Salah atabiriwa mabaya AFCON 2025
Muktasari:
- Endapo hilo litatimia, Salah aliyejiunga na wenzake wa timu ya taifa kwa ajili ya mechi yao ya ufunguzi wa michuano hiyo dhidi ya Zimbabwe itakayopigwa wiki ijayo, atarejea England mapema na huenda akacheza hata mechi dhidi ya Arsenal.
RABAT, MOROCCO: HOFU imezidi kuongezeka kwa mashabiki wa soka huko Misri baada ya timu hiyo ya staa wa Liverpool, Mohamed Salah kutabiriwa na kompyuta mpya kuwa itatolewa mapema katika michuano ya mataifa ya Afrika inayotarajiwa kuanza wiki ijayo huko Morocco.
Endapo hilo litatimia, Salah aliyejiunga na wenzake wa timu ya taifa kwa ajili ya mechi yao ya ufunguzi wa michuano hiyo dhidi ya Zimbabwe itakayopigwa wiki ijayo, atarejea England mapema na huenda akacheza hata mechi dhidi ya Arsenal.
Misri inatabiriwa kutolewa AFCON kwa kufungwa na Comoros katika hatua ya 16 bora.
Wakati fulani, ilionekana kuwa huenda nyota huyo wa Liverpool asirejee England mapema kutoka kwenye mashindano hayo yanayofanyika Morocco.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 33 aliikosoa klabu yake na kocha Arne Slot katika mahojiano yake aliyofanya baada ya kumalizika kwa mechi dhidi ya Leeds United ambayo ilikuwa ya tatu kwake kuanzishwa benchini.
Kutokana na kauli zake, Salah hakujumuishwa kwenye kikosi cha Liverpool kilichokutana na Inter, lakini alirejea kikosini na kuingia kama mchezaji wa akiba katika mechi waliyoibuka na ushindi dhidi ya Brighton.
Salah atakosa mechi kadhaa za EPL ikiwamo dhidi ya Tottenham na Wolves zitakazopigwa mwisho wa mwezi huu wakati huo Salah akiwa na kibarua cha kuipambania Misri kwenye mechi za hatua ya makundi AFCON dhidi ya Zimbabwe, Angola na Afrika Kusini.
Hata hivyo, safari ya nyota huyo kwenda Morocco huenda isiwe ndefu sana, kwa mujibu wa supercomputer ya BookmakersCameroun.com, ambayo inatabiri Misri itafungwa kwa bao 1-0 na timu ndogo ya Comoros.
Mechi za hatua ya 16 bora zitachezwa kati ya Jumamosi Januari 3 hadi Jumanne ya Januari 6, 2026, huku Liverpool ikitarajiwa kucheza na Arsenal katika Ligi Kuu England Januari 8.
Hata hivyo, huenda asicheze mechi hiyo ya Arsenal hata kama Misri ikitolewa kweli na Comoros kwani muda hautotosha kwa ajili ya maandalizi yake lakini anaweza kuiwahi mechi ya FA dhidi ya Barnsley Januari 12.
Salah hakucheza mechi ya kirafiki ya maandalizi ya michuano hiyo dhidi ya Nigeria baada ya kuchelewa kuwasili kambini pamoja na nyota wa Manchester City, Omar Marmoush.