Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Messi ameivua jezi ya Argentina tusimame tupige makofi

PAZIA Pict


WAMAREKANI bado wanapigana na Iran, inashangaza sana. Bado inashangaza. Lionel Messi amestaafu kuvaa jezi ya Argentina. Haishangazi. Zamani hili la pili lingeshangaza, halafu hilo la kwanza lisingeshangaza.


Messi ameachana na jezi ya Argentina. Tunamdai nini? Hakuna. Kitu cha haraka ambacho wataamini kwamba kimesababisha Messi aachane na timu ya taifa ya Argentina ni kwamba alifiwa na baba yake, Jorge Messi wiki chache zilizopita.


Naamini katika hili. Alikaririwa kwamba iliyopita majuzi ingekuwa michuano yake ya mwisho ya Kombe la Dunia. Lakini kuna michuano gani mingine mikubwa ambayo inaikabili Argentina baada ya kombe hili la dunia? Ni Copa Amerika ambayo inafanyika mwaka 2028.

Messi ameshatwaa Kombe la Dunia mara moja na ameshatwaa Copa Amerika mara mbili. Kwanini asubiri michuano ya Copa Amerika 2028 akiwa na umri wa miaka 41? Messi sio mbinafsi. Sidhani kama angesubiri hilo.

PAZI 01

Naamini tangazo lake la kustaafu soka lingekuja muda wowote ule hata kama baba yake asingefariki dunia. Ambacho kinanigawanya hisia ni maisha yake ya soka ngazi ya klabu. Baada ya mzee wake kufariki Messi alitoa Ishara ya kwamba angeweza kustaafu mchezo wa soka jumla jumla. Nadhani kilichomzuia ni ukweli kwamba ana mkataba na Klabu ya Inter Miami pale Marekani. Kunakuwa na mambo mengi ndani ya  mkataba wa mchezaji kama Messi anapocheza soka. Hawezi kustaafu mpira ghafla ghafla. Yeye ni nembo ya Inter Miami na ni nembo ya Ligi Kuu Marekani.

Kuna mabilioni ya pesa ambayo yanaingia Inter Miami na yanaingia katika soka la Marekani kwa sababu yake, na kuna mabilioni ya pesa yanaingia pia kwake. Nadhani mabilioni yanayoingia kwake sio shida sana. Tatizo ni pesa zinazoingia kwa wengine ambao wana mikataba naye.

Kama ingekuwa hiyari yake na kama ingekuwa amemaliza mkataba wake ni wazi kwamba Messi angetangaza kustaafu soka. Amebakisha nini zaidi? Hakuna. Ameshinda kila kitu ambacho mchezaji wa mpira wa miguu anapaswa kushinda duniani. Kuanzia tuzo binafsi mpaka zile za timu alizocheza.

PAZI 02

Huku katika timu ya taifa kustaafu kwake kunatukumbusha mambo kadhaa. Jambo la kwanza ni kwamba mchezaji bora wa muda wote duniani alifanikiwa kutwaa Kombe la Dunia. Miaka minne iliyopita alitwaa kKombe la Dunia pale Doha na maandiko yalitimia.

Jambo la pili alilotukumbusha ni kwamba nyakati kadhaa huwa tunawalaumu baadhi ya wachezaji wakubwa kwamba huwa wanajituma zaidi katika klabu zao kuliko timu ya taifa. Messi aliweka uwiano kotekote. Tofauti tu ni kwamba klabuni kuna mechi nyingi kuliko timu ya taifa.

Messi aling’ara katika klabu alizocheza na pia aling’ara katika timu ya taifa ya Argentina. Anavua jezi ya Argentina baada ya kuichezea kwa miaka 21 akiwa ndiye mchezaji aliyecheza mechi nyingi zaidi katika historia ya kikosi hicho. Mechi 207.

PAZI 03

Anavua jezi ya Argentina akiwa ndiye mfungaji bora wa muda wote katika kikosi cha Argentina akiwa amefunga mabao 125. Kumbuka kwake anayemfuatia ana mabao 56 tu. Gabriel Batistuta. Kumbuka kwamba aliyeitwa mfalme wa soka nchini humo kabla ya Messi, Diego Maradona ana mabao 34 tu.

Messi pia anavua jezi ya Argentina akiwa kifua mbele, lakini anatukumbusha kutokata tamaa. Hapo zamani baada ya kukosa Kombe la Dunia 2014 aliwahi kutangaza kustaafu soka. Akashawishiwa akarudi. Hakujua kwamba Kombe la Dunia lilikuwa linamsubiri Qatar miaka kadhaa baadaye.

Kustaafu kwa Messi kunaacha deni pia kwa swahiba wake. Hasimu wake. Cristiano Ronaldo. Wengi tuliamini kwamba Ronaldo angestaafu soka la kimataifa baada ya michuano hii ya Kombe la Dunia. Mpaka leo hajatangaza.

PAZI 04

Tunajua ambacho kinamuumiza kwa sasa. Kwamba Messi anaondoka katika michuano hii akiwa na Kombe la Dunia wakati yeye hana. Ronaldo ana taji la Euro ambalo kwa kule Amerika Kusini ni kama Copa Amerika. Hata hivyo taji kubwa zaidi duniani ni Kombe la Dunia.

Kamari ya mwisho kwa Cristiano ilikuwa ni michuano hii iliyomalizika Marekani, Canada na Mexico. Baada ya kamari hii sioni kama kuna kamari nyingine tena. Miaka miwili ijayo Euro atakuwa na miaka 43. Miaka minne ijayo katika Kombe la Dunia atakuwa na miaka 45.

Kucheza Euro na kombe lijalo la dunia utakuwa ubinafsi mkubwa kwa Ronaldo. Lakini atakuwa anaziba vipaji lukuki ambavyo vimejaa katika soka la Ureno. Hii ni mada ya siku nyingine, lakini kwa sasa tuendelee tu kumjadili Messi namna ambavyo amevua jezi ya Argentina.

PAZI 05

Wakati huu akiondoka Argentina. Wakati huu ambapo hauwezi kujua kwamba huenda kweli atastaafu soka la kulipwa jumla. Swali ni moja tu. Kunaweza kutokea Messi mwingine duniani? Hatujui. Ni swali gumu kupita kiasi.

Wengine tuliopata kutazama mikanda ya kina Pele, Diego Maradona, Johan Cruyff na wengineo tunaamini kwamba hawakuwa na uwezo wa Messi. Kuna Messi mmoja tu. Arsene Wenger aliwahi kukiri kwamba duniani hakujawahi kuwa na mchezaji kama Messi. Yeye ni mkubwa kwetu kwa umri na ufahamu katika soka. Kwanini tumbishie?

Waargentina walipata bahati ya kuwa naye na mpaka wakati huu anaivua jezi yao anaondoka bila ya deni. Kitu pekee ambacho kilikuwa kinamtenganisha yeye na Maradona ni taji la Kombe la Dunia tu. Wakati Maradona alitwaa Azteca pale Mexico City, Messi alikuja kutwaa Doha miaka mingi baadaye. Dunia haimdai Messi. Argentina haimdai Messi.