Haller kutoka kucheza Judo, Kansa hadi shujaa wa Ivory Coast
ABDIJAN, IVORY COAST. KATIKA fainali za Afcon 2023, Ivory Coast ilikuwa moja kati ya timu ambazo hazikupewa nafasi kubwa ya kushinda taji kutokana na kiwango ilichoonyesha tangu mwanzo wa mashindano.
Lakini maajabu huwa yanatokea na hicho ndicho ilichokifanya Ivory Coast ikifanikiwa kupita kwenye nafasi ya upendeleo katika hatua ya makundi hadi kushinda taji.
Kwenye mchezo wa nusu fainali bao pekee la Sebastien Romain Teddy Haller (Sebastian Haller), katika mechi dhidi ya DR Congo ndilo liliiwezesha Ivory Coast kufanikiwa kutinga fainali ambapo pia bao la Haller la dakika ya dakika ya 81 ndilo liliiwezesha timu hiyo kuchukua taji.
Hapa tunakuletea maisha ndani na nje ya soka ya Haller aliyeanza kucheza judo kabla ya kugeukia soka ambako aliwahi kukutwa na kansa na kukaa nje miezi sita.
HISTORIA YAKE
Haller alizaliwa Ris-Orangis nchini Ufaransa, Juni 22, 1994 na mama aitwaye Simone Kuyo ambaye ni raia wa Ivory Coast, huku baba, Haller akiwa ndiye raia wa Ufaransa.
Akiwa na umri wa miaka mitatu, mama aligundua kwamba Haller ana kipaji cha michezo na alitamani mtoto wake awjiunge na Judo. Kwa sababu hiyo akiwa na umri wa miaka mitatu alimpeleka kujifunza mchezo huo.
Lakini, haja ya Haller haikuwa kucheza judo na badala yake ilikuwa mpira wa miguu, lakini mama yake alipinga suala hilo. Lakini, baada ya Haller kulazimisha sana mama hakuwa na namna zaidi ya kumruhusu aendelee na kile anachopenda na kumsapoti.
Alianza safari yake ya soka kwa kujiunga na akademi ya FCO Vigneux alikodumu kuanzia 2003 hadi 2005. Baada ya hapo alitimkia zake CS Bretigny ambapo alikaa hadi 2007 na baadaye akasajiliwa na AJ Auxerre aliyoichezea timu za vijana hadi 2012, ambapo alipandishwa kwenye kikosi cha kwanza na kuanza kucheza soka la kulipwa.
Kutokana na kiwango chake alibahatika kuchezea timu mbalimbali ikiwa ni pamoja na FC Utrecht, Eintracht Frankfurt, West Ham United, Ajax na Borussia Dortmund ambako anacheza.
KANSA YAMTESA
Baada ya kufunga mabao 34 na kutoa asisti tisa kwenye mechi 43 za michuano yote msimu wa 2021/22 akiwa na Ajax, timu vigogo Ulaya zilionyesha nia ya kutaka kumsajili. Haller hakuonekana kuwa tayari kujiunga na timu kubwa zilizomhitaji hususan zile za England na badala yake, Julai, 2022 alikubali kutua Dortmund.
Ni utaratibu kabla ya mchezaji kujiunga na timu yoyote lazima afanyiwe vipimo vya afya ili kugundua ikiwa ni mzima au la. Ilikuwa hivyo pia kwa Haller ambaye baada ya vipimo aliambiwa kwamba ana kansa kwenye sehemu zake za uzazi.
Ilikuwa ni siku mbaya kwa Haller ambapo mkewe alithibitisha kwamba walipokea taarifa hizo kwa majonzi.
Alianza kupatiwa matibabu, lakini daima hakuwahi kubweteka au kukata tamaa akiamini anaweza kupona na kuendelea kucheza soka.
Akiwa hospitali alipokuwa aki-pokea matibabu mbalimbali ikiwemo mionzi na upasuaji, lakini ndani ya meizi sita alikuwa akifanya mazoezi madogo kuhakikisha mwili wake unakuwa vziuri muda wote.
Baada ya miezi sita kupita alirejea mazoezini Januari 11, 2023 ambapo alicheza mechi ya kirafiki kati ya Dortmund na Fortuna Dussedolf ambayo ilimalizika kwa Dortmund kushinda mabao 5-1. Kisha alicheza mechi ya kwanza ya Ligi Kuu Ujerumani Januari 22, dhidi ya Augsburgm ambapo Dortmund ilishinda mabao 4-3.
KUTUA IVORY COAST
Awali, Haller alikuwa akihitaji kuichezea timu ya taifa ya Ufaransa ambalo ni taifa la baba yake na alifanikiwa kuchezea timu za vijana kuanzia za umri chini ya miaka 16 hadi chini ya miaka 21, alifanikiwa kushiriki michuano mbalimbali mikubwa ikiwemo Kombe la Dunia kwa vijana wenye umri chini ya miaka 17, mwaka 2011.
Licha kuhudumu kote huko hakubahatika kuchaguliwa kwenye timu ya wakubwa ya Ufaransa, hivyo akafanya uamuzi wa kutua zake Ivory Coast na mara ya kwanza kuichezea ilikuwa 2020 katika mechi ya kufuzu Afcon dhidi ya Madagascar ambapo Ivory Coast ikiwa nyumbani kwenye Uwanja wa Alassane Ouattara katika mechi iliyokuwa haina mashabiki ilishinda mabao 2-1.
REKODI ZAKE
Katika kabati lake kuna medali za makombe mbalimbali aliyochukua kwa nyakati tofauti. Aliwahi kushinda taji la Ligi Kuu Uholanzi mara mbili akiwa na Ajax msimu wa 2020/21 na 2021/22 ambapo alikuwa ndiye mfungaji bora akimaliza na mabao 21, na vilevile akiwa na Ivory Coast kachukua taji la Afcon likiwa ni la kwanza tangu aanze kulichezea taifa hilo.
FAMILIA
Haller yupo kwenye ndoa na mrembo Priscilla ambaye ni mwandishi wa habari waliyeanza kuwa kwenye mahusiano tangu 2012 na ilipofika 2016 walifanikiwa kupata mtoto wa kwanza na hadi kufikia sasa wamebahatika kuwa na watoto watatu.
Katika familia yao kuna watoto watatu wengine wakiwa ni mmoja wa kike na wa kiume.