Guardiola aachiwa msala Man City
Muktasari:
- Man City ilichapwa 2-1 na Aston Villa kwenye mchezo wa Jumamosi iliyopita na hivyo kushuka hadi nafasi ya sita kwenye msimamo wa Ligi Kuu England, huku watesaji wa kikosi hicho cha Guardiola ni wachezaji Jhon Duran na kinda wao wa zamani Morgan Rogers, huku yenyewe ikipata bao moja la kujifariji kwenye dakika za mwisho kabisa kupitia kwa Phil Foden.
MANCHESTER, ENGLAND: MANCHESTER City imeripotiwa kwamba haitamlazimisha Pep Guardiola kung’atuka kwenye kikosi hicho cha mabingwa wa Ligi Kuu England licha ya kuandamwa kwa matokeo mabaya ya vipigo mfululizo huku gwiji wa miamba hiyo akiamini hata yeye mwenyewe hata harakisha kumwaga manyanga.
Man City ilichapwa 2-1 na Aston Villa kwenye mchezo wa Jumamosi iliyopita na hivyo kushuka hadi nafasi ya sita kwenye msimamo wa Ligi Kuu England, huku watesaji wa kikosi hicho cha Guardiola ni wachezaji Jhon Duran na kinda wao wa zamani Morgan Rogers, huku yenyewe ikipata bao moja la kujifariji kwenye dakika za mwisho kabisa kupitia kwa Phil Foden.
Man City sasa imevuna pointi nne tu katika mechi nane za mwisho ilizocheza kwenye Ligi Kuu England na hivyo kutia doa mbio za kutetea ubingwa wao, huku ikiwa kwenye shaka makubwa nafasi yao ya kufuzu kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao. Miamba hiyo pia imetupwa nje kwenye Kombe la Ligi na imevuna pointi moja tu katika mechi tatu za mwisho kwenye michuano ya Ulaya na kujiweka kwenye tishio la kutolewa mapema.
Beki wa zamani wa Man City, Joleon Lescott alisema hatarajii kumwona kocha huyo aking’atuka kwa sababu mabosi wa timu hiyo hawana mpango wa kumtimua.
“Sidhani kama atajiuzulu hivi karibuni,” alisema Lescott.
“Ni mtu anayependa kukabiliana na changamoto. Atakabiliana na changamoto hii.”
“Sidhani kama anafikiria kujizulu.”
Guardiola alisaini mkataba wa miaka miwili Novemba mwaka huu na sasa kila kitu kimebaki kwake juu ya kuamua hatima yake kutokana na ukweli kwemba hakuna bosi wa Etihad mwenye mpango wa kumfungulia mlango wa kutokea kocha huyo, ambaye amebeba mataji manne mfululizo ya Ligi Kuu England.
“Nilishasema hili huku nyuma, mimi ni kocha niliyepata kila kitu nilichokuwa nakitamani, na nashukuru kwa hilo,” alisema Guardiola.
“Nina imani sasa tunaweza kuongeza mataji mengine. Hilo ndilo litakalokuwa kwenye mipango yangu.”
Man City kiwango chao kibovu kimeathiri pia ubora wa kinara wao wa mabao, straika Erling Haaland. Staa huyo wa kimataifa wa Norway amefunga mabao 10 kwenye mechi tano za kwanza za Ligi Kuu England, lakini ameongeza mabao matatu tu kwenye mechi 12 zilizofuata na amesisitiza bado wanamuunga mkono kocha wao. Haaland alisema: “Amebeba mataji sita ya Ligi Kuu England katika miaka saba, hivyo hatutasahau hilo. Atapata suluhisho. Amekuwa akifanya hivyo kila mwaka. Bado tuna imani naye, tutapambana kuliko wakati mwingine wowote.”