Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mitindo hii haizeeki, vaa uonekane wa kisasa

Muktasari:

  • Huhitaji kununua nguo kila zinapotoka mpya wala kutumia fedha nyingi kufuata kila upepo wa fasheni. Unachohitaji ni kujua mitindo inayobaki na mvuto wake kila kizazi kinapobadilika.

Kuna watu kila kukicha wanakimbizana na mitindo mipya ya mavazi kiasi kwamba kabati lao linakuwa kama duka la nguo. Leo wanataka kuvaa hivi kwa sababu ndiyo fasheni, kesho wanabadilisha tena kwa sababu kuna mtindo mwingine umeibuka. Lakini ukweli ni kwamba, si kila kinachovuma ndicho kinachodumu. Kuna mitindo ambayo hata miaka ipite, bado ukivaa unaonekana umepangiliwa, umependeza na unaendana na wakati.

Huhitaji kununua nguo kila zinapotoka mpya wala kutumia fedha nyingi kufuata kila upepo wa fasheni. Unachohitaji ni kujua mitindo inayobaki na mvuto wake kila kizazi kinapobadilika.

1. SHATI JEUPE NA JEANS

Huu ni mchanganyiko ambao hauhitaji matangazo mengi. Shati jeupe likivaliwa na jeans ya bluu linakupa muonekano safi na wa kuvutia bila kujitahidi sana. Unaweza kulivaa ukiwa unaenda matembezini, kukutana na marafiki au hata shughuli zisizohitaji mavazi rasmi. Siri yake ni kuchagua jeans inayokutosha vizuri na shati lisilo na mikunjo mingi.

2. GAUNI JEUSI

Wanawake wanaopenda kuonekana maridadi bila kujisumbua lazima wawe na gauni jeusi kwenye kabati. Gauni hilo linafaa kwenye dinner, sherehe na matukio mbalimbali.

Unaweza kulivaa na viatu virefu, sandali au viatu vifupi kulingana na sehemu unayoenda. Uzuri wake ni kwamba halihitaji mapambo mengi ili kukupa muonekano wa kuvutia na unaingia nalo kokote.

3. SUTI YA KAWAIDA

Kwa wanaume, suti ni moja ya mavazi ambayo hayajapoteza nafasi yake. Suti ya rangi nyeusi, bluu iliyokolea au kijivu inaweza kuvaliwa kwenye shughuli rasmi, mikutano na hafla mbalimbali.

Kinachofanya suti ipendeze zaidi ni jinsi inavyokutosha mwilini. Suti iliyokaa vizuri inaweza kukupa muonekano wa kifahari hata bila kuwa na mapambo mengi na bado ukaonekana freshi.

4. BLAZER NA JEANS

Huu ni mtindo unaoweza kuvaliwa na wanaume na wanawake. Blazer (koti refu) inakupa muonekano wa heshima, wakati jeans inakupa uhuru wa kuvaa kawaida. Unaweza kuchanganya blazer nyeusi na jeans ya bluu pamoja na viatu safi kama ni raba.

Ni muonekano unaofaa kwa matembezi ya wikendi, kwenye sherehe, kazini na kila maeneo maalum na watu washikushangae kabisa.

5. TRENCH COAT

Koti flani hivi refu mpaka kwenye magoti anaweza kuvaa mwanaume na mwanamke, mara nyingi utaona mtu kavaa kwenye maeneo ya baridi au matukio na bado ukanoga, kwani ni ishu ni muonekano tu wa hilo koti.

Nguo hii imeendelea kuwa na nafasi yake katika ulimwengu wa mitindo. Trench coat ya rangi ya kahawia nyepesi, beige au nyeusi inaweza kuvaliwa juu ya gauni, jeans au suruali ya kitambaa. Linaongeza mvuto na kufanya hata mavazi rahisi yaonekane yamepangwa vizuri. Kwa wanaopenda muonekano wa kisasa wa kitajiri hili ni chaguo zuri.


6. POLO SHIRT NA SURAUALI YA KITAMBAA

Wanaume wanaweza kuonekana nadhifu bila kulazimika kuvaa suti au mashati rasmi kila wanapotoka. Polo shirt (Form six) ikichanganywa na suruali ya kitambaa inatoa muonekano wa kawaida lakini wenye heshima.

Unaweza kuchagua rangi nyeupe, bluu au nyeusi na kuunganisha na viatu vya aina yoyote. Huu ni mtindo mzuri kwa matembezi ya wikendi, kazini siku ambazo huna mambo mengi ya vikao vya heshima.

7. NGUO ZENYE MISTARI

Nguo zenye mistari, hasa nyeusi na nyeupe, zimeendelea kupendwa kwa miaka mingi. Unaweza kuvaa shati, blauzi au gauni lenye mistari na kulichanganya na suruali au sketi isiyo na michoro mingi. Uzuri wa mtindo huu ni kwamba hauhitaji rangi nyingi wala mapambo mengi ili kuvutia.

8. RABA NYEUPE

Raba nyeupe ni viatu vinavyoweza kuokoa mavazi mengi. Unaweza kuvivaa na jeans, pensi, kaptula au hata gauni la kawaida. Vinatoa muonekano wa ujana, usafi na muunganiko mzuri wa muonekano. Jambo la msingi ni kuhakikisha vinakuwa safi kwa sababu uchafu unaweza kuharibu muonekano mzima.

9. SKETI YA PENSELI

Kwa wanawake wanaopenda mavazi yanayowapa muonekano wa nadhifu, sketi ya penseli ni chaguo lisilopoteza mvuto. Inaweza kuvaliwa na blauzi, shati au sweta nyepesi. Inafaa kwa shughuli za kikazi, matembezi na hata baadhi ya hafla. Unaweza kubadilisha viatu na mapambo ili kupata muonekano tofauti.

10. JAKETI LA NGOZI

Jaketi la ngozi lina mvuto wake wa kipekee. Likivaliwa na t-shirt nyeupe na jeans linatoa muonekano wa kisasa usiohitaji vitu vingi. Unaweza kulivaa ukiwa unaenda matembezini au kukutana na marafiki. Rangi nyeusi na kahawia ni chaguo zinazoweza kuendana na mavazi mengi.