Jude, Jobe kuvunja rekodi England
Muktasari:
- Jobe amepata nafasi hiyo baada ya kuonyesha kiwango kizuri nchini Ujerumani, kufuatia mwanzo mgumu wa maisha yake Dortmund baada ya kujiunga na klabu hiyo akitokea Sunderland mwaka 2025 kwa ada ya uhamisho ya pauni milioni 28.
LONDON, ENGLAND: NDUGU Jude na Jobe Bellingham wanaweza kuwa ndugu wa kwanza kucheza pamoja katika timu ya taifa ya England baada ya takribani miaka 20, kufuatia kocha Thomas Tuchel kumjumuisha Jobe katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo.
Kiungo huyo wa Borussia Dortmund mwenye umri wa miaka 21 ameitwa pamoja na kaka yake Jude, 23, anayeichezea Real Madrid, kwa ajili ya mechi za Ligi ya Mataifa dhidi ya Croatia na Hispania.
Jobe amepata nafasi hiyo baada ya kuonyesha kiwango kizuri nchini Ujerumani, kufuatia mwanzo mgumu wa maisha yake Dortmund baada ya kujiunga na klabu hiyo akitokea Sunderland mwaka 2025 kwa ada ya uhamisho ya pauni milioni 28.
Msimu huu ameanza mechi sita kati ya nane za Dortmund katika Ligi Kuu ya Ujerumani 'Bundesliga', akitoa pasi mbili za mabao. Pia alifunga bao dhidi ya Bayern Munich mwishoni mwa wiki iliyopita, lakini bao lake likakataliwa.
Kwa upande wake, Jude tayari ni miongoni mwa wachezaji muhimu wa England. Amecheza mechi 60 za timu hiyo ya taifa na kufunga mabao 14 tangu alipoanza kuitumikia mwaka 2020 akiwa na umri wa miaka 17.
Sasa wawili hao wana nafasi ya kufuata nyayo za baadhi ya ndugu maarufu waliowahi kuitumikia England.
Ndugu wa mwisho kucheza pamoja uwanjani katika timu hiyo walikuwa Gary na Phil Neville, walioonekana wote katika mchezo wa kirafiki ambao England ilifungwa bao 1-0 na Hispania kwenye Uwanja wa Old Trafford, Februari 2007, zaidi ya miaka 19 iliyopita.
Gary alianza kuitumikia England mwaka 1995 chini ya kocha Terry Venables, kabla ya mdogo wake Phil kujiunga na kikosi hicho mwaka uliofuata.
Wote walikuwa wameibukia katika akademi ya Manchester United, kizazi maarufu kilichofahamika kama Class of '92.
Gary alicheza mechi 85 za England, akijijengea nafasi ya kudumu katika nafasi ya beki wa kulia na kuiwakilisha timu hiyo katika fainali tatu za Euro na mbili za Kombe la Dunia.
Phil, kwa upande wake, alicheza mechi 59 na alikuwa na uwezo wa kucheza nafasi za ulinzi au kiungo.
Hata hivyo, ndugu wa Neville si wa mwisho kuwa na wachezaji wawili katika familia moja waliowahi kuitumikia England. Nathaniel na Trevoh Chalobah nao waliingia katika orodha hiyo mwaka jana baada ya Tuchel kumpa Trevoh nafasi ya kucheza mechi yake ya kwanza dhidi ya Senegal, Juni 2025.
Kaka yake Nathaniel alikuwa amecheza mechi yake pekee ya England karibu miaka saba kabla, alipoingia kama mchezaji wa akiba katika ushindi maarufu wa mabao 3-2 dhidi ya Hispania mjini Seville, Oktoba 2018.
Miongoni mwa ndugu maarufu zaidi kuwahi kuichezea England ni Sir Bobby na Jack Charlton, ambao waliandika historia ya kipekee kwa kutwaa Kombe la Dunia pamoja mwaka 1966.
Bobby alianza kuitumikia England mwaka 1958 na baadaye kuwa miongoni mwa wachezaji bora zaidi katika historia ya nchi hiyo. Alicheza mechi 106 na kufunga mabao 49.
Sasa Jude na Jobe wanatarajia kuandika ukurasa wao katika historia ya familia za wachezaji wa England, ingawa si ndugu pekee maarufu waliowahi kuiwakilisha nchi hiyo.
Wachezaji wa Chelsea, Reece na Lauren James, pia wamecheza katika timu za taifa za England. Lauren alianza kuitumikia timu ya wanawake ya England, Lionesses, Septemba 2022, na kuwa ndugu wa kwanza wa jinsia tofauti kufanikisha hilo katika zama za sasa.
Ndugu waliowahi kuitumikia England
Charlie (1872) na William Clegg (1873–1879)
William (1875–1877) na Herbert Rawson (1875)
Hubert (1873–1878) na Frank Heron (1876)
Alfred (1877) na Ed Lyttelton (1878)
Ernest (1876), Charlie (1879–1887) na Arthur Bambridge (1881)
Arthur (1876–1883) na Harry Cursham (1880–1884)
Fred (1880–1882) na Jack Hargreaves (1881)
Arthur (1885–1890) na Percy Walters (1885–1890)
Alf (1882–1884) na Charley Dobson (1886)
Charlie (1888) na Alf Shelton (1889–1892)
Robert (1893–1894) na Arthur Topham (1894)
Charlie (1890–1893) na Tom Perry (1898)
Frank (1898–1903) na Fred Forman (1899)
Charles (1889) na Geoffrey Wilson (1900)
Bertie (1901) na Rex Corbett (1903)
Frank (1922–1926) na Reg Osbourne (1927)
Clem (1924) na George Stephenson (1928–1931)
Jack (1931) na Sep Smith (1935)
Bobby (1958–1970) na Jack Charlton (1965–1970)
Gary (1995–2007) na Phil Neville (1996–2007)
Nathaniel (2018) na Trevoh Chalobah (2025)
Jude (2020–) na Jobe Bellingham (2026–)