Kisa Afcon Salah kumaliza utata Misri
Muktasari:
- Misri itahitaji kuingia kambini kabla ya kukabiliana na United Arab Emirates (UAE), Desemba 6, Jordan Desemba 9 na Nigeria Desemba 14 ikiwa ni maandalizi ya michuano hiyo ya Afcon.
LIVERPOOL, ENGLAND: SUPASTAA wa Liverpool, Mohamed Salah anajiandaa kuzungumza na kocha wa Misri, Hossam Hassan wiki ijayo ili kujaribu kuzuia mgogoro mwingine unaoweza kutokea baina ya klabu yake na timu ya taifa katika kuelekea fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon).
Misri itahitaji kuingia kambini kabla ya kukabiliana na United Arab Emirates (UAE), Desemba 6, Jordan Desemba 9 na Nigeria Desemba 14 ikiwa ni maandalizi ya michuano hiyo ya Afcon.
Kwa mujibu wa WinWin, kocha wa Misri, Hassan ana haki ya kumjumuisha Salah kwenye kikosi chake sambamba na mkali wa Manchester City, Omar Marmoush kwenye mechi hizo tatu.
Liverpool, hata hivyo itakabiliwa na mechi dhidi ya Leeds United na Brighton kwenye Ligi Kuu England na Inter Milan kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya ndani ya muda huo na Mo Salah atahitaji kucheza mechi hizo.
Na ripoti zinafichua kwamba Salah atahitaji kubaki kwenye kikosi cha Liverpool kucheza mechi hizo za kiushindani kuliko kwenda kwenye mechi za kirafiki.
Salah, 33, sasa anatarajia kuzungumza na kocha Hassan kwenye mechi za kimataifa mwezi huu, wakati Misri itakapokipiga na Uzbekistan, Novemba 14 na Algeria, Novemba 17, ambapo mechi hizo mbili za kirafiki.
Staa huyo wa zamani wa Chelsea na Roma hataki kusababisha mgongano baina ya klabu yake na timu ya taifa baada ya kile kilichotokea miaka miwili iliyopita.
Na sasa Liverpool na Misri zinapaswa kukubaliana juu ya mustakabali wa Mo Salah kumruhusu kwenda kucheza michuano ya Afcon, ambayo itaanza Desemba 21 na kukamilika Januari 18 huko Morocco.