Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Hii ni vita ya watoto wa London

Muktasari:

  • Kabla ya hapo, Arsenal watakuwa wageni wa Fulham katika mchezo utakaoanza saa 11 jioni pale Craven Cottage. Hizi zote ni London Derby.

LONDON, ENGLAND: Leo kuna vita ya watoto wa London ndani ya Premier League huku mechi kubwa zaidi ikiwa ni Tottenham Hotspur dhidi ya Chelsea ambayo itafunga siku ikichezwa saa 1 usiku kwenye uwanja wa kisasa wa Tottenham Hotspur.

Kabla ya hapo, Arsenal watakuwa wageni wa Fulham katika mchezo utakaoanza saa 11 jioni pale Craven Cottage. Hizi zote ni London Derby.


Tottenham vs Chelsea

Mechi hii inachukua uzito mkubwa kutokana na historia ya ushindani wa timu hizi, hali ya sasa ya msimamo wa ligi, na matarajio ya mashabiki wa pande zote mbili. 

Kwa Tottenham, mechi hii ni nafasi ya kuokoa msimu wao unaoonekana kuyumba, huku Chelsea wakitafuta kuimarisha matumaini yao ya ubingwa wa Ligi Kuu ya England. Ni mchuano wa presha kubwa, ukijumuisha heshima, matamanio ya ushindi, na mustakabali wa makocha wa timu zote mbili.

Spurs wanakutana na Chelsea wakiwa katika hali ngumu baada ya kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Bournemouth katikati ya wiki. Makocha wengi wapya hupewa muda wa kujenga timu zao, lakini kwa Ange Postecoglou, muda huo unazidi kupungua. Hili linatokana na mwenendo usioridhisha wa timu yake katika michezo ya karibuni, ambapo wamepoteza mara tatu mfululizo. Matokeo mabaya zaidi yanaweza kumaanisha mwisho wa safari yake kama kocha wa Spurs, hasa kutokana na presha kutoka kwa bodi ya klabu chini ya mwenyekiti Daniel Levy. 

Changamoto ya majeruhi imechangia matokeo haya mabaya. Kikosi cha Spurs kimekumbwa na majeraha kadhaa ya wachezaji muhimu kama kipa Guglielmo Vicario, mlinzi Ben Davies, na mshambuliaji Richarlison. Cristian Romero, mmoja wa mabeki wao wa kutegemewa, yuko katika mashaka ya kucheza.

Hata hivyo, nahodha wao Heung-min Son anatarajiwa kurejea katika kikosi cha kwanza, huku akitarajiwa kuwaongoza vijana wa Spurs katika safu ya ushambuliaji. 

Licha ya rekodi ya kushindwa mara nyingi dhidi ya Chelsea, mashabiki wa Spurs wanahitaji kuona mabadiliko ya kasi na uwajibikaji, hasa kutokana na kipigo kikali cha 4-1 walichopokea kutoka kwa wapinzani wao msimu uliopita. Ange anajua kuwa kushinda mechi hii zaidi ya pointi tatu ni nafasi ya kurejesha imani ya mashabiki na kuzuia wingu la kufutwa kazi linalotanda juu yake.

Kwa upande wa Chelsea, hali ni tofauti kabisa. Timu hii, inayoongozwa na kocha Enzo Maresca, imeimarika baada ya ushindi mnono wa 5-1 dhidi ya Southampton wiki hii. Ushindi huu uliwaonyesha upana wa kikosi cha Chelsea, ambapo wachezaji wa akiba kama Christopher Nkunku na Noni Madueke walionyesha uwezo mkubwa. 

Kocha Maresca ameweza kudhibiti changamoto za mzunguko wa wachezaji katika ligi na michuano ya Europa Conference League, huku akihakikisha kikosi chake kinabaki na kasi ile ile. 

Katika mechi hii, wachezaji nyota kama Cole Palmer, Enzo Fernandez, Moises Caicedo, na Nicolas Jackson wanatarajiwa kuanza. Jackson, aliyefunga hat-trick dhidi ya Spurs msimu uliopita, anatabiriwa kuwa mwiba tena kwa safu ya ulinzi ya Tottenham. Morali ya kikosi cha Chelsea ni ya juu, na wanaonekana kuwa tayari kwa changamoto yoyote watakayopewa na Spurs.


Historia ya ushindani

Chelsea wamekuwa na rekodi bora dhidi ya Tottenham katika miaka ya karibuni. Wameshinda michezo minne kati ya mitano ya mwisho walipocheza ugenini dhidi ya Spurs, huku wakifunga jumla ya mabao 35 dhidi ya wapinzani wao wa jadi katika mechi za Ligi Kuu.

Kwa Tottenham, mechi yao ya mwisho ya ushindi dhidi ya Chelsea ilikuwa Februari 2023 walipoibuka na ushindi wa 2-0. 

Hata hivyo, Tottenham wameshindwa kuweka uimara wa safu yao ya ulinzi, wakikosa clean sheet katika michezo yao 22 ya mwisho ya nyumbani kwenye ligi, isipokuwa mechi dhidi ya Everton msimu huu.

Kwa Chelsea, rekodi zao bora dhidi ya Spurs zinaongeza presha zaidi kwa timu ya Postecoglou.


Nini kinaweza kuamua

Safu ya Ulinzi: Tottenham wakiwa na majeruhi wengi kwenye safu ya ulinzi, ni lazima wawe makini zaidi, hasa dhidi ya washambuliaji wa kasi wa Chelsea. 

Ubunifu wa Viungo: Enzo Fernandez na Moises Caicedo kwa Chelsea watakuwa muhimu katika kudhibiti mchezo eneo la kati, huku Yves Bissouma wa Spurs akitarajiwa kuonyesha ubunifu wa kiungo ili kuimarisha timu yake. 

Morali ya Kikosi: Chelsea wanakuja na morali ya ushindi, wakati Spurs wanajaribu kujiondoa kwenye hali ya mashaka.


Fulham vs Arsenal

Timu hizi zote zimepata ushindi katikati ya wiki, zinakwenda kukutana Arsenal ikiwa na rekodi nzuri dhidi ya Fulham ingawa mara ya mwisho wenyeji wa mchezo wa leo walishinda nyumbani kwao 2-1. Katika mechi 63 za michuano tofauti walizokutana, Arsenal imeshinda 42, Fulham ikishinda 9, sare 12.

Wakati Kocha Nicolas Jover akiendelea kupewa sifa kutokana na ufundi wake wa kuwanoa nyota wa Arsenal kutumia vizuri mipira ya kona na faulo, kocha mkuu wa timu hiyo Mikel Arteta anatafuta namna ya kupata ushindi wa tano mfululizo katika mashindano yote.

Kitendo cha kuifunga West Ham 5-2 katika mchezo wa mwisho, kumeifanya The Gunners kufunga angalau mabao matano kwa mara ya tano katika mechi za ugenini mwaka 2024 - hakuna klabu yoyote ya England iliyowahi kufanya hivyo katika mechi sita tofauti za ugenini kwa mwaka wa kalenda.

Fulham wamepata bao katika kila mechi kati ya 15 zilizopita kwenye michuano tofauti tangu watoke sare ya bila kufungana na Manchester United siku ya ufunguzi, ingawa pia bado wanasubiri kupata clean sheet ya kwanza nyumbani.

Vijana hao wa Kocha Marco Silva wamekuwa wagumu wakicheza mechi nane mfululizo za Premier League bila ya kupoteza.

Tangu 2001, wanaonekana kurudia tena rekodi hiyo ya kucheza mechi nane mfululizo za London Derby bila ya kupoteza ambapo mara ya mwisho walikwamia mechi ya tisa ikifungwa 3-1 na Arsenal nyumbani kwao Craven Cottage. Leo itakuwaje? Tusubiri tuone