Afcon 2025 itakavyoacha balaa Ligi Kuu England
Muktasari:
- Na fainali hizo za Afcon 2025, zitafika ukomo kwa mechi ya fainali itakayopigwa Januari 18, 2026. Na fainali hizo ambazo huko nyuma zilikuwa zikifanyika kati ya Januari na Februari, sasa zitaanza Desemba na kumalizika Januari na zitahusisha timu 24.
LONDON, ENGLAND: KIVUMBI cha kusaka ubingwa wa Afrika kwa timu za taifa maarufu kama Afcon kitaanza rasmi huko Morocco kuanzia Desemba 21, 2025.
Na fainali hizo za Afcon 2025, zitafika ukomo kwa mechi ya fainali itakayopigwa Januari 18, 2026. Na fainali hizo ambazo huko nyuma zilikuwa zikifanyika kati ya Januari na Februari, sasa zitaanza Desemba na kumalizika Januari na zitahusisha timu 24.
Hakika mashindano hayo ya Afcon 2025 yanakwenda kuzipa presha kubwa timu za Ligi Kuu England kwa sababu zitakosa huduma za mastaa wao wa maana ambao wataondoka kwenda kuungana na timu zao za taifa huko Afrika. Wakati ligi za mataifa mengine ya Ulaya zikiwa na utaratibu wa kuingia kwenye mapumziko katika kipindi cha Krismasi, hali ni tofauti kwenye Ligi Kuu England, ambapo kwa kipindi hicho, mambo ndiyo yanazidi kuwa moto zaidi katika mbio za ubingwa, mbio za kukimbizia tiketi ya kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya na michuano mingine ya Ulaya na pia mchakamchaka wa kukwepa kushuka daraja.
Kwenye Ligi Kuu England kuna timu kadhaa zitaathirika kwa kiwango kikubwa kutokana na mastaa wake matata kuondoka na kwenda kujiunga na timu zao za taifa kwa ajili ya kivumbi cha Afcon 2025.
LIVERPOOL
Mohamed Salah atakwenda kwenye Afcon 2025, hiyo ina maana mabingwa hao wa Ligi Kuu England watakosa huduma ya Mchezaji Bora wa Mwaka wa msimu uliopita kwenye mechi muhimu kabisa za kampeni yao ya kutetea ubingwa. Mo Salah atakuwa kwenye kikosi cha Misri na hilo bila shaka litaacha pengo kwenye kikosi cha Liverpool, ambacho kwa sasa kinajaribu kujitafuta kwenye Ligi Kuu England. Na kwa kipindi ambacho Mo Salah atakuwa kwenye kikosi cha Misri, Liverpool itakuwa na mechi kadhaa bila ya huduma yake.
Mechi itakazocheza Liverpool wakati Mo Salah atakapokuwa kwenye Afcon 2025;
-Desemba 20 vs Tottenham (ugenini)
-Desemba 27 vs Wolves (nyumbani)
-Desemba 30 vs Leeds United (nyumbani)
-Januari 3 vs Fulham (ugenini)
-Januari 7 vs Arsenal (ugenini)
-Januari 17 vs Burnley (nyumbani)
MAN CITY
Kocha Pep Guardiola anakiandaa kikosi chake cha Manchester City kucheza bila ya huduma ya mastaa wake Omar Marmoush na Rayan Ait Nouri, ambao watakuwa kwenye kikosi cha Misri na Algeria mtawalia katika michuano ya Afcon 2025. Marmoush amekuwa na mchango mkubwa tangu alipojiunga na Man City akitokea Eintracht Frankfurt na kufunga mabao ya kutosha katika kikosi hicho cha Etihad. Man City inapambana kwenye mbio za ubingwa, lakini itawakosa wachezaji wake hao kwenye mechi muhimu kabisa, ikiwamo ile ya Manchester derby itakayopigwa uwanjani Old Trafford.
Mechi itakazocheza Man City wakati Marmoush na Ait Nouri watakapokuwa Afcon 2025;
-Desemba 20 vs West Ham (nyumbani)
-Desemba 27 vs Nottingham Forest (ugenini)
-Desemba 30 vs Sunderland (ugenini)
-Januari 3 vs Chelsea (nyumbani)
-Januari 7 vs Brighton (nyumbani)
-Januari 17 vs Man United (ugenini)
MAN UNITED
Kocha wa Manchester United, Ruben Amorim atakosa huduma ya beki wa kulia Noussair Mazraoui (Morocco) na washambuliaji Amad Diallo (Ivory Coast) na Bryan Mbeumo (Cameroon). Wakati huu kocha Amorim akipambana kuweka mambo sawa kwenye Ligi Kuu England, atakabiliwa na mechi muhimu kwenye kipindi hiki cha Desemba akikosa huduma za wachezaji wake mahiri, Amad na Mbeumo watakaokuwa Afcon 2025.
Mechi itakazocheza Man United wakati Amad na Mbeumo watakuwa kwenye Afcon 2025;
-Desemba 20 vs Aston Villa (ugenini)
-Desemba 27 vs Newcastle (nyumbani)
-Desemba 30 vs Wolves (nyumbani)
-Januari 3 vs Leeds United (ugenini)
-Januari 7 vs Burnley (ugenini)
-Januari 17 vs Man City (nyumbani)
TOTTENHAM
Kocha wa Tottenham Hotspur, Thomas Frank atakosa huduma za wakati wake kama Yves Bissouma na Pape Matar Sarr katika fainali hizo za Afcon 2025, lakini bahati nzuri kwake ni kwamba ataendelea kuwa na makali ya Mohamed Kudus, kwa sababu timu yake ya Ghana haijafuzu kucheza mashindano hayo ya ubingwa wa Afrika.
Spurs ipo kwenye mchakato muhimu wa kuhakikisha inavuna matokeo mazuri ili kushindania nafasi ya kucheza kwenye michuano ya Ulaya.
Mechi ambazo Spurs itacheza bila ya huduma za wakali wake watakaokwenda Afcon 2025;
-Desemba 20 vs Liverpool (nyumbani)
-Desemba 27 vs Crystal Palace (ugenini)
-Desemba 30 vs Brentford (ugenini)
-Januari 3 vs Sunderland (nyumbani)
-Januari 7 vs Bournemouth (ugenini)
-Januari 17 vs West Ham (ugenini)
CHELSEA & ARSENAL
Makocha Enzo Maresca wa Chelsea na Mikel Arteta wa Arsenal wenyewe hawatakuwa na presha yoyote katika kuelekea mashindano hayo ya Afcon 2025 kutokana na kutokuwapo na wachezaji wowote wa Kiafrika katika vikosi vyao, hivyo watacheza mechi za kipindi hiki ambacho michuano hiyo itakuwa ikiendelea huko Morocco wakiwa na wachezaji wao wote muhimu bila ya kuharibu mipango yao.
Timu nyingine za Ligi Kuu England ambazo zitakuwa na wachezaji wao kwenye mashindano ya Afcon 2025;
Aston Villa: Evann Guessand (Ivory Coast)
Bournemouth: Amine Adli (Morocco)
Brentford: Dango Outtara (Burkina Faso), Frank Onyeka (Nigeria)
Brighton: Carlos Baleba (Cameroon)
Crystal Palace: Cheick Doucoure (Mali), Chadi Riad (Morocco), Christantus Uche (Nigeria) na Ismaila Sarr (Senegal).
Everton: Iliman Ndiaye na Idrissa Gueye (Sengal), Adam Aznou (Morocco).
Fulham: Alex Iwobi, Calvin Bassey na Samuel Chukwueze (Nigeria)
Nottingham Forest: Ola Aina na Taiwo Awoniyi (Nigeria), Willy Boly na Ibrahim Sangare (Ivory Coast).
Sunderland: Arthur Masuaku na Noah Sadiki (DR Congo), Chemsdine Talbi (Morocco), Habib Diarra (Senegal), Reinildo (Msumbuji), Simon Adingra (Ivory Coast) na Bertrand Traore (Burkina Faso).
West Ham: Aaron Wan-Bissaka (DR Congo), El Hadji Malick Diouf (Senegal).
Wolves: Marshall Munetsi na Tawanda Chirewa (Zimbabwe), Emmanuel Agbadou (Ivory Coast), Tolu Arokodare (Nigeria).