moja kwa mara ya kwanza mwisho wa mwaka huu.
Ronaldo na Messi wamekuwa wakishindana kwa zaidi ya miongo miwili, huku kila mmoja akijijengea heshima kubwa katika historia ya mchezo huo.
Ushindani wao umekuwa miongoni mwa mikikimikiki mikubwa zaidi kuwahi kutokea katika soka, wakikutana mara 37 wakiwa katika timu zao za taifa na klabu.
Hata hivyo, ripoti kutoka Argentina zinaeleza kuwa wawili hao sasa wanaweza kuunganishwa katika mazingira ya kipekee kupitia mchezo wa kumuaga aliyekuwa nyota mwenzao, Carlos Tevez.
Tevez, mwenye umri wa miaka 42, alistaafu soka mwaka 2021 akiwa katika klabu yake ya utotoni, Boca Juniors ambayo pia ndiyo klabu aliyokulia na kuanzia safari yake ya soka.
Kwa mujibu wa TYC Sports, Tevez amepanga kutumia uwanja wa Boca Juniors, La Bombonera, wenye uwezo wa kuchukua mashabiki 57,000, kwa ajili ya mchezo huo maalumu wa kumuaga rasmi akiwa na klabu hiyo.
Mchezo huo unalengwa kufanyika mwezi Desemba, ingawa tarehe kamili bado haijawekwa wazi.
Tevez ana mpango mkubwa wa kuwakutanisha baadhi ya mastaa wakubwa aliocheza nao katika maisha yake ya soka na wale aliowakaribia katika maisha yake binafsi.
Anatarajiwa kuwa na kikosi cha wachezaji 11 kitakachoundwa na marafiki zake wa karibu, huku timu pinzani ikijumuisha wachezaji ambao aliwahi kucheza nao katika hatua mbalimbali za maisha yake ya soka.
Jambo linalovutia zaidi ni uwezekano wa kuwa na Messi na Ronaldo katika mchezo huo.
Tevez aliwahi kucheza pamoja na Messi katika timu ya taifa ya Argentina, huku pia akishirikiana na Ronaldo kwa misimu miwili wakati wote walipokuwa Manchester United.
Mbali na Manchester United, Manchester City na Juventus pia zinatajwa kuwa miongoni mwa klabu ambazo wachezaji wake wanaweza kuwakilishwa katika mchezo huo.
Inadaiwa kuwa Tevez analenga kuwaalika takribani wachezaji 60 kwa ajili ya tukio hilo maalumu.
Hata hivyo, maandalizi bado yako katika hatua za awali na haijafahamika Messi angecheza upande gani iwapo angekubali mwaliko huo.
Kwa sasa Messi akikipiga Inter Miami nchini Marekani huku Ronaldo akiendelea kung'ara Saudi Arabia akiwa na Al Nassr ni vigumu kuona mastaa hao wawili wakicheza katika klabu moja kabla ya kutundika daluga.
Hata hivyo, mashabiki wa wawili hao wanaweza hatimaye kupata nafasi ya kuwaona wakishiriki chumba kimoja cha kubadilishia nguo, ikiwa mipango ya aliyekuwa mchezaji mwenzao,Tevez, itafanikiwa.
Tevez ameweka wazi kuwa yuko tayari kufanya kila awezalo kuhakikisha wanahudhuria.
“Leo Messi na Cristiano Ronaldo watakuwepo,” aliahidi Tevez.
“Ikiwa itabidi niende kuwachukua mwenyewe, nitafanya hivyo. Nina namba zao wote kwenye WhatsApp.”
Tevez alistaafu soka mwaka 2021, lakini hadi sasa hajawahi kuandaliwa mchezo maalumu wa kumuaga licha ya kuwa na mafanikio makubwa akiwa na klabu mbalimbali kubwa.
Mshambuliaji huyo wa zamani alicheza na kushinda mataji akiwa na Manchester United, Manchester City, Juventus na Boca Juniors, jambo linalofanya mchezo huo kuwa tukio kubwa endapo nyota aliowahi kucheza nao watajitokeza.
Kwa mujibu wa A Bola, Juan Roman Riquelme amemruhusu Tevez kutimiza ndoto yake ya kuandaliwa mchezo huo katika uwanja maarufu wa Boca Juniors, La Bombonera.
Mbali ya Messi na Ronaldo, mastaa wengine wanaotarajiwa kupewa mwaliko ni pamoja na Wayne Rooney, Rio Ferdinand, Andrea Pirlo na Gianluigi Buffon.
Iwapo mipango hiyo itatimia, La Bombonera inaweza kuwa uwanja wa tukio la kipekee, huku Messi na Ronaldo wakipata nafasi ya kushirikiana katika mazingira ambayo mashabiki wao wamekuwa wakiyatamani kwa miaka mingi.
Iwapo Ronaldo na Messi watashiriki, mashabiki watapata nafasi adimu kuwaona mastaa hao wawili wakicheza upande mmoja, baada ya kutumia sehemu kubwa ya maisha yao ya soka wakiwa wapinzani.
TEVEZ NA MESSI
Mechi walizocheza pamoja: 47
Messi alimsaidia Tevez kufunga: 6
Tevez alimsaidia Messi kufunga: 4
TEVEZ NA RONALDO
Mechi walizocheza pamoja: 80
Tevez alimsaidia Ronaldo kufunga: 4
Ronaldo alimsaidia Tevez kufunga: 5
MATAJI YA TEVEZ
Manchester United
Ligi Kuu England: 2007/08, 2008/09
Ligi ya Mabingwa Ulaya: 2007/08
EFL Cup: 2008/09
Manchester City
Ligi Kuu England: 2011/12
FA Cup: 2010/11
Juventus
Serie A: 2013/14, 2014/15
Coppa Italia: 2014/15
Boca Juniors
Primera Division: 2003/04, 2015, 2016/17, 2017/18, 2019/20