Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Nje ya hesabu za uchumi, Waziri Omar ni shabiki wa Arsenal

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Muktasari:

  • Ni miongoni mwa mashabiki wa soka wanaofuatilia kwa karibu Ligi Kuu ya England, akiwa na mapenzi ya kipekee kwa klabu ya Arsenal, huku Barcelona ya Hispania nayo ikiwa na sehemu yake moyoni mwake.

WAKATI wengi wanamfahamu Balozi Khamis Mussa Omar kupitia nafasi yake ya Waziri wa Fedha, inayomweka katikati ya mijadala kuhusu uchumi, bajeti na sera za kifedha, nje ya ofisi ana upande mwingine unaomhusisha na michezo na burudani.

Ni miongoni mwa mashabiki wa soka wanaofuatilia kwa karibu Ligi Kuu ya England, akiwa na mapenzi ya kipekee kwa klabu ya Arsenal, huku Barcelona ya Hispania nayo ikiwa na sehemu yake moyoni mwake.

Mapenzi yake kwa Arsenal hayaishii katika kuitaja tu timu hiyo, bali yanaambatana na utetezi wa mafanikio yake na hata historia ya klabu hiyo, hasa inapokuja suala la kusubiri kwa muda mrefu kurejea kileleni mwa soka la England.

Akizungumzia timu hiyo, Balozi Omar anajivunia mafanikio yake na anaamini ina uwezo wa kuendelea kutawala soka la England kwa misimu ijayo.

“Timu yangu kule Uingereza ni mabingwa watetezi na mabingwa watarajiwa katika msimu huu unaoendelea. Kwa miaka hii michache tutaendelea kuchukua,” anasema kwa kujiamini.

Anasema kurejea kwa Arsenal katika kilele cha Ligi Kuu ya England baada ya kusubiri kwa miaka 22 hakukuwa jambo la kushangaza, akieleza kuwa kipindi hicho ni kifupi ukilinganisha na muda ambao baadhi ya klabu nyingine kubwa zilisubiri kabla ya kurejesha ubingwa.

“Tulijifunza kutoka kwa Liverpool ambao walisubiri miaka 26 kulipata tena. Tukajifunza kutoka kwa Manchester United ambao walisubiri miaka 24 kabla ya kulipata. Hivyo, Arsenal miaka 22 ndiyo miaka michache zaidi kuliko klabu zote kubwa,” anasema.

Kwa mujibu wake, licha ya kupitia vipindi vigumu na kukosa ubingwa kwa muda mrefu, Arsenal haijawahi kupoteza hadhi ya kuwa miongoni mwa timu bora.

Anasema hata watu wasiokuwa mashabiki wa klabu hiyo wanatambua ubora wake, akifananisha changamoto ilizopitia na hali inayokikabili sasa Manchester United.

“Ilipitia vipindi vigumu kama ambavyo wenzetu wa Old Trafford wanapitia,” anasema.

Hata hivyo, anapozungumzia hali ya Manchester United kwa sasa, hawezi kuficha utani wake kwa wapinzani hao wa muda mrefu.

“Sasa hivi ukiwaangalia wazee wa Old Trafford mpaka unawahurumia, lakini ndiyo msimu, wastahili hivyohivyo. Wanaweza kujifariji na nyimbo ya Diamond iitwayo Yatapita,” anasema huku akicheka.


HANA TIMU TANZANIA

Tofauti na mapenzi yake kwa Arsenal, Balozi Omar anasema hana timu maalumu anayoishabikia katika soka la Tanzania, licha ya kufuatilia ligi na timu mbalimbali nchini.

Anasema watu wengi huwa na wakati mgumu kuamini kauli hiyo kwa sababu wamezoea mashabiki kujitambulisha kuwa ni wa Simba au Yanga.

“Watu hawaamini maana wengi wanapenda uwe ama Simba au Yanga, lakini mimi naangalia zote, hata Azam. Kuna wakati wote wananialika kwenye mechi zao,” anasema.

Anasema amekuwa akikubali mialiko ya timu hizo na kuhudhuria michezo yao bila kujifunga na upande wowote.

Anakumbuka mchezo mmoja wa Simba na Yanga uliochezwa katika Uwanja wa Amaan, ambapo mashabiki walikuwa na hamu ya kujua angeegemea upande gani.

“Wote wakinialika huwa naenda. Sasa kuna siku Simba na Yanga wakacheza Amaan, nikaenda. Wakajua siku hiyo watajua niko timu gani, wakasema watajua. Simba akapata goli sikuinuka wasije wakasema mimi Simba, lakini kutoinuka wakasema mimi Yanga. Kwa kweli sina timu mimi,” anasema.


ANAVYOIONA SOKA TANZANIA

Akizungumzia maendeleo ya soka nchini, Balozi Omar anasema mchezo huo umepiga hatua kubwa katika miaka ya hivi karibuni, ingawa bado kuna safari ndefu kufikia viwango vya mataifa yanayotamba kwa soka barani Afrika, hususan Afrika Magharibi.

Anasisitiza kuwa maendeleo ya soka hayawezi kutegemea vipaji pekee, bali yanahitaji uwekezaji wa muda mrefu unaoanzia katika umri mdogo.

Anatoa mfano wa mifumo ya akademi katika klabu kubwa za Ulaya, akitaja Arsenal na namna inavyokuza vipaji vya watoto tangu wadogo.

“Mpira siyo kitu kinachokuja kwa sababu tu mnataka au mnavipaji vya kucheza chandimu, bali ni uwekezaji. Wenzetu wanawekeza watoto wakiwa wadogo sana. Hata ukiangalia Arsenal, huyu mtoto wa sasa hivi, Dowman, kipaji chake kimeibuliwa tangu miaka minne, miaka saba yupo akademi. Professional kweli kweli,” anasema.

Kwa mtazamo wake, mafanikio ya wachezaji wengi wakubwa duniani yanatokana na malezi bora ya kisoka waliyoyapata wakiwa katika umri mdogo, jambo linaloonyesha umuhimu wa kuimarisha mifumo ya kukuza vipaji nchini.

Anasema hatua zinazochukuliwa na wadau wa soka zinatia matumaini, akitaja ziara yake ya hivi karibuni katika akademi moja mkoani Tanga na juhudi zinazofanywa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

“Hivi karibuni nilitembelea akademi ya Tanga. TFF wanafanya kazi nzuri kuimarisha mpira wa miguu. Nafikiri tunahitaji tu kupata wawekezaji zaidi, maana hiyo nayo inakuwa biashara,” anasema.

Anasisitiza kuwa pamoja na kazi nzuri inayofanywa na akademi hizo, ni muhimu kuongeza uwekezaji katika miundombinu, walimu na walezi wa vipaji ili kujenga msingi imara wa soka la ushindani.

Anasema michezo inahitaji uvumilivu na mwendelezo kama ilivyo katika sekta ya elimu, hivyo juhudi zinazowekwa sasa hazipaswi kukatizwa kabla ya kufikia matokeo yanayotarajiwa.


ALIVYOKUWA BINGWA WA MICHEZO

Mbali na kuwa shabiki wa soka, Balozi Omar anasema aliwahi kushiriki michezo mbalimbali na kufikia kiwango cha ubingwa katika mchezo wa mpira wa wavu (volleyball) na tenisi ya mezani (table tennis).

Anasema bado anaamini anaweza kucheza michezo hiyo, ingawa kuna baadhi ya mbinu ambazo hana uhakika kama anaweza kuzitekeleza kama zamani.

Akizungumzia mchezo wa tenisi ya mezani, anasema anaweza kuendelea kucheza, lakini anatia shaka uwezo wake wa kupiga ‘smash’, akitania kuwa huenda akajikuta wodini (hospitali) siku inayofuata.


MAPENZI YAKE KWA MUZIKI

Kutoka katika michezo, upande mwingine wa maisha ya Omar ni muziki, ambao anasema amekuwa akiufuatilia katika mitindo na vizazi mbalimbali.

Anasema anasikiliza muziki wa taarab wa zamani na wa kisasa, muziki wa dansi pamoja na nyimbo za kizazi cha sasa.

Katika muziki wa dansi, anawafuatilia wasanii kama Mbaraka Mwinshehe na Muhidin Ngurumo, huku pia akitaja wasanii wengine wa zamani kama Dede.

Kwa upande wa muziki wa kizazi kipya, anasema anafuatilia kazi za Diamond Platnumz, Harmonize, Mbosso, Marioo, Nandy na Zuchu. Hata hivyo, anapoulizwa msanii anayemkubali zaidi, jina la Nandy ndilo analolitaja bila kusita.

“Nikipata muda huwa nasikiliza wote, ila mmoja wao ninayemkubali sana, siyo siri, ni Nandy,” anasema.

Anasema mara nyingi husikiliza muziki akiwa safarini ndani ya gari, lakini wakati mwingine hutumia muda wake wa mapumziko nyumbani kufuatilia kazi za wasanii kupitia YouTube.

Anataja kuwa pamoja na wasanii aliowataja, pia hufuatilia kazi za Harmonize na Mbosso kupitia mtandao huo..