Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mo Salah hatatembea peke yake tutamlinda

SALAH Pict


“MO Salah! Mo Salah! Mo Salah! Running down the wing.


“Mo Salah la-la-la la-ahh, The Egyptian King!”. Ukurasa umefungwa. Mambo hufika mwisho. Mambo yamefika mwisho Anfield. Ilikuwa hadithi tamu na ya kusisimua ya mapenzi ambayo mwandishi hatimaye ameandika mstari wa mwisho katika kitabu.


Katikati ya wiki Salah amekaa mahala katika kona ya nyumba yake akajirekodi na kutangaza kwamba anebakisha wiki kadhaa tu kuwa mchezaji wa Liverpool. Kwamba anaondoka zake. Baada ya miaka tisa ya kusisimua Anfield ameamua kuondoka zake. Ni wazi kwamba watu hawajashangazwa na uamuzi wake. Miguu yake imemsaliti. Umri pia umemsaliti.


Binafsi naamini kwamba amechelewa. Niliamini kwamba yeye na Kevin De Bruyne wangeondoka pamoja katika Ligi Kuu England. Hata hivyo, yeye aliamua kubaki. Juni, mwaka huu atatimiza miaka 34. Tangu alipotimiza miaka 32 tayari miguu ilikuwa imeanza kumsaliti Salah. Akili ilikuwa inataka, lakini mwili uligoma. Mambo hufika mwisho.

Niliamini tangu miaka miwili iliyopita Salah alipaswa kwenda Riyadh kuungana na Cristiano Ronaldo kuchukua pesa za Waaarabu wenzake. Alipaswa kuua mapema ule utatu mtakatifu wa yeye, Roberto Firmino na Sadio Mane. Wenzake waliondoka mapema, lakini Salah aliamua kubaki. Mshahara wake ulienda juu maradufu, lakini wiki baada ya wiki miguu yake imeendelea kumsaliti.

Anaondoka akiwa ameacha alama. Amenifurahisha kwa mambo mengi lakini nitamkumbuka kwa kitu kinachoitwa ‘comeback’ ya maisha yake ya soka. Namna alivyoondoka zake Stamford Bridge akiwa mchezaji wa kawaida tu ambaye hakuacha alama. Akaenda zake Roma. Pale Chelsea alionekana kama vile alisajiliwa kwa bahati mbaya kutoka Basel. Hakutumika. Alikutana na vigingi vingi.

PAZ 01

Mkopo wa Fiorentina kisha uhamisho wa moja kwa moja kwenda Roma vikamfanya atuonyeshe sura halisi ya ubongo wake. Hatimaye akarudi Ligi Kuu England na kuanza kazi mbili. Kazi yake ya kwanza ilikuwa kumtia lawama Jose Mourinho na kumfanya alazimike mara nyingi kujibu swali la waandishi wa habari la kwanini Salah hakuwika Chelsea. Swali ambalo pia Mourinho alikuwa anakumbana nalo kuhusu De Bruyne.

Lakini hapo hapo Salah alikuja Anfield na kuwachanganya akili mashabiki wa Anfield. Kwanza kabisa ni namna ambavyo alijichomeka katikati ya historia ya mastaa wakubwa wa Anfield. Akafanikiwa kujichomeka kuwa lejendi wa Anfield huku akisimama juu ya wengine ambao zamani walikuwa wanaonekana kama vile miungu watu pale Anfield.

Zamani pale Anfield kulikuwa na kina Ian Rush, Kenney Dalglish, Robbie Fowler ambaye vichaa wa Anfield walikuwa wanakufuru kwa kumuita ‘mungu’ na wengineo wengi. Salah aliwasili klabuni kama mchezaji aliyefeli Chelsea na ghafla akageuza kibao cha kuwa mmoja kati ya wachezaji bora zaidi kuwahi kucheza Liverpool. Kama utaamua kufuata namba kuliko hali halisi basi Salah anaweza kuwa mchezaji bora zaidi kuwahi kutokea Liverpool.

PAZ 02

Ghafla Salah akawa mchezaji aliyeifungia Liverpool mabao mengi zaidi katika historia ya Ligi Kuu England. Alifanya hivyo huku akiwa ameifungia zaidi ya mabao 200 katika michuano mbalimbali. Kuna wachezaji ambao wanaheshimika mno Anfield, lakini Salah amewaacha mbali katika hili. Anazua utata ukimlinganisha na wengineo.

Ghafla kuna msimu ambao Salah aliweka rekodi ya kuhusika katika mabao mengi zaidi ndani ya msimu mmoja. Katika mechi 38 za Ligi Kuu alihusika katika mabao 47 kwa maana kadhaa alifunga na kadhaa alitoa pasi za mwisho. Hakuna mchezaji ndani au nje ya Liverpool ambaye amewahi kufanya hivyo. Tunazungumzia hadi kina Thierry Henry na Didier Drogba ambao pia waliacha alama katika ligi hiyo.

Ghafla akawa mchezaji aliyehusika katika mabao mengi kwenye historia ya Ligi Kuu England akiwa ndani ya timu moja tu Liverpool. Labda wengine wamehusika zaidi lakini walicheza katika timu nyingi. Salah akiwa na Liverpool pekee amehusika na mabao 281 katika Ligi Kuu ya England. Hakuna mchezaji wa Liverpool au timu nyingine ambaye amewahi kufanya hivyo.

PAZ 03

Mo Salah ni mchezaji wa kwanza kwenda zake Old Trafford akaondoka na mpira. Kwa maana ya kwamba anakuwa mchezaji wa kwanza wa Liverpool kwenda Manchester na akafunga hat trick. Unafahamu upinzani wa hawa mabwana. Ni wapinzani haswa. Kina Ian Rush hawakuweza kufanya hivyo hapo nyuma.

Lakini wakati mashabiki wa Liverpool wakimhusudu Robbie Fowler kiasi cha kumuita mungu kutokana na kumtegemea kwa kufunga mabao, Salah amekwenda zake Anfield na kuwa mfungaji bora wa tatu wa muda wote nyuma ya Rush na Roger Hunt. Sio kitu kidogo sana. Kama angebaki kidogo tu angeweza kuwa mfungaji bora wa muda wote na kuacha watu midomo wazi zaidi.

Wakati Liverpool ikitamba zaidi katika michuano ya Ulaya huku mashabiki wake wakijisifu zaidi kwa hilo, hakuna mchezaji yeyote wa Liverpool aliyefunga mabao mengi zaidi katika michuano ya Ulaya zaidi ya Salah. Amefunga mabao 53, lakini katika hayo mabao 48 amefunga katika michuano ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya. Kumbuka namna ambavyo hata kabla ya ujio wa Salah Liverpool walivyokuwa wametamba Ulaya. Kumbe bado hakuna ambaye alifikia mabao ya Salah.

PAZ 03 (1)

Mwarabu anaondoka Anfield akiwa ameacha alama nyingi. Haikutegemewa. Ameacha vurugu za rekodi ambazo wengine watapambana haswa kuzifikia. Haikutegemewa kwamba kuna Mwarabu atatoka zake Misri na kwenda kuvuruga hali ya hewa Anfield. Na sasa ukiuliza nani zaidi kati ya Fowler na Salah unaweza kupata jibu la Salah ni zaidi ya Fowler. Namba hazidanganyi lakini hata hali halisi haidanganyi.

Na katika dunia ya jumla, Salah anakuwa mmoja kati ya wachezaji wachache ambao walikuwa wanashika nafasi ya tatu nyuma ya Ronaldo na Lionel Messi. Ndio, kuna mchezaji mwingine anasimama mbele ya Salah zaidi ya hawa wawili? Hapana. Kina Kylian Mbappe wanajipeleka huko lakini sidhani hata kama Neymar anasimama juu ya Salah linapokuja jambo hilo.

Na kitu kikubwa ambacho kitambeba Salah ni mwendelezo wa ubora wake kabla miguu haijamsaliti. Kwa misimu sita mfululizo Salah alikuwa anafunga mabao 10 zaidi ya ligi na pasi 10 za kusaidia wenzake. Naposema mabao 10 namaanisha na zaidi kiasi kwamba karibu kila msimu wa ubora wake Salah alikuwa anafunga mabao 20 na zaidi.

PAZ 05

Kwa ujumla wake pia Salah alikuwa amefuata nyayo za Lionel Messi linapokuja suala la winga kufunga mabao mengi. Mpira wa kisasa ndivyo ulivyo. Salah amefanya yote hayo akiwa kama winga wa kulia anayetumia mguu wa kushoto. Zamani yote hayo yalikuwa yanafanywa na washambuliaji wa katikati. Siku hizi imekuwa fasheni lakini sio kila mmoja anaweza kufanya hilo kwa usahihi zaidi.

Pale Liverpool wana usemi mmoja. You will never walk alone. Kwamba hautatembea peke yako. Kwamba ukiwa unahusika na Klabu ya Liverpool hautatembea peke yako. Mtakuwa wengi. Ni kweli. Lakini hata sisi wengine ambao sio mashabiki wa Liverpool tutamlinda Salah na hatatembea peke yake kama baadaye kuna watu watajaribu kuyumbisha ufalme wake wa Anfield siku za mbele. Tutamlinda na kukumbusha alama zake alizoacha Anfield.

Sio kwamba Wazungu wanapenda sana rekodi za wachezaji kutoka Afrika. Baadaye wanaweza kuanza kuyumbisha historia na mengineyo. Ikifikia hapo tutamlinda. Na tutasema kuwa anaweza kuwa miongoni mwa wachezaji wawili au watatu bora kuwahi kutokea katika historia ya Luverpool.