Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kawhi ndani ya 10 bora wanaowania MVP NBA

Muktasari:

  • All-Star Game 2026 inapigwa katika uwanja wa Intuit Dome, nyumbani kwa timu ya Los Angeles Clippers na muhimu zaidi ni maskani kwa mmoja wa wachezaji bora zaidi kwa sasa katika ligi, Kawhi Leonard ambaye wiki hii alitinga ndani ya mastaa 10 bora wanaowania u-MVP.

Los Angeles, Marekani :ACHANA na bonge la mechi linalochezwa leo, Jumapili, la mastaa wa Ligi ya Kikapu Marekani (NBA) maarufu All-Star Game 2026, nyuma ya mtangange huo kuna lile vaibu ambalo bado linaendelea kusaka mchezaji bora (MVP) wa msimu wa 2025/26 wa mashindano hayo.

All-Star Game 2026 inapigwa katika uwanja wa Intuit Dome, nyumbani kwa timu ya Los Angeles Clippers na muhimu zaidi ni maskani kwa mmoja wa wachezaji bora zaidi kwa sasa katika ligi, Kawhi Leonard ambaye wiki hii alitinga ndani ya mastaa 10 bora wanaowania u-MVP.

Je, hiyo ni sifa iliyopitiliza? Labda lakini ukizingatia kwamba Kawhi alikuwa moto kabla ya kuwapoteza wachezaji wenzake wawili mahiri na bora aliokuwa akicheza nao. Cha kushangaza zaidi ameendelea kuwa bora hata baada ya kuachana nao. Clippers waliachana na James Harden siku 10 zilizopita na Ivica Zubac Alhamisi iliyopita.

Kawhi anaingia katika mbio za tuzo ya kuwania mchezaji bora MVP akiwa katika kiwango cha juu cha ubora ambapo majuzi alitawala robo ya mwisho ya mchezo dhidi ya Houston Rockets, akionyesha uhatari kila eneo uwanjani.

Lakini, zaidi ni kwamba mchezaji huyo alikuwa hatari zaidi mwishoni dhidi ya walinzi wa Rockets waliokuwa wakimlenga yeye pekee, ambapo alifunga pointi 19 katika kipindi hicho, ikiwemo mitupo yake hatari ya sekunde za mwisho za mchezo.

Kwa sasa mwamba huyo yupo fiti baada ya mateso ya majeruhi miezi michache iliyopita na ni wazi kwamba hatimaye  hana tena kizuizi cha dakika za kucheza. Awali, mashabiki hawakuwa wamemuona Kawhi akiwa bora kwa muda mrefu kiasi hiki.

Katika vipindi vyake vya afya njema amewahi kuonyesha kuwa na kipaji cha pekee, na anastahili kuwa miongoni mwa nyota bora wanaopaswa kuangaliwa katika kizazi cha sasa kinachoendelea kushindana katika mashindano hayo bora ya kikapu.

Kocha wa Clippers, Tyronn Lue, anasema: “Kizuizi cha dakika (kwa Kawhi) kimeondoka. Anaweza kucheza dakika 38 hadi 40 kila usiku na hilo linatupa nafasi ya kushinda kila mechi huku tukishambulia kwa nguvu. Na kiulinzi tunajua anaweza kufanya nini.”

Katika kinyang'anyiro cha kuwania uchezaji bora wa NBA, miongoni mwa vigezo ni pamoja na mchezaji kuwa na kiwango bora uchezaji uwanjani, kuibeba timu, kuamua mchezo au michezo, wastani bora wa pointi za kufunga na uzuiaji mashambulizi wa kiwango cha juu.

Kawhi alifunga wastani wa pointi 29.8 Desemba 2025, 27.5 Januari na 28.9 mwezi huu. Katika mechi dhidi ya Rockets pia alipata ribaundi 12 na kupora mipira minne kutoka kwa wapinzani wao.

Licha ya Clippers kuachana na Harden na Zubac wamefanikiwa kushinda mechi tatu kati ya nne kutokana na ubora wa Kawhi akitupia pointi 31, ribaundi tisa na asisti saba dhidi ya Sacramento Kings; kisha 41-8-2 dhidi ya Minnesota Timberwolves; na jumla ya 51-20-7 katika mechi mbili dhidi ya Houston.

Kwa sasa hana tena mchezaji mwenzake wa All-Star kikosini, huku John Collins, mfungaji wa pili wa timu akiwa na wastani chini ya pointi 14 kwa mechi. Zaidi ya hapo Clippers wanacheza katika Ukanda wa Magharibi ambao una timu bora zaidi.

Clippers wako chini ya asilimia .500 msimu huu na wanapambana kubaki katika mbio za kuwania kufuzu (play-in) za ukanda huo. Hiyo ina maana kwamba Kawhi hatashinda MVP, na hata kufika playoff au kumaliza na rekodi ya ushindi itakuwa changamoto. Lakini kwa sasa, anatosha kuingia nafasi ya 10 katika orodha ya wanaowania MVP.


WIKI YA ALL-STAR

Kinachofuata wiki hii ni kwamba ligi itasimama kwa karibu wiki moja kwa mapumziko ya All-Star. Ikirejea, macho yatakuwa kwa walinzi wawili wanaowania MVP — Cade Cunningham na Jalen Brunson wakati Detroit Pistons watakapokutana na New York Knicks.

Pistons wanaongoza 2-0 katika michezo waliyokutana baina yao, lakini watamkosa Jalen Duren na Isaiah Stewart kutokana na adhabu. Cunningham atalazimika kuwa bora zaidi ili kufanya ushindani uwe 3-0. Brunson ndiye mchezaji pekee wa NBA mwenye mechi zaidi ya moja ya pointi 40 mwezi huu.

TAKWIMU MUHIMU

Katika mfano mwingine wa ubora wa Kawhi, amefunga pointi 20 au zaidi katika mechi 33 mfululizo. Pia anaongoza ligi kwa jumla ya pointi mwezi huu akiwa na wastani wa pointi 30 kwa mechi Februari, 2026.

Kuhusu ushindi dhidi ya Rockets, Lue anasema: “Huyo ndiye Kawhi. Mwisho wa mechi unajua mpira utaenda kwa nani… na aliturudisha nyumbani na ushindi.”


MCHUANO MVP KWA NAMBA

Mshindi wa MVP msimu uliopita supastaa wa Oklahoma City Thunder, Shai Gilgeous-Alexander bado anaongoza kinyang'anyiro wiki hii akiwa na wastani wa pointi 31.8, ribaundi 4.4 na asisti 6.4 kwa kila mchezo akifuatiwa na

Nikola Jokic (Denver Nuggets) mwenye pointi 28.7, ribaundi 12.3 na asisti 10.7 huku Luka Doncic (Los Angeles Lakers) akiwa na wastani wa pointi 32.8, ribaundi 7.8 na asisti 8.6.

Wengine wanaofuatia ili kukamilisha tano bora wiki hii ni Cade Cunningham (Detroit Pistons) akiwa na pointi 25.3, ribaundi 5.6 na asisti 9.6 ilhali anayefunga idadi ya wakali hao ni Victor Wembanyama wa San Antonio Spurs mwenye wastani wa alama 24.4, ribaundi 11.1 na asisti 2.6.


VITA KUWANIA MVP 6–10

6. Jaylen Brown (Boston Celtics)

7. Donovan Mitchell (Cleveland Cavaliers)

8. Anthony Edwards (Minnesota Timberwolves)

9. Jalen Brunson (New York Knicks)

10. Kawhi Leonard (LA Clippers)