Carlos alivyoingizwa chaka, sasa ahueni
Muktasari:
- Beki huyo wa zamani wa kushoto, ambaye alitwaa Kombe la Dunia akiwa na Brazil 2002, amezungumzia kwa mara ya pili jinsi alivyolazimika kupambana kurejea kutoka katika hali ya kuwa karibu hana chochote baada ya kukabidhiwa nyaraka zilizokaribia kumfilisi.
BRASILIA, BRAZIL: GWIJI wa soka wa Brazil, Roberto Carlos, amefichua kuwa alipoteza asilimia 99 ya mapato yake ya Pauni 133 milioni aliyoyapata kipindi cha kucheza soka kutokana na matatizo yaliyohusisha wakala wake wa zamani na mmoja wa wanafamilia.
Beki huyo wa zamani wa kushoto, ambaye alitwaa Kombe la Dunia akiwa na Brazil 2002, amezungumzia kwa mara ya pili jinsi alivyolazimika kupambana kurejea kutoka katika hali ya kuwa karibu hana chochote baada ya kukabidhiwa nyaraka zilizokaribia kumfilisi.
“Nilikuwa na matatizo na watu walioniacha bila fedha zozote,” alisema katika mkutano wa Portugal Football Summit, kwa mujibu wa Globo.
“Kwa sababu ya mawakala na matatizo ya kifamilia, nilipoteza asilimia 99 ya kila kitu nilichokuwa nimekipata kupitia soka. Nilifanya makosa, ndiyo maana ninawaomba wachezaji vijana wasifanye makosa kama hayo. Alhamisi nililala saa sita usiku, lakini Ijumaa nilipokea rundo la nyaraka ambazo hata sikujua kama zilikuwepo. Hapo ndipo nilipopoteza historia yangu yote,” alisema.
Carlos alitalikiana na mke waliyeishi miaka 15 mwaka 2025, hatua iliyosababisha taarifa kudai kuwa alikuwa akilala katika uwanja wa mazoezi wa Real Madrid, ambako anafanya kazi kama balozi wa klabu hiyo.
Hata hivyo, alikanusha haraka madai hayo, akiandika kupitia mtandao wa X: “Katika siku za hivi karibuni, nimeona uvumi usio na msingi kuhusu mahali ninapoishi. Ninaendelea kuishi katika makazi binafsi kwa msaada wa familia yangu. Timu yangu ya wanasheria inashughulikia madai hayo, na ninaomba faragha katika kipindi hiki.”
Kwa mujibu wa chapisho la Estadio Deportivo, makubaliano ya talaka na aliyekuwa mkewe wakati huo, Mariana Luccon, yalitarajiwa kuwa magumu kutokana na utajiri mkubwa wa Carlos, uliokadiriwa kufikia takribani Pauni 133 milioni. Walipata watoto wawili pamoja.
Kabla ya hapo, aliwahi kusema kuwa ana watoto 11 na wanawake saba tofauti, akidai: “Sasa ninaishi na Manuela na nina wengine kadhaa. Nina saba Brazil. Nina mmoja Mexico, nina mmoja Hungary anayeishi Alicante na wengine wanaishi Brazil.”
Carlos ameoa mara tatu, baada ya kufunga ndoa na Soheila Tahiri mapema mwaka huu, ambapo alistaafu soka 2012 na sasa anafanya kazi kama balozi wa Real Madrid. Alikuwa akijiandaa kwa maisha nje ya soka kabla ya kumaliza siku zake za kucheza, lakini wanjanja walimuwahi.
Wakati mmoja alikuwa akilipwa hadi Pauni 85,000 kwa wiki alipokuwa katika klabu ya Urusi, Anzhi Makhachkala, lakini ilimbidi kumtegemea rafiki yake kumsaidia kurekebisha hali yake ya kifedha.
“Nilikuwa nikifikiria maisha yangu baada ya soka. Inamaanisha kujenga urithi kama mchezaji na kutumia taswira yako. Nilipoamua kuacha kucheza soka, tayari nilikuwa na leseni ya mkurugenzi wa michezo na nilikuwa nikifanya kazi na chapa nyingi,” anasema mchezaji huyo.
Inaonekana alikuwa na nafasi nyingine ya kujipanga upya, na sasa hali yake ya kifedha imeimarika zaidi huku akiendelea kufanya kazi na klabu yake ya zamani.