Kisa Luis Diaz, Liverpool yakomaa na Rodrygo
Muktasari:
- Mabosi wa Liverpool wanamwangalia Rodrygo kama mbadala wa winga wao wa kimataifa wa Colombia, Luis Diaz mwenye umri wa miaka 28 ambaye anaripotiwa kuwa huenda akaondoka katika dirisha hili kujiunga na Bayern Munich.
WINGA wa Real Madrid na timu ya taifa ya Brazil, Rodrygo mwenye umri wa miaka 24, ni mmoja wa wachezaji ambao bado wanapigiwa hesabu na Liverpool kwa ajili ya kusajiliwa katika dirisha hili.
Mabosi wa Liverpool wanamwangalia Rodrygo kama mbadala wa winga wao wa kimataifa wa Colombia, Luis Diaz mwenye umri wa miaka 28 ambaye anaripotiwa kuwa huenda akaondoka katika dirisha hili kujiunga na Bayern Munich.
Tayari staa huyo ameshazungumza na mabosi wa Liverpool kuwaeleza nia yake ya kutaka kuondoka kwa ajili ya kupata changamoto mpya sehemu nyingine.
Rodrygo anataka sana kuondoka katika dirisha hili kwa sababu hayupo katika mipango ya kocha mpya Xabi Alonso ambaye ameshafanya naye mazungumzo na kumweleza hilo.
Awali, Rodrygo alikuwa katika rada za Arsenal na Bayern Munich lakini timu hizo zimerudi nyuma kutokana na ada yake ya uhamisho.
Madrid inahitaji kiasi kisichopungua Pauni 70 milioni kama ada ya uhamisho ya Rodrygo na Liverpool pia haionekani kuwa tayari kutoa kiasi hicho lakini inataka kufanya mazungumzo ili ipunguziwe bei.
Katika msimu uliopita chini ya Carlo Ancelotti Rordygo alikuwa mmoja kati ya wachezaji tegemeo na alicheza mechi 54 za michuano yote, akafunga mabao 14 na kutoa asisti 11.
Mkataba wa sasa wa fundi huyu unaisha mwaka 2028.
Samuel Lino
EVERTON imeonyesha nia ya kumsajili winga wa Atletico Madrid na timu ya taifa ya Brazil, Samuel Lino na inahitaji kumsajili katika dirisha hili. Ripoti zinaeleza staa huyo wa Atletico Madrid, ameshawaambia hadi mabosi wa timu yake kwamba anataka kuondoka katika dirisha hili na Atletico imeonyesha kuwa tayari kumwachia. Fundi huyu mwenye umri wa miaka 25, hapati nafasi ya kutosha katika kikosi cha kwanza cha Atletico na hivyo kumsukuma kuondoka.
Morgan Gibbs-White
MABOSI wa Nottingham Forest wanadaiwa hawajafurahishwa na jinsi Tottenham ilivyokuwa inatoka nje ya utaratibu katika harakati za kutaka kumsajili kiungo Morgan Gibbs-White, 25, katika dirisha hili. Kutokana na suala hilo, Forest imegoma kumuuza Morgan Spurs na badala yale itasikiliza ofa kutoka timu nyingine. Tovuti ya Daily Mail imefichua kwamba Forest ilikerwa na kitendo cha Spurs kuzungumza na mchezaji kisiri ili kumshawishi.
Igor Paixao
MABOSI wa Leeds United wameanza mazungumzo na Feyenoord na wapo tayari kuvunja benki na kumsajili winga wa kimataifa wa Brazil anayeichezea timu hiyo, Igor Paixao katika dirisha hili la majira ya kiangazi.
Paixao mwenye umri wa miaka 25 ni miongoni mwa wachezaji tegemeo katika kikosi cha kwanza cha Feynoord na anatamani sana kuondoka kutua England katika dirisha hili.
Ademola Lookman
INTER Milan bado inasubiria majibu kutoka kwa Atlanta baada ya kutuma maombi ya kutaka kumsajili mshambuliaji wa klabu hiyo na timu ya taifa ya Nigeria, Ademola Lookman kwa mkopo ambao utakuwa na kipengele ambacho kitawawezesha kumnunua jumla kwa Pauni 36 milioni mwisho wa msimu ikiwa itaridhishwa na kiwango chake. Hata hivyo, Atalanta inadaiwa kutokuwa na mpango wa kumtoa kwa mkopo na badala yake inataka kumuuza.
Garnacho
ASTON Villa, imeripotiwa kuwasilisha ombi la kumsajili winga wa Manchester United, Alejandro Garnacho, mwenye umri wa miaka 21, katika dirisha hili. Inaaminika kuwa mchezaji huyo wa kimataifa wa Argentina anaweza kupatikana kwa takriban Pauni 40 milioni katika dirisha hili. Garnacho ni miongoni mwa wachezaji ambao kocha wa Man United, Ruben Amorim ameruhusiwa kuwauza.
Evan Ferguson
AS Roma bado inaendelea kufanya mazungumzo na Brighton kwa ajili ya kuipata saini ya mshambuliaji wa klabu hiyo na timu ya taifa ya Jamhuri ya Ireland, Evan Ferguson mwenye umri wa miaka 20. Evan ambaye awali aliwahi kuhusishwa na Man United ameonyesha nia ya kutaka kuondoka kwenda Roma kwa ajili ya kupata changamoto mpya.
Giorgio Scalvini
NEWCASTLE inaendelea kupambana ili kusuka upya safu ya ulinzi na ipo katika hatua nzuri kwenye mazungumzo yao ya kumsajili beki wa Juventus na timu ya taifa ya Italia, Nicolo Savona, mwenye umri wa miaka 22, pia beki wa Atalanta mwenye umri wa miaka 21 Giorgio Scalvini wote katika dirisha hili. Howe anajaribu kusuka kikosi chake kwa ajili ya kufanya vizuri Ulaya.