John Terry aiondoa Chelsea kwenye mbio za ubingwa England
Muktasari:
- Terry ametoa maoni hayo kufuatia kikosi cha Chelsea kupoteza mechi dhidi ya Sunderland kwa kufungwa mabao 2-1, baada ya ushindi wao dhidi ya Liverpool na Nottingham Forest.
Nguli wa Chelsea, John Terry anaamini ukosefu wa uzoefu ndani ya kikosi cha sasa cha klabu hiyo huenda ikawa kikwazo kwa The Blues kuwa sehemu ya timu zitakazowania ubingwa wa Ligi ya EPL msimu huu 2025-2026.
Terry ametoa maoni hayo kufuatia kikosi cha Chelsea kupoteza mechi dhidi ya Sunderland kwa kufungwa mabao 2-1, baada ya ushindi wao dhidi ya Liverpool na Nottingham Forest.
Kupitia mtandao wa X zamani Twitter, Terry ametoa maoni yake, akiamini Chelsea ina nafasi ngumu ya kuingia kwenye kinyang’anyiro cha ubingwa mwishoni mwa msimu huu, kwa kuamini bado wachezaji walio kikosini kwa sasa hawajakomaa kwenye ushindani wa ligi kubwa kama EPL.
Amesema kupoteza mechi muhimu dhidi ya Sunderland, ni ishara mbaya kwa klabu hiyo ambayo amekiri bado anaipenda na kuifuatilia kila inapokuwa uwanjani.
“Kupoteza dhidi ya Sunderland baada ya kufanya kazi kubwa na kuifunga Liverpool na Forest… nadhani tutaona mambo kama haya kuendelea kutokea kutokana na ukosefu wa uzoefu kwenye kikosi chetu.
“Tuna kundi la wachezaji vijana, hivyo tutashuhudia hali kama hii ikiendelea mara kwa mara, ni dhahiri tunapaswa kujipa muda, tunatakiwa kuamini kikosi chetu kinaandaliwa kwa ajili ya kesho na sio leo, siamini kama msimu huu kuna jambo tutakalolivuna kwa kweli,” amesema Terry.
Timu hiyo ya London Magharibi iliikaribisha Sunderland kwenye Uwanja wa Stamford Bridge jana Jumamosi, Oktoba 25, 2025. Chelsea iliingia kwenye mechi hiyo ikiwa na rekodi nzuri ya ushindi mara nne mfululizo katika michuano yote.
Alejandro Garnacho aliifungia Chelsea bao la kuongoza dakika ya nne, lakini Wilson Isidor alisawazisha dakika ya 22. Chemsdine Talbi aliipatia Sunderland bao la ushindi katika dakika za nyongeza.
Naye mchambuzi wa soka nchini Engalnd, Paul Merson amekosoa kiwango cha Chelsea, akimtaja Joao Pedro ambaye amekiri hakucheza kwenye kiwango chake kilichozoeleka.
Merson amesema: “Walionyesha wameshapambana hadi mwisho kisha wakajisahau kabisa… Joao Pedro alionekana kupotea kama namba 10. Kwa hakika sijaona walichokifanya Chelsea, zaidi ya kuonyesha dharau dhidi ya wapinzani ambao walionyesha juhudi na kuwashinda kirahisi.”
Kwa upande wa mchezaji wa zamani wa Chelsea Jason Cundy, ambaye naye ni mchambuzi kwa sasa, amesema: “Nimekasirika sana… Tulikuwa kama takataka.”
Wakati huohuo, beki wa kati wa Chelsea, Trevoh Chalobah alizungumza akiwa ndani ya chumba cha kubadilishia nguo baada ya mechi akieleza hisia za wachezaji wenzake, kwa kusema kulikuwa na hali ya simanzi miongoni mwao, kutokana na kilichotokea baada ya kupoteza dhidi ya Sunderland.
Chalobah amesema: “Ilikuwa mechi ngumu, walikuja kuvuruga mpango wetu wa mechi… Tulipata nafasi chache, lakini tukapoteza umakini mwishoni na tulistahili kuadhibiwa.”