FIFA yasalimu amri, yafuta m,pango wa kulipiga bei Kombe la Dunia
Muktasari:
- Rais wa Fifa, Gianni Infantino alitangaza uamuzi huo baada ya kukiri mpango huo umeleta mgawanyiko mkubwa kiasi kwamba haukuwa tena na manufaa kwa lengo lililokusudiwa.
ZURICH, USWISI: SHIRIKISHO la Soka Duniani (Fifa), limeufuta mpango wake wa kuuza sehemu ya hisa za haki za kibiashara za Kombe la Dunia kwa wawekezaji binafsi, baada ya kukumbana na upinzani mkubwa kutoka kwa mashirikisho mbalimbali ya soka na vitisho vya kususia mashindano yake.
Rais wa Fifa, Gianni Infantino alitangaza uamuzi huo baada ya kukiri mpango huo umeleta mgawanyiko mkubwa kiasi kwamba haukuwa tena na manufaa kwa lengo lililokusudiwa.
Pendekezo hilo lilizua mtafaruku mkubwa katika ulimwengu wa soka, huku Shirikisho la Soka Ulaya (UEFA) likitishia kususia Kombe la Dunia na mashindano mengine ya Fifa endapo mpango huo ungepitishwa. Mashirikisho mengine, yakiwemo la Asia (AFC) na Concacaf linalowakilisha nchi za Amerika Kaskazini, Amerika ya Kati na Karibiani, pia yalitangaza kupinga mpango huo.
Mbali na upinzani kutoka kwa mashirikisho, mmoja wa washauri wakuu wa Infantino, Carlos Cordeiro, alijiuzulu kupinga mpango huo, huku Ofisa Mkuu wa Uendeshaji wa FIFA, Kevin Lamour, akimkosoa vikali Infantino kwa kile alichokiita ukosefu mkubwa wa heshima kutokana na kujaribu kuusukuma mpango huo bila ushauriano wa kutosha.
Ripoti zinaeleza kuwa hata kampuni ya uwekezaji ya Thrive Capital, iliyokuwa inaongoza kundi la wawekezaji waliotarajiwa kushiriki kwenye mpango huo, ilianza kuwa na mashaka baada ya kuona mgogoro ulioibuka ambao ulitishia kuigawa dunia ya soka.
Katika taarifa yake, Infantino alisema: “Baada ya kusikiliza kwa makini maoni yote, imekuwa wazi kwamba mradi huu umeleta mgawanyiko ambao, bila kujali kiwango cha uungwaji mkono, hauko tena katika maslahi ya lengo lililowekwa hapo awali.”
Aliongeza kuwa dhamira ya FIFA siku zote imekuwa kuunganisha na kuendeleza mchezo wa soka, hivyo pendekezo hilo halitaendelea.
“Lengo letu limekuwa na litaendelea kuwa kuunganisha na kuboresha mchezo. Kutokana na hali hiyo, pendekezo hili halitatekelezwa. Sasa dhamira yangu ni kuwakutanisha tena wadau wote katika siku na wiki zijazo ili tuendelee kukuza soka duniani kote, hasa katika nchi zinazohitaji msaada zaidi.”
Mpango huo, ulioitwa Fifa Forward Enterprise (FFE), ulilenga kukusanya mamia ya mamilioni ya dola kwa kuuza sehemu ya haki za kibiashara za Kombe la Dunia la wanaume, Kombe la Dunia la wanawake pamoja na Kombe la Dunia la Klabu kwa wawekezaji binafsi.
Kupitia fedha hizo, FIFA iliahidi kuongeza fedha zinazogawiwa kwa mashirikisho yake 211 wanachama hadi zaidi ya dola bilioni 10. Mashirikisho yaliyokubali kushiriki yangepata pia dola milioni 20 kila moja, huku Septemba 19 ikiwa ndiyo tarehe ya mwisho ya kujiunga na mpango huo.
Hata hivyo, mpango huo ulikataliwa kwa kauli moja na mashirikisho ya Ulaya katika kikao cha dharura kilichofanyika Alhamisi. AFC na Concacaf pia yaliweka wazi msimamo wao wa kuupinga.
Ingawa Infantino bado anaungwa mkono na baadhi ya mashirikisho barani Afrika, idadi ya nchi zilizokuwa zikiupinga mpango huo ilikuwa kubwa kiasi cha kufanya isiwezekane kuupitisha kwa uhalali.
Sasa macho yanaelekezwa kwenye mustakabali wa Infantino mwenyewe, baada ya kukumbwa na uasi mkubwa ndani ya FIFA na kuporomoka kwa hadhi yake katika medani ya soka duniani.
Mashirikisho ya UEFA na mengine tayari yameanza kutafuta mgombea wa kumpinga Infantino katika uchaguzi ujao wa urais wa FIFA mwaka ujao, ambapo hapo awali alionekana kuwa na nafasi kubwa ya kushinda muhula wa nne mfululizo.
Licha ya FIFA kusisitiza hapo awali kuwa “hakuna anayeliuza soka”, shinikizo kutoka kwa wadau wa mchezo huo duniani hatimaye limeifanya taasisi hiyo kuachana na mpango huo, huku baadhi ya viongozi wa mashirikisho wakiamini kuwa kufutwa kwa mpango pekee hakutoshi, na kwamba Infantino anapaswa kuwajibika kwa mgogoro huo.