Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Gianni Infantino agoma kujiuzulu

INFANTINO Pict

Muktasari:

  • Baada ya kuitisha kikao cha dharura mjini Rabat, Morocco, Infantino ameonekana kunusurika kwa sasa katika kashfa kubwa inayohusu mpango wake uliositishwa wa kuuza sehemu ya haki za kibiashara za Kombe la Dunia kwa wawekezaji binafsi.

RABAT, MOROCCO: RAIS wa FIFA Gianni Infantino amekataa kujiuzulu, huku akipewa kile kilichoelezwa kuwa ni uungwaji mkono kamili kutoka kwa viongozi wa juu wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), hatua inayomuweka katika nafasi nzuri ya kuendelea kuiongoza taasisi hiyo licha ya wimbi kubwa la shinikizo la kuondoka madarakani.

Baada ya kuitisha kikao cha dharura mjini Rabat, Morocco, Infantino ameonekana kunusurika kwa sasa katika kashfa kubwa inayohusu mpango wake uliositishwa wa kuuza sehemu ya haki za kibiashara za Kombe la Dunia kwa wawekezaji binafsi.

Mwisho wa siku nyingine yenye misukosuko mikubwa ndani ya FIFA, nguli wa soka wa Ureno, Luis Figo alijiunga na orodha ya watu maarufu waliomtaka Infantino aondoke madarakani, akitoa mashambulizi makali dhidi yake.

Katika makala yenye maneno zaidi ya 600, Figo aliuelezea mpango huo wa kuuza hisa za Kombe la Dunia kuwa ni “kitendo cha chini kabisa, cha udanganyifu mkubwa na cha ubinafsi wa kutisha kuwahi kushuhudiwa”, huku akiuita pia kuwa ni “mpango mchafu uliofanywa kwa kificho.”

Kauli hizo ziliongeza presha kubwa dhidi ya Infantino, ambaye alikuwa ameita kikao hicho cha dharura akijaribu kuokoa nafasi yake ya uongozi.

Hata hivyo, taarifa ndefu iliyotolewa na FIFA usiku wa Jumatano ilikiri kuwa kulikuwa na makosa katika mchakato huo, lakini ikaeleza kuwa tayari wameomba radhi kwa vyama wanachama kupitia barua rasmi na kwamba kutafanyika mapitio ya kina kuhusu kilichotokea.

Katika taarifa hiyo, FIFA ilisema Katibu Mkuu wake Mattias Grafstrom, ambaye hapo awali alikuwa ameonyesha kutoridhishwa na mwenendo wa Infantino, pamoja na wajumbe wengine wa bodi ya utendaji waliohudhuria kikao hicho, “wamethibitisha tena kumpa Rais uungwaji mkono wao kamili.”

FIFA pia ilisisitiza kuwa haitavumilia mashambulizi yoyote dhidi ya uadilifu, utawala bora na taratibu zake za kisheria.

“Daima kuna masomo ya kujifunza, na FIFA itaendelea kuboresha mifumo yake kutokana na uzoefu huu. Hata hivyo, ni muhimu kusisitiza kwamba licha ya makosa yaliyotokea, kila hatua iliyochukuliwa ilikuwa ndani ya mfumo wa kanuni za FIFA.”

INFA 01

FIGO AMSHAMBULIA VIKALI

Figo, ambaye aliwahi kuzichezea Barcelona, Real Madrid na Inter Milan, amesema Infantino ni “masalia ya zamani yasiyostahili kuwa sehemu ya mustakabali wa soka.”

Mreno huyo, ambaye mwaka 2015 alikuwa mmoja wa waliomuunga mkono Infantino, alimshutumu kwa kile alichokiita “mfululizo wa matumizi mabaya ya madaraka.”

Mbali na sakata la kuuza sehemu ya Kombe la Dunia, Figo pia alikosoa uamuzi wa kusimamisha adhabu ya mshambuliaji wa Marekani Folarin Balogun baada ya kadi nyekundu aliyoipata Kombe la Dunia, pamoja na kuanzishwa kwa burudani ya mapumziko ya kipindi cha kwanza katika fainali ya Kombe la Dunia, jambo alilodai “lilivunja sheria za mchezo.”

“Infantino ameishusha hadhi ofisi ya Rais wa FIFA ambayo aliahidi kuiinua. Ameongoza kwa uongo, udanganyifu na kutumia nafasi yake kujinufaisha binafsi kwa gharama ya mchezo anaopaswa kuutumikia.”


UEFA NA CONCACAF WAMGEUKIA

Kauli za Figo zilikuja baada ya Shirikisho la Soka Ulaya (UEFA) kutangaza kupoteza imani kwa Infantino.

UEFA iliuelezea mpango wake wa kuuza shughuli za biashara na matukio ya FIFA kuwa ni “mpango wa aibu, wa kificho na usio na uwazi.”

Kwa upande mwingine, Shirikisho la Soka la Amerika Kaskazini, Kati na Caribbean (CONCACAF) pia limeungana na UEFA kumtaka Infantino aondoke madarakani.

INFA 02

BARUA YA GRAFSTROM

Katika kipindi ambacho mashinikizo yalikuwa yanaongezeka, Katibu Mkuu wa FIFA Mattias Grafstrom aliwatumia wafanyakazi wote wa FIFA ujumbe wa ndani akieleza kuwa hali hiyo ilikuwa “ya kusikitisha na ya kulaumiwa.”

Katika ujumbe huo aliongeza:

“Watu binafsi, nyakati zisizo na utulivu na matukio mabaya huja na kupita.”

Hata hivyo, baada ya kikao hicho, Grafstrom alionekana akicheka na kufanya mazungumzo ya kirafiki na Infantino wakati wa mchezo wa Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake, kabla ya FIFA kutoa taarifa rasmi ya kumuunga mkono rais huyo.


UCHAGUZI WA MACHI

Iwapo ataendelea kubaki madarakani, Infantino atawania tena urais wa FIFA mwezi Machi.

Ili kushinda muhula mwingine, atahitaji kura 106 kati ya wanachama 211 wa FIFA.

Infantino aliwasili Morocco kwa ajili ya kikao hicho muhimu huku akikabiliwa na presha kubwa kufuatia upinzani mpana dhidi ya mpango wake wa kuuza sehemu ya haki za Kombe la Dunia.

Kutokana na upinzani huo mkubwa, alilazimika kufuta mpango huo, huku kukiwa hata na uasi kutoka ndani ya FIFA yenyewe.

INFA 03

JORDAN YAUNGANA NA WANAOMPINGA

Presha iliongezeka zaidi baada ya Rais wa Chama cha Soka Jordan, Prince Ali bin Hussein, kumshutumu Infantino kwa kutumia vitisho na ushawishi usiofaa.

Jordan ikawa nchi ya kwanza kutoka Asia kuasi dhidi ya Rais huyo wa FIFA.

Kwa hatua hiyo, Jordan ikawa chama cha 91 mwanachama kuonyesha msimamo wa kumpinga Infantino, ikiwa mataifa yote ya UEFA na CONCACAF yatafuata msimamo wa mashirikisho yao.

Kwa mujibu wa taratibu za FIFA, mataifa 106 yanahitajika ili kumng’oa Rais wa FIFA madarakani.


FIGO: “NINA MANENO MATATU TU…”

Katika makala yake, Figo amesema:

“Ningeweza kuandika maneno 10,000 kuhusu matatizo yaliyopo FIFA. Lakini suluhisho linahitaji maneno matatu tu: Infantino lazima aondoke.”

Aliendelea kusema:

“Nimependa soka maisha yangu yote. Nilikuwa mchezaji wa kulipwa kwa miaka 20. Nimekutana na watu wengi wasio waaminifu katika mchezo huu, lakini nilichokiona ndani ya siku kumi zilizopita ndicho kiwango cha chini kabisa cha udanganyifu na ubinafsi kuwahi kushuhudiwa.”

Figo alihoji pia ukosefu wa uwazi katika mpango huo.

“Kama ulikuwa mpango mzuri, kwa nini hukuwaeleza wanachama wako ulipokuwa nao wote kabla ya fainali ya Kombe la Dunia? Kama ulikuwa mpango imara, kwa nini hukuweka wazi hatari zake pamoja na faida ulizokuwa unazitaja?”

INFA 04

Aliendelea kuhoji:

“Kama ulikuwa mpango usio na shaka yoyote, kwa nini hukusema wazi kwamba ungepata kazi yenye mshahara wa dola milioni 30 kwa mwaka baada ya utekelezaji wake?”

Kwa mujibu wa Figo, mpango huo haukuwa wa uaminifu kwa sababu haukuwaweka wazi wanachama kuhusu faida kubwa ambazo wawekezaji binafsi wangepata, huku pia ukinyang’anya vizazi vijavyo umiliki wa sehemu ya Kombe la Dunia.

Aliongeza kuwa FIFA tayari ina akiba ya zaidi ya dola bilioni tano, hivyo hakukuwa na sababu ya kuuza sehemu ya mashindano hayo kwa wawekezaji binafsi.

“Infantino ameidhalilisha ofisi ya Rais wa FIFA ambayo aliahidi kuiinua. Ameongoza kwa uongo, udanganyifu na kujitafutia maslahi binafsi kwa gharama ya mchezo anaopaswa kuutumikia... anapaswa kuondoka sasa.”

INFA 05

WENGINE WAJITENGA

Infantino pia anakabiliwa na upinzani kutoka kwa baadhi ya viongozi waandamizi wa FIFA.

Ofisa Mkuu wa Uendeshaji wa FIFA, Kevin Lamour, amesema alihisi kudanganywa kuhusu mpango huo, huku Mkuu wa Maendeleo ya Soka Duniani Arsene Wenger akiwa miongoni mwa waliojitenga na mpango huo uliositishwa kwa haraka.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya FIFA, morali ya wafanyakazi imeshuka hadi kiwango cha chini kabisa.


FIGO ATAJWA MRITHI WA CEFERIN

Figo, ambaye sasa ana miaka 53 na aliwahi kugombea urais wa FIFA, anaonekana na wengi kama mmoja wa watu wanaoweza kumrithi Rais wa UEFA Aleksander Ceferin siku zijazo.

Mwaka 2015, Figo na Prince Ali bin Hussein waligombea urais wa FIFA dhidi ya Sepp Blatter.

Figo alijiondoa kabla ya uchaguzi kukamilika, huku Prince Ali akijiondoa baada ya duru ya pili ya upigaji kura.

Blatter alitangaza kujiuzulu siku nne tu baada ya kuchaguliwa tena kutokana na shinikizo kubwa alilokumbana nalo.

Kwa mujibu wa gazeti la The Times, washirika wa Infantino walikuwa wakijaribu kuwashawishi baadhi ya nyota wa zamani wa soka wanaoshirikiana na FIFA kutoa kauli za kumuunga mkono hadharani, lakini jitihada hizo hazikufanikiwa.

Wachezaji hao wa zamani ni miongoni mwa wale wanaolipwa na FIFA kushiriki katika shughuli mbalimbali za shirikisho hilo duniani.