Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Jichanganye, uchanganywe! Arsenal haikati utani EPL

EPL Pict

Muktasari:

  • Kwenye mchakamchaka huo wa kusaka ubingwa, chama hilo la Mikel Arteta, litakabiliwa na mechi ngumu kabisa dhidi ya Aston Villa uwanjani Villa Park, Jumamosi hii. Na Arsenal haitaki kujichanganya kwenye mbio za ubingwa ili isichanganywe na wapinzani wao.

LONDON, ENGLAND: NDO hivyo. Arsenal iko siriazi kwenye kuusaka ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu. Pointi 33 kileleni baada ya mechi 14, ikishinda 10, sare tatu na kupoteza moja tu. Imefunga mabao 27 na kufungwa saba tu, huku ikiweka pengo la pointi tano dhidi ya timu inayoshika nafasi ya pili, Manchester City.

Kwenye mchakamchaka huo wa kusaka ubingwa, chama hilo la Mikel Arteta, litakabiliwa na mechi ngumu kabisa dhidi ya Aston Villa uwanjani Villa Park, Jumamosi hii. Na Arsenal haitaki kujichanganya kwenye mbio za ubingwa ili isichanganywe na wapinzani wao.

Aston Villa inanolewa na kocha wa zamani wa Arsenal, Unai Emery, ambaye amekuwa na rekodi nzuri ya kutibua mambo dhidi ya wababe hao wa Emirates. Safari hii itakuwaje?

Rekodi zinaonyesha kwamba, Aston Villa na Arsenal zimekutana mara 60 kwenye mechi za Ligi Kuu England, mara 15 gemu zilimalizika kwa sare, huku miamba ya Villa Park imeshinda 13, mara sita nyumbani na saba ugenini, wakati Arsenal imeshinda 32, mara 17 nyumbani na 13 ugenini ilipokwenda Villa Park. Kwenye rekodi za jumla, Arsenal imetamba mara nyingi mbele ya Aston Villa, lakini kwa takwimu za mechi tano zilizopita miamba hiyo ilipokutana kwenye Ligi Kuu England, Aston Villa imeshinda mara tatu, sare moja na Arsenal imeshinda moja tu. Je, Unai Emery atamtibulia tena Arteta?

EP 01

Arteta na chama lake la Arsenal atahitaji kupata ushindi ili kuendeleza pengo la pointi lililopo huku akiombea mabaya wapinzani wateleze kwenye mechi zao.

Wapinzani wa Arsenal kwenye mbio za ubingwa, Man City wenyewe watakuwa na kibarua cha kukabiliana na timu ngumu ya Sunderland uwanjani Etihad. Ni mechi ngumu kwa vijana wa Pep Guardiola kutokana na kiwango cha Sunderland msimu huu baada ya kupanda daraja.

Kwenye vitabu vya rekodi, Man City na Sunderland zimekutana mara 26 kwenye mechi za Ligi Kuu England na tatu kati ya hizo zilimalizika kwa sare, huku miamba ya Etihad ikiwa imeshinda 18, mara 11 nyumbani na saba ugenini, huku Sunderland yenyewe imeibuka na ushindi mara tano tu ilipocheza na wapinzani wao hao, huku mechi zote hizo ikishinda nyumbani na haijawahi kuonja ushindi ugenini. Je, safari hii watatoboa?

Mabingwa watetezi Liverpool watakuwa kwenye wakati mgumu sana watakapokwenda ugenini kucheza na Leeds United. Kipute hicho cha uwanjani Elland Road kitachezeshwa na mwamuzi Anthony Taylor huku Leeds United ikonyesha kuwa ni timu inayofunga mabao mengi kwa siku za hivi karibuni baada ya kufunga mara saba katika mechi mbili za mwisho, dhidi ya Man City na Chelsea. Je, kwa beki ile ya Liverpool itaweza kuidhibiti Leeds United isitikisa nyavu zao?

EP 02

Lakini, kwenye rekodi zao, Leeds na Liverpool zimekutana mara 30, huku sare ni tatu na Leeds imeshinda saba, mara tatu nyumbani na nne ugenini, huku Liverpool imeshinda mara 18, mara 10 ilipocheza nyumbani na nane ugenini ilipokwenda kwenye Uwanja wa Elland Road. Mechi tano zilizopita, Liverpool imeshinda tatu, sare moja na Leeds imepata ushindi mmoja. Lakini, kasheshe lipo msimu huu. Itakuwaje?

Katika mechi nyingine zitakazopigwa Jumamosi hii, Bournemouth itakipiga na Chelsea ikiwa ni moja ya mechi zitakazokuwa na mvuto mkubwa huku Everton ikitarajia kucheza na Nottingham Forest, wakati Newcastle United itajimwaga uwanjani kwake St James' Park kukabiliana na Burnley, huku Tottenham Hotspur itakuwa na kasheshe zito la kuonyesha ubabe na wababe wenzao wa London, Brentford.

Mchakamchaka wa ligi hiyo utaendelea Jumapili kwa mechi mbili, ambapo Brighton itakuwa nyumbani kukabiliana na West Ham United, huku Fulham ikikabiliwa na mechi ngumu kabisa ya kuvaana na Crystal Palace. Ni vuta nikuvute.

Wazee wa mwendo wa kusuasua wa moja nzuri tatu mbaya, Manchester United itasubiri hadi Jumatatu kukipiga na Wolves ugenini. Man United ya kocha Ruben Amorim ilipoteza nafasi ya kupata hadi nafasi ya tano kwenye msimamo wa Ligi Kuu England baada ya kubanwa uwanjani Old Trafford na kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya West Ham United usiku wa Alhamisi iliyopita.

Man United sasa itarusha kete yake muhimu ugenini kwa kukabiliana na Wolves inayoburuza mkia kwenye msimamo wa Ligi Kuu England, ikiwa imevuna pointi mbili tu katika mechi 14 ilizocheza. Katika rekodi za mechi za Wolves na Man United zilipokutana kwenye Ligi Kuu England, mara 22 na sare zilikuwa tatu huku Wolves ikishinda sita, nne nyumbani na mbili ugenini, wakati Man United imeshinda 13, mara saba nyumbani na sita ilipokwenda ugenini Molineux kukipiga mahali ambako itafanyika mechi hiyo ya Jumatatu, itakayochezeshwa na mwamuzi Michael Salisbury.