Jipindue uchekwe! EPL lazima kieleweke
Muktasari:
- Mechi ya mwisho katika mzunguko huu wa ligi itapigwa Jumatatu, ambapo Fulham itakuwa uwanjani Craven Cottage kukipiga na Nottingham Forest katika moja ya mechi zinazotazamiwa kuwa na upinzani mkali ndani ya uwanja. Mambo ni moto.
LONDON, ENGLAND: MSIMAMO wa Ligi Kuu England unavyosoma, Arsenal ipo kileleni kwa tofauti ya pointi mbili dhidi ya Manchester City.
Unaweza kuona presha inavyozidi kupanda. Hii ina maana, ukizubaa tu, umeachwa kwa mataa. Na presha zaidi ipo kwa kocha Mikel Arteta, atashuka uwanjani na kikosi chake cha Arsenal wakati huo akiwa tayari ameshajua matokeo ya wapinzani wake kwenye mbio za ubingwa, Man City ya Pep Guardiola.
Man City mapema tu itajimwaga uwanjani kwake Etihad kukipiga na West Ham United, saa kadhaa kabla ya Arsenal kucheza ugenini kuwakabili Everton. Patamu hapo.
Rekodi zinaonyesha, Man City na West Ham zimekutana mara 48 kwenye mechi za Ligi Kuu England, ambapo kwenye mechi hizo sare ni nane, huku wababe wa Etihad wakishinda 31, mara 20 nyumbani na 11 ugenini, wakati West Ham imeshinda tisa tu, mara saba nyumbani na mbili tu ilipokwenda kucheza ugenini. Mechi tano zilizopita, Man City imeshinda zote, hivyo kwenye karatasi, chama la Guardiola lina nafasi kubwa ya kuibuka na ushindi.
Ushindi kwa Man City utafanya kuwaengua Arsenal kileleni kwa tofauti ya pointi moja na hivyo kumpa presha Arteta atakayehitaji kuichapa Everton ugenini ili kurejea kwenye kilele cha ligi hiyo.
Kwenye rekodi za Ligi Kuu England, Everton na Arsenal zimekutana mara 66, ambapo 16 zilimalizika kwa sare, huku wenyeji wa mchezo huu, Everton wameshinda 12, mara 10 nyumbani na mbili ugenini, wakati Arsenal imeshinda mara 38, mechi 25 nyumbani na 13 ugenini.
Hiyo ina maana Arsenal imeshinda mara nyingi ilipokwenda kuwakabili Everton kwao, tofauti na walivyoshinda wenyeji wao wa mchezo wa Jumamosi. Mambo ni moto.
Chelsea itahitaji kushinda mbele ya Newcastle United ili kujiimarisha kwenye nafasi ya nne katika msimamo wa ligi hiyo.
Ripoti zinaonyesha Chelsea na Newcastle zimekutana mara 60 kwenye Ligi Kuu England, huku 13 zikimalizika kwa sare, wakati Newcastle ikishinda 16, mara 15 nyumbani na moja tu ugenini, wakati Chelsea yenyewe imeshinda 31, mara 22 nyumbani na tisa tu ilipokwenda kuikabili Newcastle kwenye Uwanja wa St James' Park.
Kipute kingine cha vuta nikuvute kitakuwa huko London, wakati Tottenham Hotspur itakapojaribu kurudi kwenye hali yake ya ushindi itakapokabiliana na Liverpool inayoonekana kujipata kwa sasa.
Namba zinaonyesha, Spurs na Liverpool zimekutana mara 66 kwenye Ligi Kuu England, 17 zilimalizika kwa sare, wakati wenyeji wa kipute hicho cha Jumamosi hii, Spurs wameshinda 15, mara 13 walipocheza nyumbani na mbili ugenini, wakati Liverpool imeshinda mara 34, ambapo mara 22 ilifanya hivyo nyumbani na mara 12 ugenini.
Mechi nyingine za Jumamosi, Bournemouth itakuwa nyumbani kucheza na Burnley, Brighton itakipiga na Sunderland, wakati Wolves itamaliza ubishi na Brentford katika mechi inayotazamiwa kuwa na upinzani mkali huko Molineux huku Leeds United ikiwa na kasheshe la kuulizana maswali magumu na Crystal Palace.
Jumapili itapigwa mechi moja tu, lakini yenyewe imebeba presha kubwa kwa Arsenal na Man City kutokana na timu mbili zinazokutana, moja kuwa na nafasi kubwa ya kuzifikia timu mbili za juu endepo kama zitaboronga kwenye katika mechi zao.
Aston Villa ipo kwenye nafasi ya tatu katika msimamo, pointi tatu nyuma ya vinara Arsenal na pointi moja tu nyuma ya timu inayoshika nafasi ya pili, Man City.
Hiyo ina maana, kuteleza kwa Arsenal na Man City kwenye mechi zao, kisha Aston Villa ikashinda mechi yake ya Villa Park watasogea kukabana koo kwenye kilele cha msimamo.
Lakini, kibarua cha Aston Villa chini ya kocha Unai Emery hakikatakuwa chepesi kutokana na ukweli itakabiliana na Manchester United iliyopo kwenye kiwango chake bora kwa sasa.
Hata hivyo, Arteta na Guardiola presha inaweza kuwaondoka kutokana na rekodi za mechi za Ligi Kuu England ilizokutanisha Aston Villa na Man United.
Namba zinaonyesha kwamba miamba hiyo imekutana mara 60, ambapo mara 14 zilimalizika kwa sare, huku Aston Villa ikishinda tano tu, mara tatu nyumbani na mbili ugenini, huku Man United ikishinda mara 41, mara 23 ilipocheza nyumbani na 18 ilipoifuata Aston Villa kwenye uwanja wao wa Villa Park.
Mechi tano zilizopita, Man United imeshinda nne na sare ni moja tu, namba ambazo zinaonekana kwenye karatasi kikosi cha Ruben Amorim kina nafasi kubwa ya kushinda mechi hiyo. Itakuwaje?
Mechi ya mwisho katika mzunguko huu wa ligi itapigwa Jumatatu, ambapo Fulham itakuwa uwanjani Craven Cottage kukipiga na Nottingham Forest katika moja ya mechi zinazotazamiwa kuwa na upinzani mkali ndani ya uwanja. Mambo ni moto.