Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kinachopaswa kufanywa Arsenal, Man United dirisha la Januari

Muktasari:

  • Shida inaanzia sehemu moja, hakuna timu inayokubali kujiweka kwenye hali ya hatari ya kuuza wachezaji wake bora katikati ya msimu.

LONDON, ENGLAND: USAJILI wa Januari ni dirisha la kijanja na gumu sana kwa klabu za soka kupata mastaa inayowataka wawepo kwenye timu zao.

Shida inaanzia sehemu moja, hakuna timu inayokubali kujiweka kwenye hali ya hatari ya kuuza wachezaji wake bora katikati ya msimu.

Katika dirisha la Januari hii, kwa klabu za Ligi Kuu England hasa kwa baadhi ya zile za Big Six, watahitaji kufanya usajili wa lazima ili kuweka mambo sawa.

Chelsea, Arsenal na Manchester United ni klabu tatu kati ya sita sita kubwa, ambazo piga ua zitahitaji kufanya usajili wa kuboresha vikosi vyao dirisha hili.

Makala haya yanahusu mchezaji mmoja kwa kila timu ambaye klabu itahitaji kumsajili ili kufikia malengo yao ya msimu.


Chelsea

Tangu ilipochukuliwa na bilionea Todd Boehly, Chelsea imekuwa bize kufanya usajili kwenye dirisha la Januari. Hata hivyo,  Chelsea licha ya kuwa na kikosi kizuri chenye mastaa wanaocheza kwa kiwango bora, bado hawana machaguo ya kutosha kwenye safu yao ya mabeki wa kati.

Siku hizi timu zinaonekana kuhitaji mabeki wa kati ambao wamekuwa na uwezo mkubwa wa kuuchezea mpira ili zianze kupanga mashambulizi yao kuanzia nyuma. Ukiichukulia Chelsea ya miaka ya nyuma ilipokuwa chini ya Jose Mourinho, yenyewe ilihitaji mabeki wa aina kama ya John Terry, ambao ni hodari kwenye kukaba na kunasa mipira kwenye miguu ya wapinzani tofauti na mabeki wa kisasa, ambao wanahitajika wenye uwezo wa kupiga pasi nyingi.

Kitu hicho kwa sasa kinakosekana kwenye kikosi cha Chelsea na ndiyo maana inaamini, staa wa Lens, Abdukodir Khusanov atakwenda kufiti vyema. Kinda huyo wa miaka 20 ndiyo kwanza msimu wake wa kwanza huko Ligue 1 ya Ufaransa, lakini tayari ameanza kuhusishwa na klabu nyingi kubwa za Ulaya. Ana nguvu, msumbufu wa washambuliaji huku umri wake ukionekana kufiti vyema kwenye mipango ya Chelsea na staili yake ya uchezaji inatajwa kwamba ni kama Terry.

Kinachoelezwa ni beki mzuri sana linapokuja suala la kukabiliana na mshambuliaji ‘one v one’, kwenye hali hiyo basi litatokea jambo moja kati ya haya mawili, upite mpira mtu abaki, au apite mtu mpira ubaki. Tatizo lake moja ambalo amekuwa akikosolewa sana ni matumizi makubwa ya nguvu, lakini kama Chelsea itamsajili Khusanov itakuwa imeingiza kitu muhimu kwenye kikosi chao ambacho imekuwa ikikosa.


Arsenal

Arsenal chini ya Mikel Arteta inahisi kwamba imeshatengeneza mazingira bora kabisa kwa ajili ya kushinda taji la Ligi Kuu England.

Mwezi uliopita ilijikuta imempoteza staa wake Bukayo Saka kutokana na majeraha, ambayo yatamfanya kuwa nje ya uwanja hadi Machi, kitu ambacho kinaweza kuwa pigo kwao kutokana na mchango wa mchezaji huyo kwenye timu.

Lakini, kitu muhimu ambacho Arsenal inakosa ni straika ambaye atakuwa anafunga na kuwatengenezea wengine nafasi za kufunga, ambaye pia atakuwa na uwezo wa kuwapa shida mabeki wa timu pinzani katika kumdhibiti. Gabriel Jesus na Kai Havertz wana viwango vizuri, lakini wawili hao hakuna hata mmoja ambaye akipangwa kwenye fowadi ya Arsenal anakuwa tishio kwa mabeki wa timu pinzani. Na hapo ndipo linapokuja suala la straika wa Newcastle United, Alexander Isak kuhusishwa na miamba hiyo ya Emirates. Fowadi huyo amefunga mabao 13 na asisti nne kwenye michuano yote msimu huu, lakini shida inayowakabili Arsenal ni kwamba bei yake ipo juu sana. Isak ni mchezaji tishio sana anapokuwa kwenye safu ya ushambuliaji na kitu kama hicho ndicho inachohitaji Arsenal ili kufikia malengo yao ya kubeba ubingwa. Isak akicheza mbele ya wabunifu kama Saka na Martin Odegaard kuna jambo litafanyika na Arsenal itakuwa kwenye nafasi nzuri ya kumaliza ukame wao wa kunyakua taji la Ligi Kuu England kwa mara ya kwanza tangu 2003-2004.


Manchester United

Katikati ya msimu wa 2024/25, Manchester United inashika nafasi ya 14 kwenye msimamo wa Ligi Kuu England, hivyo imeingia mwaka mpya ikiwa kwenye nafasi hiyo. Ilimfuta kazi kocha Erik ten Hag na kumleta kocha aliyewahi kushinda mara mbili ubingwa wa Ligi Kuu Ureno, Ruben Amorim, licha ya kwamba matokeo ya uwanjani bado hayajawa mazuri. Kwa kifupi, Man United ina ishu kadhaa za kuzikabili kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya baridi. Inahitaji kufanya usajili wa kujenga upya kikosi ili kunasa wachezaji ambao watakaweza kufiti kwenye mfumo wa kocha huyo Amorim na wenye ubora unaotakiwa kuwa nao kwa mchezaji wa Man United. Unaweza kuona timu hiyo inahitaji beki wa kati, kiungo wa kati na mshambuliaji, maeneo matatu yanayohitaji kuboreshwa kwenye dirisha hili kabla mambo hayajaendelea kuwa mabaya zaidi kwenye kikosi hicho.

Kocha Amorim anamfikiria straika wa Sporting Lisbon, Viktor Gyokeres, akiamini kwamba akitua kwenye kikosi chake atakwenda kumaliza tatizo la upatikanaji wa mabao kwenye kikosi hicho. Washambuliaji Rasmus Hojlund, Joshua Zirkzee na Marcus Rashford bado wanashindwa kufanya kile ambacho kocha Amorim anahitaji wachezaji wake wafanye uwanjani, huku kupoteza nafasi nyingi za kufunga kumeigharimu sana timu hiyo. Kocha Amorim alidai kwamba timu yake kwa sasa ipo kwenye vita ya kupambana isishuke daraja na kushinda kwenye vita hiyo unahitaji kuwa na wachezaji wa maana kama straika Gyokeres kuja kuokoa jahazi huku timu hiyo ikiwa na mchakato wa kufukuzia nafasi za kucheza michuano ya Ulaya msimu ujao.


Hitimisho

Dirisha la Januari mara nyingi wachezaji hawauzwi kwa bei zao halisi. Wachezaji wamekuwa wakiuzwa kwa bei kubwa sana. Lakini, kwa klabu za Ligi Kuu England zinazohitaji wachezaji wa kuboresha vikosi vyao hakuna namna kwamba zitapambana na kulipa kiwango chochote cha pesa kinachotakiwa ili kupata huduma za wachezaji ambao wanaamini watakuja kuongeza kitu tofauti kwenye timu zao. Shida inakuwa sehemu moja, kupata mchezaji sahihi, kwa bei sahihi ni mtihani unaowakabili makocha wengi wanaohitaji wachezaji wa kwenda kuboresha vikosi vyao kwenye dirisha hili la uhamisho wa Januari.