Kisa kuuza kombe: Infantino angejilipa kama Haaland au Hamilton
Muktasari:
- Infantino, ambaye amekuwa akikosolewa vikali, alitikisa ulimwengu wa soka mapema wiki hii baada ya kupendekeza kuanzishwa kwa kampuni mpya iitwayo FIFA Forward Enterprise.
LONDON, ENGLAND: RAIS wa FIFA, Gianni Infantino, angeweza kujikuta akilipwa mshahara unaolingana na nyota wakubwa wa michezo duniani kama Erling Haaland, Lewis Hamilton na Stephen Curry iwapo mpango wake wa kuuza sehemu ya haki za biashara za Kombe la Dunia ungepitishwa.
Infantino, ambaye amekuwa akikosolewa vikali, alitikisa ulimwengu wa soka mapema wiki hii baada ya kupendekeza kuanzishwa kwa kampuni mpya iitwayo FIFA Forward Enterprise.
Kwa mujibu wa mpango huo, kampuni hiyo ndiyo ingesimamia shughuli zote za kibiashara na vyanzo vikuu vya mapato vya mashindano ya FIFA, ikiwemo Kombe la Dunia.
Infantino, mwenye umri wa miaka 56, alipanga kuuza asilimia 20 ya hisa za kampuni hiyo kwa wawekezaji binafsi kwa thamani inayokadiriwa kufikia Dola bilioni 4.2 (zaidi ya Sh11 trilioni za Tanzania).
Hata hivyo, mpango huo ulisitishwa baada ya mataifa yanayounda Shirikisho la Soka Ulaya (UEFA), yakiwemo England, kutishia kususia mashindano ya Kombe la Dunia endapo ungeendelea.
Kwa sasa, Infantino analipwa mshahara wa takribani Pauni milioni 2.6 kwa mwaka kama rais wa FIFA, ingawa inaelezwa kiasi hicho kiliongezeka kutokana na bonasi alizopata mwaka jana.
Lakini kama mpango huo ungefanikiwa, Infantino alitarajiwa kuwa Kamishna wa FIFA Forward Enterprise baada ya kumaliza muhula wake wa mwisho wa urais mwaka 2031.
Kwa mujibu wa gazeti la The Times, nafasi hiyo ilitarajiwa kuwa na mshahara unaokaribiana na ule wa Kamishna wa NFL, Roger Goodell, anayelipwa karibu Dola milioni 64 (zaidi ya Sh172 bilioni) kwa mwaka.
Kiasi hicho kingemuweka Infantino katika kiwango sawa cha mishahara na baadhi ya wanamichezo wanaolipwa zaidi duniani.
Kwa mujibu wa Capology, mshambuliaji wa Manchester City, Erling Haaland, anaweza kulipwa hadi Pauni milioni 45.5 kwa mwaka endapo atatimiza bonasi zote zilizowekwa kwenye mkataba wake.
Naye dereva wa Ferrari katika Formula One, Lewis Hamilton, analipwa karibu Dola milioni 60 kwa mwaka, huku nyota wa Golden State Warriors, Stephen Curry, akitarajiwa kuvuna zaidi ya Dola milioni 62.5 katika msimu ujao wa NBA.
Kwa upande wa nyota wa NFL, Patrick Mahomes, mkataba wake mpya na Kansas City Chiefs utamuingizia takribani Dola milioni 64 kwa mwaka kuanzia 2027.
Baada ya mpango huo kuporomoka, Infantino sasa anakabiliwa na shinikizo kubwa ndani ya FIFA, huku baadhi ya viongozi wakitaka ajadiliwe katika kikao cha Baraza la FIFA na wengine wakimtaka ajiuzulu kutokana na mzozo uliozuka.