Ndo hivyo! Baada Buffon, Gravina ni zamu ya Gattuso
Muktasari:
- Kutokana na kushindwa huko kwa mara nyingine, zimewafanya viongozi hao kujiuzulu nafasi zao za rais na ukuu wa uwasilishaji wa taarifa.
MILAN, ITALIA: HAKUNA namna. Baada ya kipigo kilichoiondoa Italia kwenye kufuzu fainali za Kombe la Dunia 2026, baadhi ya viongozi wa timu ya taifa wameanza kujichomoa kwenye timu hiyo wakiwamo Rais wa shirikisho la soka la Italia (FIGC) Gabriele Gravina na kipa mkongwe Gianluigi Buffon, sasa ni zamu ya Kocha Gennaro Gattuso.
Inaelezwa Gattuso anatarajiwa kujiuzulu katika nafasi yake kama kocha mkuu wa timu hiyo baada ya viongozi hao wawili muhimu wa shirikisho lao la soka kutokana na kushindwa kufuzu kwenye fainali hizo kwa mara ya tatu mfululizo.
Italia ilichapwa kwa penalti 4-1 na Bosnia na Herzegovina katika mechi ya mchujo Jumanne usiku kulifanya taifa hilo, mabingwa wa Kombe la Dunia mara nne, kuwa la kwanza lililowahi kushinda taji hilo kushindwa kufuzu kwa mashindano matatu mfululizo, baada ya kukosa michuano ambayo ilifanyika Russia 2018 na Qatar 2022.
Kutokana na kushindwa huko kwa mara nyingine, zimewafanya viongozi hao kujiuzulu nafasi zao za rais na ukuu wa uwasilishaji wa taarifa.
Gravina alikuwa amemwomba Gattuso aendelee kubaki kama kocha saa chache kabla ya yeye mwenyewe kujiuzulu katika mkutano wa dharura uliofanyika makao makuu ya FIGC mjini Rome.
Ripoti kutoka Italia zinaeleza Gattuso atachukua siku chache kutafakari mustakabali wake lakini inatarajiwa ataondoka pia. Kuna uwezekano pia akaendelea kuinoa timu katika mechi za kirafiki za mwezi Juni wakati wakisubiri kocha mpya.
Kwa mujibu wa gazeti la Corriere dello Sport, makocha wawili wanaoongoza kwa nafasi ya kumrithi ni Roberto Mancini na Antonio Conte.
Mancini aliwahi kuinoa Italia baada ya kushindwa kufuzu Kombe la Dunia la 2018 chini ya Gian Piero Ventura.
Aliiongoza Italia kushinda michuano ya Euro 2020 kwa rekodi ya mechi 37 bila kufungwa. Hata hivyo, alikuwepo pia wakati Italia iliposhindwa kufuzu Kombe la Dunia la Qatar 2022 baada ya kufungwa na Macedonia.
Mancini alijiuzulu ghafla kabla ya kampeni ya kufuzu Euro 2024 na baadaye akaifundisha timu ya taifa ya Saudi Arabia. Kwa sasa anaifundisha klabu ya Al-Sadd ya Qatar.
Kwa upande wa Conte, aliifundisha Italia kati ya 2014 hadi 2016 kabla ya kujiunga na Chelsea FC. Aliifikisha Italia robo fainali ya Euro 2016, akiifunga Hispania kabla ya kutolewa na Ujerumani. Kwa sasa Conte ana mkataba na mabingwa wa Italia, SSC Napoli.
Majina mengine yaliyotajwa ni Massimiliano Allegri wa AC Milan na Jose Mourinho wa Benfica. FIGC imetangaza uchaguzi wa rais mpya utafanyika Juni 22 baada ya kujiuzulu kwa Gravina.
Buffon alithibitisha kujiuzulu kwake mara moja, akisema ilikuwa “Hatua ya kuwajibika.” Aliandika kwenye Instagram alihisi maumivu makubwa baada ya kushindwa kufuzu Kombe la Dunia na kuona ni sahihi kuachia nafasi yake.
Miongoni mwa wachezaji waliokosolewa zaidi ni Alessandro Bastoni wa Inter Milan, hasa baada ya kupata kadi nyekundu wakati timu yao ilikuwa inaongoza 1-0.
Mchezaji wa zamani Beppe Bergomi, ambaye alishinda Kombe la Dunia la 1982 na Italia, alionya Bastoni huenda atalazimika kuondoka nchini kwa usalama wake kutokana na ukosoaji mkubwa.