Kisa Arsenal, Gyokeres kupewa adhabu mbili
Muktasari:
- Varandas amethibitisha kuwa mshambuliaji huyo mwenye umri wa 27, hakuripoti kambini wiki hii licha ya kupewa mapumziko ya ziada hadi Jumamosi, Julai 12.
LISBON, URENO: RAIS wa Sporting Lisbon, Frederico Varandas, amethibitisha kuwa mshambuliaji wa timu hiyo Viktor Gyokeres atapewa adhabu mbili kubwa baada ya kugoma kuripoti mazoezini akishinikiza aruhusiwe kuondoka.
Varandas amethibitisha kuwa mshambuliaji huyo mwenye umri wa 27, hakuripoti kambini wiki hii licha ya kupewa mapumziko ya ziada hadi Jumamosi, Julai 12.
Hata hivyo, uvumilivu wa timu sasa umefikia ukomo na Varandas ametangaza kuwa mshambuliaji huyo anakabiliwa na faini kubwa.
Inadaiwa kuwa tayari Gyokeres ameshafikia makubaliano binafsi ya kimkataba na Arsenal, lakini kizuizi pekee kilichosalia ni ada ya uhamisho.
Arsenal bado haijafikia thamani ya pauni 69 milioni ambayo Sporting wanaitaka na Gyokeres analalamika kuwa alifanya makubalino na mabosi wa timu kwamba watamwachia kwa kiasi cha chini tofauti na hicho wanachokihitaji.
Kutokana na kushikilia msimamo wa kutaka kumuuza kwa pauni 69 milioni, Gyokeres amegoma tena kurudi kwenye timu ikiwa ni katika njia za kulazimisha vigogo hao warudi katika makubaliano waliyowekeana hapo awali.
“Tuko watulivu. Kila kitu kinaweza kuwa sawa pengine kabla ya dirisha la usajili kufungwa, tutatoa faini kubwa na kumwambia aombe msamaha kwa kikosi,” alisema Varandas alipokuwa akizungumza na shirika la habari la Ureno, Lusa.
“Hawa viongozi wanaoendesha mpango huu wanafikiri kwamba hii itanilazimisha kumwachia kwa urahisi, basi wamekosea kabisa badala yake wamefanya dili liwe gumu zaidi. Hakuna aliye juu ya maslahi ya klabu, yeyote yule.”
Gyokeres, ambaye alifunga mabao 54 msimu uliopita katika mashindano yote akiwa na Sporting, anachukuliwa kama mmoja wa washambuliaji hatari zaidi barani Ulaya kwa sasa.
Akiwa bado na miaka mitatu kwenye mkataba wake na Sporting tangu alipojiunga kutoka Coventry City kwa ada ya pauni 20 milioni mwaka 2023, mshambuliaji huyo amekuwa kwenye kiwango cha juu akifunga mabao 97 katika mechi 102 ndani ya misimu miwili.
Kabla ya kujiunga na Sporting, Gyokeres alifunga mabao 43 katika misimu miwili na nusu akiwa na Coventry, lakini hakuwahi kucheza hata mechi moja ya Ligi Kuu England akiwa na Brighton.
Ameshawahi kueleza dhamira yake ya kurudi England ili kuhakikisha anacheza Ligi Kuu England baada ya kushindwa kufanya hivyo hapo awali akiwa na Brighton.
“Ni moja ya ligi kubwa zaidi barani Ulaya,” alisema Gyokeres. “Nilikaa huko miaka kadhaa bila kucheza hata mechi moja. Kwa hiyo, bila shaka, ni jambo ningependa kulifanya. Itakuwa ni kulipiza kisasi kizuri sana.”
Kwa mujibu wa Mail Sport, kocha wa Arsenal, Mikel Arteta, alikuwa na mpango wa kumpata mshambuliaji mpya kabla ya kikosi chake kusafiri kwenda Singapore Julai 19 kwa ajili ya maandalizi ya msimu ujao.
Hata hivyo, kwa sasa, inaonekana Sporting wameshika kila karata na hawana haraka yoyote kumwachia Gyokeres.