Rayon yatinga nusu kibabe Cecafa, Al Hilal ikipenyea mlango mwingine
Muktasari:
- Bao pekee la mchezo huo limefungwa na Attisso Kodjo katika dakika ya 26 likiwawezesha wenyeji hao kumaliza hatua ya makundi wakiwa na pointi tisa baada ya kushinda mechi zote tatu za Kundi C.
KIGALI: RAYON Sports ya Rwanda imeendelea kuthibitisha ubora kwenye Kombe la CECAFA Kagame baada ya kutinga nusu fainali kwa rekodi ya ushindi kwa asilimia 100 kufuatia ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Al Hilal ya Sudan kwenye Uwanja wa Amahoro, Kigali.
Bao pekee la mchezo huo limefungwa na Attisso Kodjo katika dakika ya 26 likiwawezesha wenyeji hao kumaliza hatua ya makundi wakiwa na pointi tisa baada ya kushinda mechi zote tatu za Kundi C.
Rayon Sports ilionyesha ubora tangu dakika za mwanzo, ikitawala mchezo na kutengeneza nafasi kadhaa kabla ya Kodjo kufumania nyavu na kuweka bao lililodumu hadi mwisho wa mchezo.
Kabla ya ushindi huo, Rayon Sports ilikuwa tayari imezichapa KVZ ya Zanzibar na Tusker ya Kenya, hivyo kuifanya kuwa timu ya kwanza kufikisha pointi tisa katika hatua ya makundi ya michuano ya mwaka huu.
Ushindi huo umeifanya klabu hiyo ya Rwanda kumaliza kileleni mwa Kundi C na kutuma salamu kwa wapinzani wake kuelekea hatua ya nusu fainali.
Licha ya kupoteza mchezo huo, Al Hilal ya Sudan nayo imefanikiwa kutinga hatua ya nusu fainali baada ya kuwa timu iliyokusanya pointi nyingi zaidi miongoni mwa zilizomaliza katika nafasi ya pili kwenye hatua ya makundi.
Miamba hiyo ya Sudan imekusanya pointi sita, idadi inayofanana na Vipers SC ya Uganda, lakini imefaidika na tofauti nzuri ya mabao baada ya kufunga sita na kuruhusu bao moja pekee huku Vipers ikiwa imefunga mabao matano na kuruhusu mawili..
Katika mchezo mwingine wa Kundi C, Tusker ya Kenya iliifunga KVZ ya Zanzibar mabao 2-0 na kuhitimisha ushiriki wake kwa ushindi.
Kwa upande wa KVZ, timu hiyo imemaliza mashindano bila kupata pointi hata moja baada ya kupoteza mechi zote tatu ilizocheza.
Pia imeshindwa kufunga bao lolote huku ikiruhusu mabao manane, rekodi iliyoifanya kuaga michuano hiyo ikiwa miongoni mwa timu zilizokuwa na wakati mgumu zaidi katika hatua ya makundi.
Na sasa Rayon Sports na Al Hilal zinaungana na Gor Mahia ya Kenya pamoja na Jamus ya Sudan Kusini zilizofuzu hatua ya nusu fainali huku wenyeji hao wa Rwanda wakibeba matumaini ya mashabiki wao ya kutwaa ubingwa wa CECAFA Kagame wakiwa na rekodi safi ya ushindi katika hatua ya makundi.