Gyokeres apiga mbili, Arsenal ikiichapa Atletico 4-0
Muktasari:
- The Gunners ilianza mechi kwa kasi, huku shuti la Eberechi Eze lililoguswa na beki likigonga mwamba katika kipindi cha kwanza, wakati Julian Alvarez wa Atletico alipokaribia kumfunga kipa David Raya kwa shuti la mbali baada ya kumkuta akiwa nje ya eneo lake.
LONDON, ENGLAND: ARSENAL imefunga mabao manne ndani ya dakika 14 pekee ilipoichapa Atletico Madrid 4-0 na kuendeleza mwanzo wao mzuri katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, mechi ikichezwa usiku wa Oktoba 21, 2025 Uwanja wa Emirates, England.
The Gunners ilianza mechi kwa kasi, huku shuti la Eberechi Eze lililoguswa na beki likigonga mwamba katika kipindi cha kwanza, wakati Julian Alvarez wa Atletico alipokaribia kumfunga kipa David Raya kwa shuti la mbali baada ya kumkuta akiwa nje ya eneo lake.
Kipindi cha kwanza kilikuwa na tahadhari nyingi, hali ambayo iliendelea mwanzoni mwa kipindi cha pili huku mashabiki wakijiuliza bao la kwanza lingeanzia wapi.
Beki wa kati, Gabriel Magalhães alijibu swali hilo alipofunga kwa kichwa akiunganisha mpira wa adhabu uliopigwa kwa ustadi na Declan Rice dakika ya 57.
Bao hilo lilianzisha maafa kwa Atletico, kwani Arsenal iliwafanya wapinzani wao ambao kwa kawaida ni wagumu, kuteseka vilivyo.
Gabriel Martinelli aliongeza bao la pili kwa shuti la ustadi baada ya kupokea pasi kutoka kwa Myles Lewis-Skelly, kabla ya mshambuliaji Viktor Gyökeres kufunga bao lake la kwanza baada ya mechi nane akiwa na Arsenal.
Mshambuliaji huyo raia wa Sweden, alipachika bao lake la pili dakika tatu baadaye akimalizia mpira wa kichwa uliopigwa na Gabriel Magalhães kufuatia kona nyingine hatari ya Arsenal.
Matokeo hayo yanamaanisha kuwa Arsenal imeshinda mechi zake tatu za kwanza za mashindano hayo msimu huu kiwa haijaruhusu bao huku yenyewe ikifunga manane.
Arsenal imefikisha pointi tisa, sawa na PSG na Inter Milan zinazoshika nafasi ya kwanza na pili kwa tofauti ya mabao baada ya kucheza mechi tatu.
Washika bunduki hao wa London wanaokamata nafasi ya tatu kwenye msimamo wa michuano hiyo, inakuwa timu pekee sambamba na Inter Milan ambazo hazijaruhusu bao hadi sasa kati ya timu 36 shiriki.