Evra amtetea Ruben Amorim
Muktasari:
- Man United ilipata ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Wolves yenye hali mbaya, lakini licha ya ushindi huo bado kumekuwa na minong’ono tangu kuanza kwa msimu huu ambapo baadhi ya wachambuzi wamekuwa wakimkosoa kwa uamuzi wake ukiwamo wa kutomchezesha Kobbie Mainoo na kuwaachia wachezaji vijana kama Alejandro Garnacho kwenda timu nyingine za EPL.
MANCHESTER, ENGLAND: BEKI wa zamani wa Manchester United, Patrice Evra, ameonyesha kumuunga mkono kocha wa mashetani wekundu hao, Ruben Amorim, akidai kuwa ndiye mtu sahihi kwa sasa kwani anatanguliza maslahi ya klabu badala ya kwake binafsi.
Man United ilipata ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Wolves yenye hali mbaya, lakini licha ya ushindi huo bado kumekuwa na minong’ono tangu kuanza kwa msimu huu ambapo baadhi ya wachambuzi wamekuwa wakimkosoa kwa uamuzi wake ukiwamo wa kutomchezesha Kobbie Mainoo na kuwaachia wachezaji vijana kama Alejandro Garnacho kwenda timu nyingine za EPL.
Evra ambaye aliwahi kucheza Man United kwa miaka tisa na akiwa sehemu ya kipindi cha mafanikio makubwa zaidi katika historia ya klabu, amepingana na wachezaji wenzake wa zamani Paul Scholes na Gary Neville ambao wamekuwa wakimsema vibaya Amorim katika wiki chache zilizopita.
“Hata katika nyakati mbaya bado nitaendelea kumwamini. Yeye ni mtu ambaye kwa sasa yupo tayari hata kufa kwa ajili ya klabu. Hivyo ndivyo hisia zangu zinavyoniambia kuhusu Amorim. Namwona kama ni mtu ambaye anaweka maslahi ya klabu mbele kisha yeye anakaa nyuma, tofauti na baadhi ya kocha aliyepita kabla yake, namuona yuko tofauti.
“Kuhusu mwenendo wa timu nafikiri labda anahitaji wachezaji zaidi. Nikiiangalia Man United kwa sasa siwezi kuipa asilimia kubwa ya mafanikio, dakika moja inafaulu na dakika nyingine inafeli, hivyo huwezi kutabiri matokeo yao.”
Man United imesogea hadi nafasi ya sita katika msimamo wa Ligi Kuu England baada ya ushindi wake dhidi ya Wolves ambao umeiwezesha kufikisha pointi 25.