Infantino atwishwa kashfa ya mapenzi UEFA
Muktasari:
- UEFA imethibitisha kwamba ilifanya malipo ya kuondoka kazini kwa mfanyakazi huyo, ambaye ameripotiwa kuwa alikuwa katika uhusiano na Infantino. Hata hivyo, FIFA imepuuza madai hayo na kuyaita “siyo ya kweli.”
LONDON, ENGLAND: RAIS wa Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), Gianni Infantino amekanusha madai kwamba Shirikisho la Soka Ulaya (UEFA) lilimlipa fedha mfanyakazi wa kike aliyedaiwa kuwa na uhusiano naye wa kimapenzi wakati akiwa katibu mkuu wa taasisi hiyo.
UEFA imethibitisha kwamba ilifanya malipo ya kuondoka kazini kwa mfanyakazi huyo, ambaye ameripotiwa kuwa alikuwa katika uhusiano na Infantino. Hata hivyo, FIFA imepuuza madai hayo na kuyaita “siyo ya kweli.”
Gazeti la Daily Telegraph limeripoti kwamba mwanamke huyo alipokea kiasi cha fedha chenye thamani ya zaidi ya tarakimu sita kufuatia uhusiano huo uliodaiwa kuwa dhidi yake na Infantino.
Katika taarifa yake, UEFA imethibitisha kwamba malipo yalifanyika pamoja na kugharamia ada za kozi ya Shahada ya Pili ya Biashara, ikisema hatua hiyo ilikuwa “sambamba” na kanuni zilizokuwepo wakati huo. Hata hivyo, FIFA ilijibu taarifa hizo kwa kukanusha madai hayo.
“Rais wa FIFA, Gianni Infantino, anakanusha vikali madai haya na hayana ukweli kabisa. Dhana yoyote ya tabia isiyofaa au ukiukaji wa katiba na kanuni ni ya kumchafua,” msemaji wa FIFA ameiambia Telegraph.
Msemaji huyo ameongeza: “Hakuna mfanyakazi yeyote wa UEFA au FIFA aliyewahi kuwasilisha malalamiko kuhusu tabia ya Bw. Infantino kwa sababu hakukuwa na tukio lolote alilohusika.”
Taarifa hizo zimeibuka wakati presha dhidi ya Infantino ikiongezeka kufuatia mpango wake wa kutafuta uwekezaji kutoka kwa kampuni binafsi katika kampuni ambayo ingeendesha mashindano ya FIFA, ikiwamo Kombe la Dunia la wanaume na wanawake.
Infantino alifanya kazi UEFA kwa miaka 16, na mwaka 2009 akawa katibu mkuu wa taasisi hiyo. Alimudu nafasi hiyo hadi alipochaguliwa kuwa rais wa FIFA Februari 2016.
Kwa upande wake, msemaji wa UEFA amesema: “Tunafahamu madai hayo na tunaweza kuthibitisha kwamba malipo ya kuondoka kazini yalifanywa kwa mtu husika, pamoja na kugharamia ada za kozi ya Shahada ya Pili ya Biashara katika shule ya biashara ya eneo hilo.”
UEFA imesema malipo hayo yalikuwa kwa mujibu wa kanuni zilizokuwa zinatumika kwa wafanyakazi waliokuwa wakiondoka katika taasisi hiyo wakati huo.
Taasisi hiyo imeongeza kwamba kanuni zake zimeimarishwa tangu mwaka 2016, huku taratibu zinazotumika sasa kwa wafanyakazi wote wa UEFA, bila kujali nafasi zao zikilenga kuakisi viwango vya taasisi ya kisasa yenye hadhi kubwa.
Infantino amekuwa katikati ya mvutano mkubwa kwa takribani wiki mbili kufuatia mpango wake wa kuuza hisa kwa wawekezaji binafsi katika kampuni ambayo ingeendesha Kombe la Dunia.
Mpango huo ulikataliwa na UEFA pamoja na mashirikisho mengine mawili ya mabara.
Jumatano, Infantino alipata uungwaji mkono kutoka kwa bodi ya uongozi ya FIFA baada ya kikao kilichofanyika Morocco, huku pia akiomba radhi kuhusu namna mchakato huo ulivyoendeshwa.
Hata hivyo, tishio la UEFA kwa nchi zake wanachama 55 kususia mashindano ya FIFA hadi mpango huo utakapoondolewa bado lipo.
UEFA ilisema Alhamisi kwamba tangazo la Jumatano “halibadilishi chochote” kuhusu msimamo wake.