Jose Mourinho atajwa Newcastle United
Muktasari:
- Kwa mujibu wa tovuti ya talkSPORT, wamiliki wa Newcastle ambao ni matajiri kutoka Saudi Arabia wanataka kumteua kocha mwenye hadhi ya kimataifa kuiongoza klabu hiyo.
NEWCASTLE, ENGLAND: KOCHA wa Benfica, Jose Mourinho anaweza kurejea katika Ligi Kuu England baada ya uongozi wa Newcastle United kudaiwa unafikiria kumwajiri kuelekea msimu ujao.
Mourinho ambaye amewahi kuzifundisha Tottenham, Chelsea na Manchester United anaripotiwa kuwa miongoni mwa makocha wanaoweza kuajiriwa na klabu hiyo ikiwa Eddie Howe ataondoka.
Kwa mujibu wa tovuti ya talkSPORT, wamiliki wa Newcastle ambao ni matajiri kutoka Saudi Arabia wanataka kumteua kocha mwenye hadhi ya kimataifa kuiongoza klabu hiyo.
Ingawa Howe bado anaungwa mkono na bodi, presha kutoka kwa mashabiki imeongezeka kutokana na matokeo mabaya ya hivi karibuni hali inayosababisha yeye mwenywe kufikiria kutaka kuondoka bila hata ya kufukuzwa.
Newcastle inajiandaa kwa mabadiliko makubwa dirisha la majira ya kiangazi bila kujali nani atakuwa kocha.
Wachezaji nyota kama Sandro Tonali na Tino Livramento wanahusishwa na kuondoka, huku Anthony Gordon naye akiwindwa na klabu kubwa kama Bayern Munich na Arsenal.
Kwa sasa Mourinho anainoa Benfica, na hajawahi kuficha mapenzi yake na Newcastle, hasa kutokana na uhusiano wake wa karibu na gwiji wa timu hiyo Sir Bobby Robson aliyekutana naye wakati ni sehemu ya benchi la ufundi la Barcelona.
ikiwa Mourinho ataenda Newcastle, itakuwa ni ajira yake ya 12 katika maisha yake ya ukocha, akiwa na historia kubwa ndani ya Ligi Kuu England.
Alianza mafanikio yake na Chelsea, akitwaa mataji mawili mfululizo ya ligi katika misimu yake miwili ya kwanza, kabla ya kurejea baadaye na kushinda taji la tatu. Kisha alifundisha Manchester United kuanzia 2016 hadi 2018, akiiongoza kushinda UEFA Europa League na EFL Cup katika msimu wake wa kwanza, pamoja na kumaliza nafasi ya pili msimu uliofuata kabla ya kuondoka katikati ya msimu wake wa tatu.
Hata hivyo, licha ya mafanikio yake makubwa, bado kuna mashaka kama Mourinho ndiye chaguo sahihi kwa kwa timu hiyo huku baadhi ya wachambuzi wakidaiwa mbinu zake zimepitwa na wakati.