Hili ndio jeshi la fadlu Yanga
KLABU ya Yanga imemtambulisha rasmi aliyekuwa Kocha Mkuu wa Simba raia wa Afrika Kusini, Fadlu Davids huku akishuka na wasaidizi wake ambao wasifu wao umejaa akiwemo Darian Wilken na mchambuzi wa video za mechi (Video Match Analyst / Performance Analyst), Mueez Kajee ili kujenga jeshi jipya kwenye kikosi hicho cha Jangwani.
Darian na Mueez waliwahi kufanya kazi pamoja na Kocha Mkuu, Fadlu Davids tangu akiwa Simba, Maritzburg United FC ya kwao Afrika Kusini, Raja Casablanca ya Morocco na sasa wanaungana tena katika kikosi hicho cha mabingwa watetezi hapa nchini.
Hata hivyo, Darian anaonekana kuwa na CV kubwa akionekana kuwa aliwahi kutumika kwenye kikosi cha Orlando Pirates cha Afrika Kusini kama msaidizi huku akifanya kazi na makocha wakubwa kama Rulani Mokwena, Milutin Sredojevic, pamoja na Josef Zinnbauer.
Kwa upande wa Mueez yeye wasifu wake siyo mkubwa sana kwani ametumika zaidi akiwa na Fadlu kwenye kikosi cha Raja pia akifanya kazi na Zinnbauer.
Wengine wanaoungana na Fadlu Yanga ni Kocha wa Utimamu wa Mwili na Viungo (Fitness Coach), Riedoh Berdien aliyewahi pia kufanya naye kazi akiwa Simba, akienda kuchukua nafasi ya Tshephang Mokaila ‘Chyna’, aliyeondoka tangu, Oktoba 24, 2026.
Huyu anaweza kuwa mwamba zaidi kuliko wengine wote, akiwa ameshafanya kazi kwenye timu za taifa mbalimbali na anawajua wachezaji wengi akiwemo kipa wa Yanga Djigui Diarra kwa kuwa alishafanya kazi na timu ya Taifa ya Mali, Gambia, Togo, Botswana, Bangladesh, Trinidad & Tobago, Guyana na Philippines.
Kocha huyo anakumbukwa pia na mashabiki wa Yanga kwa kuwa alishapita kwenye timu hiyo ingawa hakukaa muda mrefu, akiwa pia aliifundisha Mamelodi Sundowns,Chippa United, Free State Stars, na Bloemfontein Celtic, akiwa kwenye timu zote ameshafanya mambo makubwa.
Katika mapendekezo hayo, mwingine aliyependekezwa na Fadlu ni Kocha wa Makipa, Milton Nienov aliyewahi kufanya kazi na Didier Gomes wakiwa Simba, japo dili hilo litakamilika ikiwa aliyepo kwa sasa, Mnigeria Greg Etaif ataondoka kikosini baada ya kuona sura mpya zinaingia.
Huyu naye siyo mgeni kwa mashabiki wa Yanga, kwani alitumika kwenye kikosi hicho kwa muda mfupi akiwa na kocha Nassredine Nabi, lakini pia amewahi kufanya kazi kwenye vikosi vya Polokwane City, timu ya Taifa ya Botswana na kikosi cha El Mereikh cha Sudan, akiwa anatajwa kama mmoja kati ya makocha wa makipa wenye uzoefu wa hali ya juu kwenye soka la Afrika.
Taarifa kutoka ndani ya Yanga, zinadai ujio wa makocha hao ni pendekezo la Fadlu ambaye amewataka kufanya nao tena kazi na amekuwa nao sehemu nyingine yakiwa ni makubaliano kuanzia kwenye mkataba wake, akiamini uhusiano wao mzuri wa kufundisha timu mbalimbali, utakuwa ni chachu zaidi ya kuleta mafanikio ya kikosi hicho.
Kocha huyo amejiunga na Yanga akitokea mapumzikoni Afrika Kusini baada ya kauchana na Raja Casablanca ya Morocco, Fadlu alijiunga na Simba kwa mara ya kwanza, Julai 5, 2024, kisha kuondoka Septemba 22, 2025, kwa makubaliano ya pande mbili, ikiwa alidumu kikosini kwa siku 444.
Kocha huyo ambaye alikwenda Raja na kukaa kwa muda mfupi bila kupata mafanikio yoyote, amejiunga na Yanga akichukua nafasi iliyoachwa na raia mwenzake wa Afrika Kusini, Manqoba Mngqithi aliyeondoka Oktoba 24, 2026, baada ya kusitishiwa mkataba wake.
KUWEKA KAMBI ZANZIBAR
Wakati Fadlu akitua rasmi nchini jana alifajiri, Novemba 7, 2027, timu hiyo inatarajia kuondoka Dar es Salaam leo Jumapili kwenda visiwani Zanzibar, ili kuweka kambi fupi ya maandalizi ya michuano ijayo ya Ligi Kuu na Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.
Fadlu amependekeza timu hiyo kuweka kambi fupi visiwani, Zanzibar katika kipindi hiki cha kupisha Kalenda ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), ikiwa ni mkakati mzuri wa kutengeneza utulivu mkubwa na kuamsha morali ya wachezaji upya.
Hatua hiyo ya kuweka kambi visiwani Zanzibar kwa Yanga, ni kutokana na kuchagua kuutumia Uwanja wa New Amaan Complex, katika mechi zake za hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika msimu huu, itakayoanza mwishoni mwa Novemba.
Fadlu ana kibarua kigumu cha kuivusha Yanga kwenda hadi hatua ya Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, huku timu hiyo ya Yanga ikipangwa kundi B sawa na Zamalek SC ya Misri, MC Alger ya Algeria na Club Africain kutokea Tunisia.
MTIHANI UKO HAPA
Hata hivyo, kocha huyo atatakiwa kutengeneza mpango wake vizuri ili timu hiyo iweze kukaa sawa kwa kuwa anakabiliwa na michezo migumu hivi karibuni. Baada ya mechi za timu za Taifa za kufuzu AFCON 2027, ratiba inaonyesha kuwa Yanga itaanza kwa kuvaana na Polisi, Mbeya City kwenye Ligi Kuu, kisha itaingia kwenye mechi za hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya MC Alger na kurudi kwenye ligi kuvaana na Azam FC michezo ambayo inaweza kutoa muelekeo wa timu hiyo msimu huu.
AWEKA MALENGO
Akizungumza baada ya kutambulishwa kukifundisha kikosi hicho, Fadlu alisema amerudi akiwa na dhamira bora ya kuhakikisha Yanga inatetea mataji yote inayomiliki, huku akifurahia kurejea Tanzania chini ya uongozi wa Rais, Injinia Hersi Said.
“Tunataka kutengeneza mtindo wa uchezaji, falsafa ya soka, kufanya maboresho hatua kwa hatua, kuendeleza mafanikio yote yaliyopo na kuongeza nguvu kwenye dirisha la usajili ili kuifanya Yanga iwe imara na kubakia kileleni,” alisema Fadlu.
Aidha, Fadlu alisema uongozi wa timu hiyo chini ya Rais wa Yanga, Hersi Said walifanya mazungumzo naye kwa zaidi ya mara mbili huko nyuma, ingawa, baada ya kumfuata tena mara ya tatu, ameona ni ndio muda sahihi wa kukifundisha kikosi hicho.
Katika hatua nyingine, Fadlu alisema licha ya majeraha ya baadhi ya wachezaji wa timu hiyo, ila anaamini wana kikosi chenye ubora mzuri wa kushindana katika michuano mbalimbali msimu huu, kwa lengo la kutetea mataji yote waliyoyachukua.